Thursday, October 18, 2012

BAYUME MOHAMED HUSSEIN, MTANZANIA MASHUHURI ALIYEUAWA NA HITLER.


                                Bayume Mohamed Hussein katika mavazi ya askari wa kijerumani.



ALIVYOTAJIKA.

Je, ni jina jipya?, Geni au umewahi kulisikia sehemu?. Hebu leo jipe muda kumuangalia Mtanzania huyu wa tangu na Mmashuhuri wa leo katika Ukurasa huu wa "Watanzania Mashuhuri". Hasa jina lake aliitwa Bayume Mohammed Hussein, akatajwa kuwa ni Mcheza Filamu, Askari wa Vita vile Vikuu vya Kwanza vya Dunia enzi zile za 
Ukoloni wa Kijerumani, wakati ambao unatajwa kuwa halali kwa Watoto kujiunga na Jeshi.

Huyu akawa Shujaa Mwenda Vitani aliyeondoka Tanzania kwenda Ujerumani ambako alifundisha na kueneza Lugha ya Kiswahili na pia aliigiza kama Askari katika Filamu anuai za Kijerumani. Katika kuonyesha namna alivyo mtafutaji asiyechoka, Bayume alifanya kazi zote ili kujipatia Mkate wake wa halali, amekuwa Mhudumu wa Mgahawa, amekuwa Baharia (mfanyakazi Melini), amekuwa Karani na kazi nyengine Lukuki tu.

Alikuwa Mtu mwema na aliyependa kusamehe hata kwa wale waliomtenda vibaya na kumdhulumu haki zake mbalimbali, dhulma na ufedhuli aliotendewa haukumpa vitisho wala kumrudisha nyuma siku zote katika kuvidai vile ambavyo ni haki kwake na anavistahili. Ni mtu mweneye Shukran kwa Mungu kwa Mitihani yote apewayo, alimtumaini Mungu wakati wote na hakukata Tamaa kwake hata wakati wa Misiba yake Mizito.

"Vizuri havidumu Duniani" na "Dunia ni Uwanja wa Fujo", ndizo kauli mbili sahihi ninazoweza kuzitumia kuelezea Masikito na huzuni juu ya namna Bayume Alivyouawa kwa Uchungu zaidi katika kambi ya mateso ya Sachsenhausen kwa Amri ya Bwana Mkatili Adolf Hitler kwa sababu ya Weusi wake ambao ulionekana kama ni Uduni na Ukilema.

Maisha yake yana Mengi ya kujifunza kwetu Watanzania wa sasa, yanachochea utafutaji weledi na kuzitumia fursa, yanahimiza Uchapakazi na kutokukata Tamaa, yanaonyesha upendo na utu hata kwa wale madhalimu, yanashajiisha kudai haki hata mbele ya vitisho vya kuogofya na zaidi yanatoa Mafunzo juu ya kusamehe na kutokulipiza kisasi kwa maovu utendwayo na Wanaadam wenzio. Mashuhuri Bayume Mohammed Hussein ni Mtanzania wa Kipekee.

MAZAZI YA MAHJUB ADAM MOHAMMED, WASIFU KIPANDE WA MWANADARISALAMA WA ENZI.

Bayume Muhammed Hussein aliyezaliwa Februari 22, mwaka 1904 Jijini Mzizima (Sasa Dar es Salaam) Katika Koloni la Ujerumani lililokuwa likijulikana kama German East Afrika au Mrima (Sasa Ikiwa ni Sehemu ya Tanzania) ni barobaro wa Askari mwafrika wa jeshi la kijerumani "Schutztruppe", aliyejulikana kwa jina la Adam Mohammed.

Wazazi wake wakampa jina Mahjub bin Adam Mohammed ikiwa ni ishara njema juu ya mambo yenye kufichikana (Mahjub) katika Maisha yake ya Mbeleni, tokea miaka ya mwanzoni tu ya Utoto wake akionyehs Vipawa vya kipekee katika nyanja mbalimbali jambo ambalo lilimfanya mapema tu aanze kusogezwa karibu na kila aliyemshuhudia.

KUDHIHIRI KWA VIPAWA VILIVYOFICHIKANA, UKOLONI HAUKUWA NA UTU.

Kijana Mdogo Mahjub alianza kuvidhihirisha Vipawa vyake mbalimbali vilivyojificha mapema tu, katika umri wake Mdogo tu wa miaka 9 alikuwa na Fasaha nzuri mno ya Matamshi na pia akawa na uwezo mkubwa mno katika ujuzi wa Lugha ya Kiswahili na pia Lugha ya Kijerumani, jambo ambalo lilimfanya akiwa na umri wa chini ya Miaka 10 tu aajiriwe kinyume kabisa na Haki za Mtoto wa umri wake ambaye alitakiwa aende masomoni kwanza.

Mahjub alikuwa Mbora katika mbinu kadhaa za matumizi ya lugha ya Kiswahili na uigizaji, kiasi cha kuchukuliwa Jeshini akiwa mtoto, Huko Jeshini akaanza kusoma katika shule za Serikali ambako alipata mafunzo na ujuzi zaidi juu ya Lugha, Tamaduni na Taratibu za Serikali ya Kijerumani. Baada ya Mafunzo hayo ya muda akahamia Lindi na katika Mwaka 1913 akawa anafanya kazi kama Karani katika kiwanda cha kijerumani cha Pamba kilichokuwa chini ya Bwana Karl Strecker. 

Yote haya yanaonyesha uwezo na Uchapakazi wa Mahjub katika umri wake mdogo tu lakini pia haya yanaonyesha namna Ukoloni ulivyokosa Utu na Heshima ya Kibinaadam kwa kuwatumikisha watoto wadogo ambao umri wao haukuruhusu kutumikishwa. 

VITA YA KWANZA YA DUNIA, JEMEDARI MTOTO BAYUME.

Watika wa Vita ya Kwanza ya Dunia ambayo kwa wastani iliwakusanya Askari wa "usalama wa kikosi" wa Ujerumani na Askari Mamluki kutoka katika Nchi Mbalimbali za Afrika ambazo zilikuwa Makoloni ya Ujerumani kupigana dhidi ya Askari wa Uingereza, Bayume Mohammed Hussein naye alikuwa sehemu ya Jeshi hilo la Ujerumani ambapo wakati huo alikuwa na umri wa Miaka 13 tu, Kikosi chake kilikuwa chini ya Mkuu wake Bwana Paul von Lettow-Vorbeck kama Kiongozi wa Kikosi cha Askari Watoto.

Katika "Mapigano ya Mahiwa" katika Mwezi Oktoba Mwaka 1917 Bayume Mohammed Hussein alijeruhiwa kwa risasi katika paja na akaanguka hivyo akawa ni Mateka au Mfungwa wa vita wa Jeshi la Uingereza. Kwa sababu ya Majeraha yake alitumia muda wa Miezi kadhaa akijiuguza katika Kambi ya POW Jijini Nairobi, ambapo baadaye aliachiwa huru kwa sababu ya Umri wake Mara baada ya Vita.

"MASALIA", KUTENGWA NA KUTOKUAMINIWA.

Mara Baada ya kumalizika kwa Vita vya Kwanza vya Dunia na kusababisha kumalizika kwa utawala wa kibabe wa Wajerumani jambo ambalo lilipelekea kuja kwa Wababe wapya wa Uingereza watu wote ambao waliitumika Ujerumani hasa wale wa Jeshini walianza kuangaliwa kwa Jicho baya na Wakoloni wapya wa Kiingereza. Wengi wa Wanajeshi wa zamani wa Ujerumani walionekana kama "Masalia" ya Utawala wa Kijerumani jambo ambalo liliwafanya wakososhwe fursa mbalimbali za Ajira zilizotolewa na Wakoloni wapya wa Kiingereza ambao walikabidhiwa Nchi kwa muda mara baada ya kuondoka kwa Wajerumani.

Masahibu hayo yaliwakuta watu kama Mzee Sykes Mbuwane (Baba wa Abdulwahid, Ally na Abbasi Sykes), Bayume na Askari wenziwao wa zamani. Bayume hakuonekana kuwa na fursa ya kuwajibika katika utawala wa Kiingereza ambao ulikuwa na Jukumu la Udhamini wa kuiongoza Tanganyika ya wakati huo kwa Amri ya Umoja wa Mataifa. Fursa pekee kwake ilikuwa ni dharura ya Ukosefu wa Walimu huko Zanzibar ambapo Bayume Mohammed Hussein alipewa kazi ya Ualimu, pia aliutumia wakati huo kufanya vibarua vya ziada kwa kufanya kazi ndogo ndogo katika Meli za Wajerumani na Waingereza zilizotia nanga katika Pwani ya Zanzibar.

Mwaka 1925 Bayume Mohammed Hussein alibahatika kuajiriwa katika Meli ya Shirika la Meli la German East African Line kama Mtoa Huduma wa Mgahawa wa Melini (Waiter), kazi ambayo aliifanya kwa ufanisi Mkubwa mno na kumfanya apendwe mno na Waajiri wake.

SAFARI YA KUDAI MAFAO, HAKI HAIOMBWI BALI HUDAIWA.

Kazi yake ya Kutoa Huduma katika Mgahawa wa Meli ya Shirika lile la Meli la Wajerumani ilimpa nafasi ya kuitembea na kuitalii dunia, uzoefu na mafunzo ambayo aliyapata kwa aliyoyaona katika Nchi mbalimbali alizotembelea ulimpa hamu na kumchochea kupigania Haki zake mbalimbali ambazo alidhani alistahili azipate. Mwaka 1929 aliamua kuacha Kazi kwenye Shirika hilo la Meli na Kuhamia Nchini Ujerumani alipokuwa huko Ujerumani.

Safari yake ya kuingia Ujerumani ilimletea Matatizo mwanzoni tu mara baada ya kufika kwake kwa kuwa aliingia kwenye Mgogoro Mkubwa na Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Ujerumani kwa kudai kwake mafao yaliyotokana na Utumishi wake binafsi na ule wa baba yake katika Jeshi la Ujerumani. 

Madai yake juu ya "Kiinua Mgongo" hicho yalitupwa na Ofisi ile ya Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Ujerumani kwa hoja kuwa Mafao husika yalikwishalipwa na Serikali hiyo japo yeye anadai hayakumfikia, Majawabu hayo hayakumridhisha Bayume na hivyo kumchochea kudai zaidi haki na stahili zake kiasi iliwalazimu Maafisa wale wa Ujerumani kumtishia kumrejesha Afrika kama ataendelea kudai Mafao hayo jambo ambalo halikumtisha Bayume kabisa, na yeye kuishia kuwajibu kuwa Mafao yake ni jambo moja na kurudishwa Ujerumani ni jambo jengine. Bayume mpaka anakufa hakulipwa Mafao hayo na Serikali ya Kikoloni ya Wajerumani.

USULI WA "KUPIGA BOX", NDOA NA MAPAMBANO DHIDI YA UBAGUZI, BAYUME HAKUKATA TAMAA.

Adha ya kadhia ya kuzungushwa na kuhangaishwa juu ya Mafao ya Familia yake ilianza kumchosha Bayume, gharama za kuishi nazo Ujerumani zilikuwa juu jambo ambalo lilimfanya Bayume asahau kwa muda juu ya Mafao yake na kuingia Mjini kutafuta kazi ya kufanya ili mradi apate cha kujikimu (kazi hizi ni Maarufu zaidi kwa Vijana wa Kitanzania wanaoishi Ughaibuni kama Kubeba Box au Kupiga Box). 

Bayume alipata kazi ya Uhudumu (Waiter) katika Bar Maarufu enzi hizo ya "Wild West Bar" iliyokuwa katika Eneo la Potsdamer Platz huko Jijini Berlin Tangu Mwezi Aprili 1930 mpaka alipofukuzwa Mwaka 1935. Pia kuanzia Mwaka 1931 hadi 1941 Bayume alijiongezea kipato kwa kujihimiza kuwajibika katika Idara ya Mafunzo ya Kigeni yaani "Foreign Studies Department" katika Chuo Kikuu cha Berlin kwa ajili ya lugha ya Kiswahili akiwa kama Muelekezaji na Msaidizi. 

Chuoni hapo kazi kuu ya Bayume ilikuwa ni kuwaelekeza na kuwafundisha Lugha ya Kiswahili Maafisa wa Ujerumani waliokuwa katika maandalizi ya kupanga mpango wa Ufufuo wa Tawala za Mwambao wa Makoloni ya Kijerumani yaliyoharibiwa na vita ya kwanza ya Dunia. Hayo aliyafanya kwa Mshahara kiduchu chini ya Muasisi wa Idara hiyo ya Kijerumani ya Mafunzo ya Kiafrika na Lugha za Mashariki, Bwana Mzungu wa Berlin Diedrich Westermann. 

Mwezi Januari Mwaka 1933 ikiwa ni siku Kadhaa tokea Kansela Mpya wa Ujerumani, Bwana Mkatili Adolf Hitler aingie Madarakani, Bwana Bayume alifunga ndoa na Mrembo wa Kijerumani Maria Schwadner ambapo walifanikiwa kuzaa watoto watatu katika ndoa yao, Watoto hao walikuwa ni Ahmed Adam Mohamed Hussein aliyezaliwa Mwezi Machi Mwaka 1933, na kisha bint Mziwanda aliyeitwa Anne Marie Hussein, ambaye alizaliwa mnamo September 1936. Hiyo ilikuwa baada ya mtoto wao mkubwa Bodo kuzaliwa kabla ya wenzake.

Baadae 1933 wote katika familia yake walipoteza uhalali wa ukazi wa Ujerumani, hivyo Hussein Bayume akawa na mazingira magumu katika hali ya utawala wenye ugandamizaji wa hali ya juu, alikosa kazi yake ya uhudumu kutokana na kutokuelewana na watendaji wenzake waliogoma kufanya kazi nae kwa sababu za kibaguzi, hivyo wajibu wake ukawa mgumu licha ya unguli wake katika matumizi ya lugha ya wenyeji

MASHUHURI BAYUME, KINARA MWEUSI WA KWANZA KUIGIZA FILAMU UJERUMANI.

Bayume Mohammed Hussein hakuficha kipawa chake cha sanaa ya Uigizaji na Filamu hata akiwa Ughaibuni, mara baada ya kupoteza haki zake za ukaazi wa Ujerumani fahari pekee aliyobaki nayo ni ile ya kuitwa Askari tu ikiwa ni kiashirio cha Utumishi wake kama Askari Mamluki wa Afrika kwa Jeshi la Ujerumani.

Kati ya Mwaka 1934 na 1941 Bayume aliigiza katika Filamu Maarufu 21 akiwa ndiye Mwafrika wa Kwanza kuigiza kwenye Filamu za Ujerumani, Filamu husika zilihusisha Mambo tofauti ya Kiutamaduni, Kijasusi na Kijamii ambapo mara nyingi Bayume alipenda kuigiza kama Askari katika Filamu na mara kadhaa akiigiza kama Mtapta (Mkalimani).

Filamu yake ya Kwanza ilijulikana kwa jina la "The Riders of German East Africa" ambapo Bayume alichukua nafasi kubwa tu kwenye uigizaji japo mara nyingi alipewa nafasi ndogo ndogo za maongzi kwa sababu ya Maudhui ya Filamu husika ambazo zilikuwa na muelekeo wa ubaguzi kwa Waafrika. Umahiri wake kwenye Uigizaji wa Filamu zake hasa katika Filamu ya "To New Shores" ulimpa Umashuhuri Mkubwa kiasi kupata Mashabiki sawa na Waigizaji Mashuhuri wenyeji kama Zarah Leander, Hans Albers na Willy Birgel japo akiwazidi kiasi kwa kuwa ukiacha kipaji chake kikubwa kwenye Uigizaji lakini pia alijua lugha nyingi zaidi ya waigizaji hao.

Jina la Bayume Mohammed Hussein lilitangaa zaidi na kuwazidi Umashuhuri waigizaji wenzie wengi kati ya Mwaka 1940 na Mwaka 1941 mara baada ya kutoka kwa Filamu yake Mpya ya Kipropaganda ya Nazi iliyojulikana kwa Jina la "Carl Peters". Katika Filamu hiyo Bayume aliigiza kama Bwana "Ramadan" ambaye alikuwa Mkalimani wa Kinara wa kutafuta Makoloni wa Ujerumani Bwana Carl Peters.

Filamu hiyo ilimpa Umashuhuri Mkubwa mno na kumzidishia Mashabiki wengi zaidi kuliko wale wa Mwanzoni, hii inatajwa kuwa ndiyo iliyokuwa Filamu yake ya Mwisho kuigiza kwa kuwa Upendo wa Mashabiki wake kwake (Hasa Wanawake warembo) ulimletea matatizo ambayo ndiyo kwa kiasi kikubwa yalichangia kifo chake.

"MAJANGA".

Maisha ya Bayume yaliandamwa na mengi mara baada ya utawala mpya wa Hitler kuingia Madarakani, Hisia za Machungu ya kubaguliwa katika Bar aliyokuwa akifanya kazi mwanzoni ziliibuka tena mwaka 1941 pale alipoamua kujiuzulu kazi pale Chuo Kikuu cha Berlin alipokuwa akifanya kazi kama Mtaalam wa Lugha ya Kiswahili hasa kutokana na kutendewa kinyume na utu na fedha kutoka kwa mmoja kati ya Wahadhiri pale aliyekuwa akiitwa Profesa Martin Heepe, japo pia suala la kutokupandishwa daraja la Mshahara kwa kipindi chote ambacho alifanya kazi hapo lilichangia kujiuzulu kwake. 

Machungu zaidi yalikuja kwake pale ambapo watoto wake Ahmad na Anne Marie walifariki dunia katika Umri mdogo tu na kuwaachia Bayume na Mkewe huzuni na majonzi makuu yaso mfano, Baadaye Mwanaye Mkubwa Bodo naye aliiaga Dunia kwa Mashambulizi ya Angani wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia na kuchochea zaidi upweke na majonzi kwa Familia ya Bayume.

Kukatishwa tamaa kwengine kulikuja mara baada ya kufurumuka kwa vita vya pili vya dunia, ambapo Bayume alikwenda kuomba nafasi katika Jeshi la Ujerumani ya kuruhusiwa kuwa sehemu ya wapigani wa Jeshi hilo jambo ambalo lilikataliwa mara moja na maofisa hao wa Jeshi.

"ARYAN", USALITI NA UBAGUZI. 

Filamu ya mwisho aliyoigiza Bayume ya "Carl Peters" nayo ikamuongezea Matatizo, Umahiri wake na kipaji chake kikuu cha uigizaji alichokionyesha kwenye Filamu hii kilimfanya apate mashabiki wengi zaidi ambao baadhi ya Mashabiki wake wa Kike walimtaka kimapenzi na kuitia Majaribuni ndoa yake na Mkewe. Hali hiyo ilipelekea Bayume kuanza kuandamwa na kashfa za usaliti katika ndoa yake na pia tetesi kuwa baadhi ya hao wanawake wake wa nje walipata ujauzito.

Kilele zaidi cha Kashfa zote hizo ni kuthibitika kwa Uhusiano wa Kimapenzi kati ya Bayume na Mmoja wa Mashabiki wake ambapo iligundulika kuwa sio tu walikuwa wapenzi bali Bayume alipata Mtoto kabisa na Mwanamke huyo wa kijerumani ikiwa ni usaliti wa hali ya juu kwa ndoa yake na mkewe.

Sheria za Ujerumani za wakati huo ziliruhusu Ndoa ya Mwanamke wa Kijerumani na Mwanaume Mwafrika lakini zilipinga kwa uwazi kabisa Mahusiano ya Kimapenzi kati ya Mwafrika na Mzungu bila ndoa. Wajerumani walijichukulia kuwa wao ni "ARYAN" (Waungwana) na kuwa waafrika ni watwana tu ambao hawakuruhusiwa kuwa na mahusiano na Wajerumani pasi na ndoa.

Haikuwa kazi kubwa kumkamata mtwana mkosefu katika kipindi hicho, hivyo basi katika Mwezi Agosti 1941 Bayume Mohammed Hussein alikamatwa na askari wa siri Maarufu zaidi kwa jina la “Gestapo” kwa kosa lake hilo la kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanamwali mweupe “Aryan” bila ndoa, ambapo alipelekwa kwenye kambi ya Mateso ya Sachsenhausen.

SIKU ZA GIZA NA HUZUNI, TALAKA NA KIFO.

Kukamatwa kwa Bayume hakukumpa muda mrefu wa mateso tu bali pia kulitumika kumtenganisha kwa lazima na mkewe kipenzi, chini ya shinikizo na usimamizi wa Nazi Mkewe akalazimishwa kujaza fomu za kujikhului(kudai talaka) katika ndoa yake na Mtamwa huyu mweusi. Talaka husika ilimuongezea Bayume Huzuni, Upweke, Majuto na Jakamoyo kiasi cha kumfanya kupoteza nuru ya utu wake na uchangamfu wake.

Na hayakuwa tena manufaa kwa Shujaa mwafrika, baada ya miaka mitatu katika maisha ya dhiki, tabu, mateso na dhulma nyingi katika ile ya Kambi ya Sachsenhausen ambapo mnamo terehe 24 Novembea 1944 Bayume Mohammed Hussein alisafiri safari ya milele. Safari ile kishujaa kutokana na Matokeo ya hali mbaya ya mateso kambini mwishowe iliamriwa na Kansela Hitler kuwa Bwana Shujaa wa Tanzania Bayume auawe na hivyo kuhitimishwa kwa maisha yake yenye mafunzo mengi.

BAYUME NI FAHARI YETU NA NI KIELELEZO CHA MAPAMBANO YA WAAFRIKA.

Kituo cha Utamaduni cha Ujerumani kilichopo Upanga jijini Dar es Salaam, kimeandaa filamu inayoelezea historia ya Mtanzania Mashuhuri Bayume Mohammed Hussein ikiwa ni kukumbusha Ushujaa wake na utumishi wake wa kutukuka na pia kulaani madhila na mabaya yaliyofanywa dhidi yake.

Filamu husika ilitokana na Chapisho Maarufu la Maisha ya Bayume ambali liliandikwa na Mwanazuoni Nguli wa Historia wa Ujerumani Bi Marianne Bechhaus-Gerst lililojulikana zaidi kwa jina "TRUTHFUL TILL DEATH". 

Si hivyo tu bali bali ipo Mipango tokea Mwaka 2002 ya kujenga bustani Maarufu katika Jiji la Humburg nchini Ujerumani ambayo imezungukwa na Mapambo ya sanamu kadhaa zinazotoa taswira za Askari wa Kiafrika kama Bayume ambao waliolitumika Jeshi la Ujerumani katika kipindi cha Vita kuu ya kwanza ya Dunia, Bustani husika ilipangwa kujulikana kama "Bayume Mohammed Husssein Park", likiwa ni eneo maarufu la utalii, Urafiki kati ya Ujerumani na Marafiki zake wa Afrika na kuhuisha Tamaduni za Waafrika na Historia yao ndani ya Ujerumani japo bado hilo halijakamilishwa.

Makazi ya zamani ya Bayume sasa ndio kilipo Kituo Maarufu cha Sony Center Berlin, ikiwa ni eneo Maarufu la watu kukutana, kumbi za Sinema, Migahawa na Michezo Mbalimbali ya Watoto, Mahali ambapo "Wild West Bar" ilikuwepo ilijengwa Hoteli ya Kimataifa ya Kempiski na jengo la Hotel hiyo lilivunjwa mwaka 1976.

Bayume Mohammed Hussein ni Fahari yetu Watanzania na ni Kielelezo cha Uchapakazi, Uvumilivu na Ustahamilivu, Ushupavu na Ushujaa na Weledi wa Kitanzania. Mola amlaze Pema.

Chanzo: ukurasa wa facebook ‘watanzania mashuhuri’

No comments:

Post a Comment