Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu
kwa mahujaji (2012/10/25 - 12:53)
Hamdu zote ni za Allah,
Mola Mlezi wa viumbe pia. Na rehema za Allah na salamu Zake zimfikie Mtume
Mtukufu Mwaminifu na Aali zake watoharifu, wateule na masahaba wake wema. Msimu
wa Hija uliojaa rehema na baraka umewadia na kwa mara nyingine na watu
waliofanikiwa kwenda katika miadi hii iliyojaa nuru, wamo katika kumiminiwa
baraka za Mwenyezi Mungu. Hapa, ninatoa mwito kwenu nyote mahujaji kutumia
fursa ya kuwepo mahala hapa na kuwemo katika wakati huu, kujiimarisha kimaanawi
na kimaada. Hapa, Waislamu wanaume kwa wanawake wanaitikia labeka mlingano wa
Mola wao Mkubwa wa kujipamba kwa sifa na matendo mema; kwa nyoyo na midomo yao. Hapa watu wote
wanapata fursa ya kufanya mazoezi ya kudumisha udugu, mshikamano na kujiepusha
na maasi. Hii ni kambi ya malezi na mafunzo, ni maonyesho ya umoja, adhama na
jinsi umma wa Uislamu ulivyokusanya pamoja sura za watu tofauti, ni kambi ya
kupambana na shetani na mataghuti. Hapa Mwenyezi Mungu Mwingi wa hekima na
Muweza amepafanya kuwa ni mahala ambapo waumini waweze kuona manufaa yao ndani yake.
Tutakapofungua macho yetu ya busara na ibra basi ahadi ya mbinguni itaweza
kuenea katika maisha yetu yote; ya kila mmoja wetu na ya jamii nzima. Sifa za
kipekee za amali za Hija ni kule kuchanganya kwake dunia na Akhera na
kuchanganya kwake masuala ya watu binafsi na ya kijamii. Al Kaaba isiyo na doa
na iliyotukuka; kutufu miili na nyoyo za watu katika mhimili mmoja madhubuti na
wa milele; amali ya Sai (baina ya Safa na Marwa) na kufanya jitihada za
mfululizo na za mpangilio mmoja kutoka nukta ya kuanzia hadi nukta ya kuishia;
kugura mahujaji wote kuelekea kwenye nyuga za ufufuo za Arafa na Mash'ar na
shauku na uhudhurishaji wa moyo katika Mash'ar na maqam hayo adhimu, huleta
unyofu na hali mpya, mapambano ya pamoja ya watu wote ya kukabiliana na
vielelezo vya shetani, na hatimaye kwa pamoja na kutoka kila mahala na kila
rangi na kila namna; wote wanashiriki kwa pamoja katika amali hizo tukufu
zilizojaa neema na utukufu na zilizojaa maana na ishara za uongofu. Sifa za
kipekee za faradhi hii zimejaa maana na madhumuni. Ni amali kama hii ndiyo
ambayo inauunganisha moyo na kumkumbuka Mwenyezi Mungu, na kuujaza nuru na kuunawirisha
upweke wa moyo wa mwanadamu kwa imani na taqwa na wakati huo huo kumvua
mwanadamu kutokana na mzingiro wa ubinafsi na kumsahilishia mambo katika jamii
iliyopambika kwa sura za kila namna, ya umma wa Kiislamu na kumvisha nguo ya
kujiepusha na madhambi ambayo huilinda roho yake kutokana na mashambulizi
yaliyojaa sumu ya mashambulizi na vile vile humuongezea nguvu na moyo wa
kupambana na mashetani na mataghuti. Ni mahala hapo ndipo ambapo hujaji
anapoweza kuonana na Waislamu wenzake wengi wanaunda umma mkubwa wa Kiislamu na
kuona kwa karibu nguvu na uwezo wa umma huo na hivyo kupata matumaini kuhusu
mustakbali mwema na vile vile kupata hisia za wajibu wa kutoa mchango wake wa
kuimarisha umma huo na pia kama atapata taufiki na msaada wa Mwenyezi Mungu
aweze kutoa bay'a na kutangaza utiifu wake kwa Mtume (Muhammad) Mtukufu wa
daraja na kufunga mithaki na ahadi imara kwa Uislamu azizi na kutia nia ya
kweli ya kuijenga kiimani nafsi yake, kuleta marekebisho katika umma na kutia
nguvu neno la Uislamu. Mambo yote haya mawili, yaani kuijenga nafsi na kuujenga
umma (wa Kiislamu) ni faradhi zisizoishiwa na wakati na wala zisizofungwa. Njia
za kuweza kufanikisha faradhi hizo mbili si nzito kwa watu wenye mazingatio na
wanaoangalia mambo kwa kina katika utekelezaji wa majukumu ya kidini na kutumia
vizuri akili, tabasuri na wenye mtazamo wa mbali. Kujenga nafsi huanzia kwenye
kupambana na hisia za kishetani na kufanya juhudi za kujiepusha na madhambi na
kujenga umma huingia sura kwa kumjua adui na njama zake, kufanya jitihada za
kupelekea mashambulizi, hadaa na uadui wa maadui usiwe na athari zozote na hadi
kufikia kwenye kuziunganisha nyoyo na mikono pamoja na lugha za matabaka yote
ya Waislamu na mataifa yote ya Kiislamu. Katika wakati huu tulio nao hivi sasa,
moja ya masuala muhimu zaidi ya umma wa Kiislamu ambalo lina mfungamano (wa
moja kwa moja) na mustakbali wa umma wa Kiislamu, ni matukio ya mapinduzi
katika nchi za kaskazini mwa Afrika na katika eneo la Mashariki ya Kati ambayo
hadi sasa yameshapelekea kuanguka tawala kadhaa fasidi na vibaraka wa Marekani
na waitifaki za Uzayuni na kuzitikisa tawala nyingine kama hizo. Kama Waislamu
watapoteza fursa hii adhimu na iwapo watashindwa kutumia fursa hii katika
kuujenga vizuri na kuleta marekebisho kwenye umma wa Kiislamu, basi watakuwa
wamepata hasara kubwa. Hivi sasa mabeberu wavamizi na waingiliaji wa masuala ya
ndani ya mataifa mengine wanafanya juhudi zao zote kujaribu kupotosha harakati
hizo adhimu za Kiislamu. Katika harakati hizo kubwa, Waislamu wake kwa waume
wamesimama kupambana na ukandamizaji wa watawala (wao madhalimu) na kupambana
na udhibiti wa Marekani ambao umepelekea kudhalilishwa na kudunishwa mataifa ya
Waislamu na kusababisha kushuhudiwa ushirikiano baina ya tawala za nchi hizo na
utawala mtenda jinai wa Kizayuni. Waislamu wamegundua kuwa kitu kinachoweza
kuwaokoa katika mapambano haya ya kufa na kupona ni Uislamu, mafundisho ya dini
hiyo tukufu na nara na kaulimbiu zake zenye
uwokovu na hilo
wamelitangaza wazi wazi. Ajenda yao
kuu wameifanya kuwa ni kulitetea taifa madhulumu la Palestina na kupambana na
utawala ghasibu (wa Kizayuni). Wamenyoosha mkono wa urafiki kwa mataifa yote ya
Waislamu na wanataka kuona umma wa Kiislamu unashikamana na kuwa kitu kimoja.
Hii ndiyo misingi mikuu ya harakati za wananchi kwenye nchi ambazo katika
kipindi cha miaka miwili iliyopita, wananchi wake wamenyanyua bendera ya uhuru
na mabadiliko na kujitokeza kwa viwiliwili na roho zao kwenye medani za
mapinduzi na ni mambo kama haya ndiyo
yanayoweza kuwa misingi mikuu ya kuleta marekebisho katika umma mkubwa wa
Kiislamu. Kusimama imara na kushikamana vilivyo na misingi mikuu ni sharti la
lazima la kuweza kupata ushindi wa mwisho wa harakati za wananchi kwenye nchi
hizo. Lengo la adui ni kutaka kuhakikisha anateteresha misingi hii mikuu.
Mikono fasidi ya Marekani na NATO na Uzayuni inatumia baadhi ya mighafala na
mitazamo finyu kujaribu kupotosha wimbi la harakati ya vijana Waislamu na
wanatumia jina la Uislamu kuwagombanisha Waislamu na wanaiita jihadi ya
kupambana na ukoloni na Uzayuni kuwa ni ugaidi usio na macho katika ulimwengu
wa Kiislamu ili Waislamu wauane wao kwa wao na hivyo maadui hao wa Uislamu
waweze kuokoka na Uislamu na wanajihadi wake watazamwe kwa sura mbaya na chafu.
Baada ya maadui kukata tamaa kwa kuona kuwa hawawezi kuushinda Uislamu wala
kuzima nara na
kaulimbiu zake, hivi sasa wameamua kuzusha fitna kati ya makundi tofauti ya
Waislamu na wanafanya njama za kueneza chuki dhidi ya Ushia na chuki dhidi ya
Usuni ili kuzuia kupatikana mshikamano na umoja katika umma wa Kiislamu. Maadui
wanawatumia vibaraka wao katika eneo (la Mashariki ya Kati), kuzusha mgogoro
nchini Syria
ili kuzishughulisha akili za mataifa ya dunia na kuzifanya zisahau masuala
muhimu ya nchi zao na zisahau pia hatari zinazowakabili. Maadui hao wanajaribu
kuwashughulisha (Waislamu) na masuala ya umwagaji wa damu ambayo maadui
wameyazusha wao wenyewe. Vita vya ndani nchini Syria na kuuliwa vijana wa Kiislamu
kwa mikono ya Waislamu wenzao ni jinai ambazo zilianzishwa na Marekani na
Uzayuni na tawala tiifu kwa maadui ambazo wanazidi kuchochea moto huo. Nani
anaweza kuamini kuwa, tawala ambazo zilikuwa waungaji mkono wa madikteta waovu
wa Misri na Tunisia na Libya, hivi sasa wamekuwa waungaji mkono wa
kutaka demokrasia taifa la Syria?
Kadhia ya Syria ni suala la
kulipiza kisasi dhidi ya utawala wa nchi hiyo ambao katika kipindi cha miongo
mitatu ulikuwa umesimama peke yake kupambana na Wazayuni maghasibu na kuyaunga
mkono makundi ya wanamuqawama wa Palestina na Lebanon. Sisi tunaliunga mkono taifa
la Syria
na tunapinga uchochezi na uingiliaji wa aina yoyote ile wa kigeni nchini humo.
Marekebisho ya aina yoyote ile nchini humo inabidi yafanywe na wananchi wenyewe
na kwa kutumia njia zinazokubaliwa kikamilifu na wananchi wa taifa hilo. Hatua ya mabeberu
wa kimataifa ambao kwa msaada wa tawala za vibaraka wao katika eneo hili
wanatumia kisingizio cha kuenea mgogoro na wakati huo huo kutumia kisingizio
cha kuweko mgogoro kuhalalisha kufanya kila aina ya jinai nchini humo ni hatari
kubwa ambayo kama tawala za eneo hili hazitajiepusha nayo basi inabidi zisubiri
zamu yao ifike ya kukumbwa na hadaa hizo za kibeberu. Makaka na madada! Msimu
wa Hija ni fursa ya kutaamali na kuyaangalia kwa kina masuala muhimu ya
ulimwengu wa Kiislamu. Hatima ya mapinduzi ya eneo hili na juhudi za madola
makubwa yaliyojeruhiwa kutokana na mapinduzi (ya wananchi wa eneo hili) za
kutaka kuyapotosha mapinduzi hayo ni miongoni mwa masuala hayo (muhimu ya
ulimwengu wa Kiislamu ambayo inabidi kuyaangalia kwa kina). Njama za wasaliti
za kutaka kuzusha hitilafu kati ya Waislamu na kuleta ugomvi na suutafahumu
kati ya nchi ambazo zimeamua kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu; kadhia ya
Palestina na juhudi za kuifanya itengwe na kuizima jihadi ya Wapalestina;
propaganda za kueneza chuki dhidi ya Uislamu zinazofanywa na tawala za
Magharibi na uungaji mkono wa tawala hizo kwa watu wanaomvunjia heshima Mtume
Muhammad SAW; kuandaa mazingira ya kuzuka vita vya ndani na kugawanywa vipande
vipande baadhi ya nchi za Waislamu; kuzitisha tawala na wananchi wa nchi za
Kiislamu zilizofanya mapinduzi kuhusiana na hatari za kupinga siasa za kibeberu
za Magharibi na kueneza dhana potofu kuwa mustakbali wao unategemea
kujisalimisha kwao mbele na madola ya kibeberu na masuala mengine muhimu sana
kama hayo, ni miongoni mwa kadhia muhimu ambazo inabidi ziangaliwe kwa taamuli
na kwa mazingatio makubwa katika fursa inayopatikana kwenye Hija na chini ya
kivuli ya kupendana na kuwa na fikra moja nyinyi mahujaji. Wassalaamu Alaykum
Warahmatullahi Wabarakaatuh. Sayyid Ali Khamenei, 30/Mehr/1391 (Hijria Shamsia)
inayosadifiana na tarehe tano Dhulhijjah 1433 Hijria.
No comments:
Post a Comment