MONDAY, OCTOBER
15, 2012
Spika wa Bunge Anna Makinda ndani ya wiki moja atumie madaraka
na mamlaka yake kutangaza kwa umma kamati nyingine ya kudumu ya Bunge
itayoshughulikia masuala ya gesi asili kabla na wakati wa mkutano wa tisa wa
Bunge uliopangwa kuanza tarehe 30 Oktoba 2012 kufuatia hali tete na tata kuhusu
sekta ndogo ya gesi asilia nchini na kwa kuzingatia umuhimu na unyeti wa sekta
hiyo katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.
Pamoja na mambo mengine aelekeze kamati hiyo kupokea na
kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge ya mwaka 2011 kuhusu Sekta
Ndogo ya Gesi Asili ikiwemo juu ya hatua iliyofikiwa katika kushughulikia
tuhuma za ufisadi, madai ya mapunjo ya fedha za mauzo ya Gesi asili na hatua
iliyofikiwa katika maandalizi ya sera, mpango mkakati na sheria ya gesi asili.
Hatua hii ni muhimu kufuatia ukimya wa Waziri wa Nishati na
Madini Prof. Sospeter Muhongo kuhusu kauli yangu ya tarehe 4 Oktoba 2012 ya
kutaka Taarifa ya ufafanuzi kuhusu utafutaji wa mafuta na gesi asili nchini
iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini tarehe 21 Septemba 2012 ifutwe kwa
kuwa italinda ufisadi na kukwaza utetezi wa rasilimali za taifa.
Taarifa hiyo ya Wizara ya Nishati na Madini ilieleza kuwa
maandalizi ya sera ya gesi asili yapo katika hatua za mwisho wakati ambapo
kamati mbalimbali za kudumu za Bunge hazijahusishwa katika mchakato huo muhimu
pamoja na kuwa mamlaka ya kutunga sera kwa mfumo wetu wa sasa ni ya Baraza la
Mawaziri hata hivyo kwa unyeti na upekee wake sera ya gesi Spika wa Bunge
anapaswa kuwezesha Kamati za Kudumu za Bunge zihusishwe ili pawepo mashauriano
na maridhiano kwa mapana na marefu.
Taarifa hiyo ya Wizara ya Nishati na Madini ilieleza kuwa
mikataba 26 ya TPDC ni sehemu ya nyaraka muhimu za kuboresha utayarishaji wa
sera ya gesi asili, hata hivyo mikataba hiyo imeendelea kuwa siri hivyo Spika
aingilie kati kuziwezesha Kamati za Kudumu za Bunge kuisimamia serikali
kurekebisha mikataba ya sasa na kuboresha mikataba ijayo kwa Serikali
kutekeleza mwito wangu wa toka mwaka 2011 wa kutaka mikataba hiyo iwasilishwe
bungeni na iwekwe wazi kwa umma.
Izingatiwe kwamba katika Mkutano wa Nane wa Bunge Spika
alitangaza kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imevunjwa na
kwamba majukumu yaliyokuwa yakishughulikiwa na kamati hiyo yatashughulikiwa na
kamati nyingine kwa mujibu wa madaraka na mamlaka ya Spika.
Irejewe kwamba kwa mujibu wa Kanuni ya 116 na Kanuni ya 114
fasili ya 14 Spika ana mamlaka na madaraka ya kukabidhi mambo mengine
yashughulikiwe na Kamati ya Kudumu ya Bunge nyingine kama
atakayoelekeza.
Ikumbukwe kuwa Julai 2011 na Julai 2012 kwa nafasi yangu ya
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini na kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani
nilieleza namna nchi yetu ilivyojaliwa utajiri wa gesi asilia katikati ya lindi
la umasikini wa wananchi na kwamba taifa letu lina fursa ya kuwa nchi kiongozi
katika gesi Afrika na kushindana kimataifa ikiwa tutaweka mstari wa mbele upeo,
umakini na uadilifu katika sekta ya nishati kuepusha laana ya rasilimali.
Hata hivyo, mapitio ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2011/2012
yanaonyesha bado serikali haichukui hatua thabiti kushughulikia ufisadi na
udhaifu wa kiuongozi katika sekta ndogo ya gesi asili hivyo hatua za
haraka zisipochukuliwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 na kuendelea
rasilimali inaweza kuwa chanzo cha migogoro na kuhatarisha pia usalama wa
nchi.
Kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani nilieleza bungeni tarehe 15
Julai 2011 kuhusu tuhuma za ufisadi na ukiukwaji wa mikataba katika sekta ndogo
ya gesi inaoihusu pia Kampuni ya Pan African Energy Tanzania (PAT) na kutaka
kuundwa kwa kamati teule ya bunge kuchunguza suala hilo .
Badala yake Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini
uliunda kamati ndogo ya iliyofanya uchunguzi uchunguzi wa masuala husika na
taarifa kuwasilishwa bungeni mwaka 2011 ; hata hivyo mpaka sasa maamizio ya
bunge kufuatia taarifa hiyo hayajatekelezwa kwa ukamilifu.
Tarehe 27 Julai 2012 kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani
niliitaka Serikali kueleza ni kwanini mpaka sasa kiasi cha dola milioni 20.1
zilizopunjwa kifisadi hazijareshwa na kuitaka serikali iache kutumia kisingizio
cha kuundwa kwa Timu ya Majadiliano (GNT) kuchelewesha utekelezaji wa maazimio,
suala ambalo Wizara ya Nishati na Madini itapaswa kueleza hatua iliyofikiwa
iwapo Spika atazingatia mwito huu na kuchukua hatua za haraka.
Ifahamike pia kwamba mwaka 2011 kwa nafasi yangu ya Waziri
Kivuli wa Nishati na Madini niliitaka serikali ambazo kuweka wazi bungeni
na kwa umma mikataba ya madini, mafuta na gesi asili katika nchini ili
kuongeza tija na uwajibikaji.
Aidha nilitoa mwito mwito kwa wananchi na wabunge kuongoza
marekebisho ya kikatiba na kisheria ili kuweka vifungu vya kulazimisha uwazi
katika mikataba katika hizo muhimu kwa uchumi na usalama wa nchi.
Uwazi katika mikataba utadhibiti pia mianya ya ufisadi miongoni
mwa baadhi ya watendaji wa serikali kwa kuwa mikataba hiyo itajadiliwa na umma
na hivyo kupunguza uwezekano wa viongozi kutanguliza maslahi binafsi na kuwa na
mikataba bora ya baadaye yenye kuzingatia maslahi ya umma.
Usiri katika mikataba ni tatizo kwa sababu masharti kama ya
kushughulikia madhara ya kimazingira na kuchangia katika huduma za jamii pamoja
na kulipa kodi zinazokusudiwa yanaweza yasitekelezwe kwa ukamilifu kama
hayatafahamika kwa wabunge na umma. Aidha, ipo mikataba yenye vifungu ambavyo
vinakinzana na sheria nyingine ama vinalinda kupindukia makampuni dhidi ya
sheria nyingine za nchi zinazotungwa masuala ambayo yanaingilia mamlaka ya
bunge ya kutunga sheria na kuisimamia serikali.
Sheria mpya ya madini Tanzania ya mwaka 2010 ina kifungu
kinachotaka uwazi hata hivyo kimejikita katika uwazi wa rekodi na ripoti
hakijaweka bayana mfumo wa uwazi katika mikataba ya madini, sheria
ya mafuta nayo haina kifungu cha uwazi katika mikataba na sheria ya gesi haipo kabisa;
hali ambayo inahitaji kurekebishwa.
Pamoja na mapato uwazi katika mikataba utachangia katika kupata
tija ya ziada katika uchimbaji kwa kulinda maslahi ya wafanyakazi na kuweka
mfumo mzuri zaidi wa makampuni kununua bidhaa za ndani kwa majibu wa vifungu
vya mikataba hali ambacho itawezesha rasilimali kunufaisha wananchi wengi zaidi.
Uwazi katika mikataba utawezesha wabunge na wadau wengine
kusimamia ipasavyo taasisi za kiserikali kuhusu mifumo ya kifedha na kibenki
ambayo itaongeza mchango wa sekta za nishati na madini katika kuimarisha
uchumi kwa kudhibiti mfumuko wa bei na kuporomoka kwa sarafu wakati huu ambapo
thamani ya mauzo imeongezeka duniani lakini mzunguko umejitika katika masoko na
mabenki ya nje. Kwa ujumla, uwazi katika mikataba utapanua pia uwajibikaji wa
kuongeza umiliki wa nchi na wananchi wa michakato ya utafutaji na uchimbaji wa
mafuta na gesi asili.
Pamoja na kuwa ibara ya nne ya katiba inasema kwamba rasilimali
na mali asili zote ziko chini ya usimamizi wa serikali; na ibara ya 63 inaeleza
kwamba bunge ndicho chombo kikuu cha kuisimamia serikali kwa kutunga sheria na
kupitisha mipango, katiba haijalazimisha mikataba ya madini, mafuta na gesi
kuridhiwa na bunge hivyo katika kipindi cha sasa mikataba hiyo iwasilishwe kwa
rejea na mapitio.
Katika muktadha huo, tarehe 4 Oktoba 2012 nilimtaka Waziri wa
Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo afute taarifa iliyotolewa na Katibu
Mkuu wa wizara hiyo kuwa lengo la agizo lake la kupitiwa kwa mikataba yote 26
ya utafutaji mafuta na gesi asili ni “kuhakikisha kwamba endapo kuna mapungufu
katika mikataba hiyo, mapungufu hayo yasijirudie tena katika mikataba mipya ya
baadaye” kwa kuwa ikiachwa ilivyo italinda ufisadi na kukwaza utetezi wa
rasilimali za taifa.
Nilieleza kwamba ufafanuzi uliotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini unatoa mwanya kwa mikataba mibovu kulindwa wakati ambapo
kuna madai tuliyotoa toka mwaka 2011 kwamba baadhi ya mikataba hiyo imeingiwa
kifisadi na mwaka huu wa 2012 zimeibuka tuhuma za vigogo wa serikali kuingiziwa
fedha kifisadi katika akaunti zao za nchini Uswisi na makampuni ya nje ya
utafutaji mafuta na gesi asili.
Aidha, pamoja Serikali kuwasilisha bungeni mikataba inapaswa pia
kuwasilisha mipango kabambe (master plan) ya mafuta na gesi asili yenye
kuzingatia mabadiliko ya kisera na kimfumo yenye kuwezesha nchi na wananchi
kunufaika na rasilimali husika.
Kauli hii nimeitoa leo tarehe 14 Oktoba 2012 ikiwa ni Siku ya
Kumbukumbu ya Hayati Julius Nyerere ambaye alipinga ufisadi na kutaka
rasilimali za nchi zitumike kwa manufaa ya maisha ya wananchi:
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
No comments:
Post a Comment