Sunday, October 14, 2012

Miaka 13 tangu kufariki Mwalimu Nyerere...

JULIUS KAMBARAGE NYERERE, MWANAADAM MWENYE KIPAWA ALIYEJENGWA NA KUANDALIWA NA WENGI.

MWENYE KIPAJI ALIYEANDALIWA NA KUUNDWA KWA UHUNZI WA KIPEKEE.

Leo ni Maadhimisho ya Miaka 13 tangu Kifo cha Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kifo ambacho kiliacha Majonzi na Simanzi kubwa miongoni mwa Watanzania wengi kama si wote.

Nyerere alikuwa Kiongozi wa watu, mtu mwadilifu na mchapakazi ambaye siku zote aliwapigania kwa dhati watanzania masikini wakomboke kutoka katika tope la umasikini walilozama. Uadilifu wake wakati wa uongozi wake na hata mara baada ya Uongozi ni jambo ambalo halina mfano.

Nyerere alikuwa Mwanaadam na hakuna Malaika, anayo makosa pia lakini yalizidi yale mema yake na mara zote alituasa Watanzania tuache yale mabaya ya Uongozi wake na Wazalendo wenziwe na tuige tu yale mema ya wakati wa Uongozi wao.

Ukurasa wa "WATANZANIA MASHUHURI" unamtazma Mwalimu Julius K Nyerere kama Kiongozi aliyekuwa na Kipawa Kikuu cha Uongozi kilichotambuliwa na wenziwe ambao walifanya kila juhudi kukiongeza Busara na Hekima, kukilinda kwa kila hali, kukitanguliza mbele na kukipa fursa, kukipa nafasi ya kudhihiri na kuenenda katika ukilele wake na pia kukiheshimu.

Watanzania hao Wazaledo wenzake wa zamani walikithamini sana Kipawa hiki kiasi Uhunzi wao katika kukiunda umetupa Kiongozi Bora aliye na Kipaji cha Kipekee cha Uongozi ambacho hakijawahi kutokea tena Tanzania Mpaka leo.

"NDOVU AKAVIRWA WIMA", NYERERE ALIPENDWA NA KILA MTU.

Mwaka 1958 kilianzishwa Chama cha Washairi Tanganyika ili kuwajajiisha Washairi kutunga na kutoa Diwani zao na pia kutumia Sanaa na Kazi za Ushairi katika kuhamasisha Mapambano ya kudai Uhuru. Mkutano wa Kuunda Chama hicho cha Washairi uliundwa na Magwiji kama Sheikh Amri Abedi Kaluta, Martias Mnayampala, Hemed Feruz Mbiyana, Dr. Lyndon Harris na Wengineo

Katika Mkutano huo Mwenyekiti wa Chama alichaguliwa kuwa Mahmood Hamduni (Jitu Kali) na Kamati ya Wataalamu wa Uchunguzi na Utafiti wa Lugha walichaguliwa Shaaban Robert, Saadan Abdu Kandoro na Sheikh Kaluta ambapo moja ya kazi Bora za kutumia Ushairi kupinga Ukoloni waliyoifanya ni Shairi lifuatalo.

Shairi hili liliitwa "NDOVU AKAVIRWA WIMA, SISIMIZI AKAKWAMA". Shairi husika lilitungwa kuwazungumzia MaDC ambao walitumia nafasi zao kujipendekeza kwa Utawala wa Kikoloni kwa kuwabughudhi Viongozi wa Tanu na kumkashifu Nyerere ambapo Nyerere alipowajibu walimfungulia Mashtaka Mahakamani. Nisiwachoshe kwa Maneno Furahieni Shairi husika na sote tutafakari kuwaunda Viongozi wetu tunaotoka watuongoze.

Mambo ya Kale na Leo, pindi ukiyatizama,
Kwa juu maogeleo, au kwa mbizi kuzama,
Ni ajabu kumbweneo, Panda za mti kuchama,
Ndovu akavirwa wima, sisimizi akakwama!

Tobo lilivyaa tata, na tembe ilisakama,
Tanganyika na Mvita, jikumbateni matama,
Na Unguja nawaita, panda za mti kwachama,
Ndovu akavirwa wima, sisimizi akakwama!

Mwanambiji mzingile, zinguo ni makarama,
Vyambile zilungupule, vyawataka Mahukama,
Msambe kitukumile, panda za Mti kwachama,
Ndovu akavirwa wima, sisimizi akakwama!

Tambo ni hii yatamba, tambueni Maulana,
Kuitoa mkizimba, si kuimba lelemama,
Si uto wa kuku temba, panda za mti kwachama,
Ndovu akavirwa wima, sisimizi akakwama!

Ajabu Ndovu avirwe, pasi jani kutetema,
Kuja apite Nyerere, kazua nyamttitima,
Wakashangaa ngedere, panda za mti kwachama,
Ndovu akavirwa wima, sisimizi akakwama!

Iwapo umfunguzi, fungulia kilokwama,
Uwapo ni mchukuzi, zigo hili kwa likwama,
Ufumbue ufumbuzi, panda za mti kwachama,
Ndovu akavirwa wima, sisimizi akakwama!

Saba hizi abuyati, atangze kiloloma,
Atilie tashtiti, zijibiwe na Ulama,
Kisa cha panda za mti, panda zilizoachama,
Ndovu akavirwa wima, sisimizi akakwama!

Katika Shairi Husika Nyerer ametajwa kama Sisimizi na DC ametajwa kama Tembo, Shairi hili hupatikana katika Kitabu "Almasi ya AFRIKA: Maisha ya Sheikh Kaluta Amri Abedi".

Ulale Pema Julius Kambarage Nyerere.

Chanzo: Watanzania mashuhuri facebook page.

No comments:

Post a Comment