Thursday, October 25, 2012

Msiba hauna kadi wala mwaliko....

                   Nilipofika Korogwe nilianzia Masuguru kuangalia Ngombe wa babu Katani..
 Hizo picha za juu watu hawaziki,bali ni vijana wanaandaa kaburi. nami nilishiriki kuandaa kaburi la dada Mwanasha. Nilifurahishwa sana na maisha ya wakazi wa Korogwe, hakuna kuwalipa wachimba makaburi. Mtu akipatwa na msiba vijana wote katika kijiji wanapigiwa mbiu na kuelekea makaburini kuchimba kaburi, wanachopewa ni ndoo ya maji, uji ama chai. safi sana, Mjini huku kaburi maka uwe na laki moja au zaidi.

 Hapanilikuwa naandaa jeneza la dada, naam waislam hatuagi maiti. Ila kuna kitu kinaitwa kupamba jeneza, unalifunika jeneza kwa shuka na vitambaa, kama ni la mwanamke linawekwa khanga, kama ni la mwanaume linawekwa shuka tupu. Nilijifunza juzi mambo hayo. Ndiyo raha ya kukaa karibu na wazee.

 Huyo mnene kabisa ni mdogo wetu sote wawili hapo. Anaitwa Mustapha, mtoto wa mama mkubwa, baba yake ndie aliekuwa mmiliki wa ile hoteli maarufu Korogwe ya 'River Side' kwa waliopita Korogwe lazima wanaijua Hoteli ile maana ipo barabarani kabisa karibu na gereza la korogwe.

 Mapacha watatu, wa kwanza kutoka kushoto ni mtoto wa mama mkubwa anaitwa Hussein Ally, wa pili ni dogo langu Juma Kido na wa tatu ni jembe mwenyewe, baada ya mazishi tukaamua kujipumzisha kidogo. Korogwe pamekuwa pazuri jamani.

Tatizo la mdogo wangu huyu Juma Kido, akipata upenyo kidogo anauchapa usingizi..........


Ndugu zangu,

Ukisikia mtu anasema maiti ya mwenzio gogo wala usimlaumu. Maana juzi nilipata msiba wa dada bila ya kutegemea. Nikiwa katika mizunguko yangu kaka mtoto wa shangazi akanipigia simu kuniuliza nyumbani kijitonyama kuna nini?

Nikawa sijui kitu, nikampigia mdogo wangu wa kike Nafisa Kido, huku analia akanambia dada Mwanasha ameletwa nyumbani akiwa maiti. Awali sikumuelewa,na kichwani nikawa nimechanganyikiwa. Nilichofanya ni kukatisha mizunguko yangu na kurudi nyumbani.

Nilipofika nikamkuta mjomba Selemani Katani (baba mmoja na mama yangu mzazi Rehema Katani). Akiwa nyumbani amejiinamia macho yamemuiva kwa kulia; naam ukimuona mtu mzima analia ujue kuna jambo.

Nikapatwa na dukuduku rohoni, machozi ya mwanaume yapo mbali sana hasa baada ya kugundua mimi ndie kaka pekee pale nyumbani. Nyumba nzima wanaume tulikuwa mimi na mjomba. Hivyo kulia ni udhaifu.

Mwanasha Selemeni Juma Katani, ni mtoto wa mjomba, alikuwa ni mdogo kwangu kwa miaka zaidi ya mitano. Lakini kwa kuwa ni mwanamke anakuwa mkubwa, maana tayari alishazaa watoto wanne, wa mwisho ni mdogo ana miezi chini ya sita. Na ndie aliesababisha kifo chake.

 Ndivyo, hakutakiwa kubeba ujauzito kwa mujibu wa daktari, lakini kwa bahati mbaya ama nzuri akapata ujauzito mwingine kutoka kwa mumewe wa halali kabisa. Alijifungua kwa taabu sana tena baada ya kuwahishwa na gari ya wagonjwa kutoka Hospitali ya Korogwe- Magunga kuenda Bombo Tanga mjini.

Tangu siku hiyo alisumbuliwa na moyo mkubwa, mauti yalimkuta ndani ya gari akipelekwa Hospitali ya Muhimbili Dar es Salaam kupata matibabu. Alitoka Korogwe siku ya jumanne, nadhani mitikisiko ya safari ilisababisha mauti yake.

Wakati anashushwa kutoka ndani ya Basi la Burudani ili apakiwe katika Tax kuelekea Hospitali moja kwa moja. Ndipo roho ikaacha mwili, ikabidi safari ya hospitali iahirishwe maiti apelekwe nyumbani Kijitonyama alimaua.

Baada ya hapo kilichofuata ni kusafirisha maiti kwa ajili ya maziko mjini Korogwe eneo la Masuguru. Mungu ailaze roho ya marehemu.

HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM, TANZANIA
0713 593894/ 0752 593894
25/10/2012  


No comments:

Post a Comment