Huyu mama anatoka idara ya habari Maelezo, namkubali sana katika suala zima la upigaji picha.
Mwenyekiti akisisitiza jambo wakati akijibu maswali magumu ya wanahabari.
Wanahabari wakiwa kazini katika mkutano huo leo asubuhi.
Na Hafidh Kido
Ripoti ya tume ya haki za
binaadamu na utawala bora nchini imebaini kulikuwepo na uvunjifu wa amani
katika tukio zima lililosababisha kifo cha mwanahabari Daudi Mwangosi mjini Iringa
miezi michache iliyopita.
Akizungumza jijini Dar es
Salaam leo asubuhi wakati wa kutoa muhtasari wa matokeo ya uchunguzi wa tukio
hilo lililotokea Septemba 2, mwaka huu katika kijiji cha Nyololo mjini Iringa
mwenyekiti wa tume hiyo jaji kiongozi mstaafu Amiri Manento, alisema uchunguzi
wao ulibaini kuwepo kwa uvujifu wa haki za binaadamu na mikataba ya kimataifa
na kikanda inayohusu amani.
“Tume imejiridhisha kuwa
tukio lililopelekea kifo cha Daudi Mwangosi limegubikwa na uvunjwaji wa haki za
binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora. Kwa mujibu wa katiba ya nchi
yetu eneo la sheria za makosa ya jinai, azimio la kimataifa la haki za
binaadamu, mkataba wa kimataifa kuhusu haki za kiraia na kisiasa na mkataba wa kimataifa kuhusu haki za kiraia na kisiasa pamoja na mkataba wa mataifa ya Afrika kuhusu
haki za binadamu na watu.
“Kutokana na mikataba yote
hiyo tume imeona kuwa jeshi la polisi katika tukio lile limevunja haki
zifuatazo: haki ya kuishi, haki ya kutoteswa na kupigwa, haki ya usawa mbele ya
sheria na haki ya kukusanyika na kutoa maoni,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo
ambayo imeshakabidhiwa kwa serikali kwa mujibu wa mwenyekiti wa tume hiyo.
Aidha kwa mujibu wa jaji
Manento, mkutano wa kufungua matawi mawili ya chama cha chadema mjini Iringa
ilipata ruhusa ya kamanda wa polisi wa wilaya ya Mufindi ambae ndie alikuwa
‘officer in-charge’ wa polisi wa eneo husika kama sheria inavyotaka lakini siku
iliyofuata RPC wa Iringa alikataza mikutano hiyo kinyume na taratibu.
“Uchunguzi umebaini kuwa
kamanda wa polisi mkoa wa iringa Michael Kamuhanda katika utekelezaji wa
majukumu yake alikiuka sheria ya vyama vya siasa (Cap 258 RE.2002) kifungu cha
11(a) na (b) na sheria ya polisi sura (322) kwa kuingilia kazi za OCD wa
Mufindi ambae ndie ‘officer in-charge’. Kwa maana hiyo amri iliyotolewa kuzuia
mikutano hiyo haikuwa halali kwakuwa ilitolewa na mtu ambae hakuwa na mamlaka
kisheria kutoa amri hiyo,” alisema jaji Manento.
Alipozungumzia hatua ya
msajili wa vyama vya siasa nchini John Tendwa kuwaandikia barua viongozi wa
vyama vya siasa kusitisha shughuli zao kwasababu ya sensa alisema suala hilo ni kinyume na sheria
za takwimu kusimamisha shughuli za kijamii wakati wa sensa.
“Maelezo yaliyotolewa ndani
ya barua hizo yanakinzana na sheria ya takwimu Namba 1 ya mwaka 2002 inayotoa
fursa kwa wananchi kuendelea na kazi zao wakati wa sensa pia ni kinyume na
sheria ya vyama vya siasa kufanya shughuli zake bila kuingiliwa,” aliongeza.
Katika hatua nyingine
mwenyekiti wa tume hiyo amezungumzia ripoti nyingine zilizotangulia na kusema
kila mtu anayo haki kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kuhusu matokeo kila mtu ana namna
yake ya kurekebisha jamii.
“Sisi tupo kisheria na hakuna
mtu wa kutuingilia, mara nyingine changamoto tunazokutana nazo ni kutokana na
ukosefu wa fedha hivyo isionekane tunabagua matukio ya kuyafanyia utafiti. Sisi
ripoti yetu tumeipeleka serikalini hao wengine wataipeleka wapi?”, alihoji.
Hii ni ripoti ya tatu
iliyotolewa kuhusiana na kifo cha Daudi Mwangosi katika kipindi cha wiki moja.
Siku ya jumanne Octoba 8 ripoti mbili zilizokinzana za baraza la habari
Tanzania (MCT) na wizara ya mambo ya ndani na ulinzi; ambapo MCT ripoti yao
ilionyesha jeshi la polisi lilihusika moja kwa moja na kifo cha mwandishi huyo
pamoja na chuki za muda mrefu baina ya jeshi la polisi na wanahabari wa mkoa wa
Iringa.
Wakati ripoti ya wizara
iliyopewa jina la ripoti ya Dk Nchimbi, imetoa majibu tofauti kwa kueleza kuwa
jeshi la polisi halikuhusika na mauaji hayo kabisa.
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM , TANZANIA
0713 593894/ 0752 593894
10/10/2012
No comments:
Post a Comment