Zitto Zuberi Kabwe
Toleo la 262
10
Oct 2012
JOHNSON Mbwambo
ameandika katika Gazeti la Raia Mwema la Oktoba 3, mwaka huu, kuhusu dhihaka za Zitto kwa Prof. Muhongo (Waziri wa Nishati na Madini).
Nimesoma na nimemuelewa. Kwanza naomba radhi
iwapo tafsiri ya taarifa yangu niliyoitoa kwa vyombo vya habari na kuwekwa
kwenye blogu yangu (zittokabwe.com) ilikuwa ina dhihaka.
Nimefundishwa kutodhihaki watu na hasa watu
wanaonizidi umri na siasa zangu sio za dhihaka bali za masuala (issues).
Kupitia kwa ndugu Mbwambo naomba radhi kwa wote walioona kuna dhihaka katika
andiko langu. Sikuwa na nia ya kumdhihaki Waziri Muhongo. Nia yangu ni
kuonyesha kuwa Waziri Muhongo alichokifanya ni kuwacheza shere Watanzania, kwa
kuwaambia maneno ambayo yeye mwenyewe alikuwa anaamini kuwa hayawezekani.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara
yake, Eliakim Maswi, ilithibitisha kauli yangu siku chache tu baada ya kuitoa.
Mbwambo kaandika makala yake kana kwamba hapakuwa na kauli ya kufuta maneno ya
Waziri. Ninaamini Mbwambo aliiona kauli ile lakini aliamua kupuuza ili
kujifurahisha na imani yake kwa Prof. Muhongo na mawaziri aliowataja kwenye
makala yake kwamba ni mawakala wa mabadiliko. Mbwambo anaamini kabisa kwamba
ndani ya utawala wa CCM, kuna mawaziri wenye nia ya dhati ya kuleta mabadiliko.
Nieleze wazi kwamba nilishtuka sana kuona toleo moja la
Gazeti la Raia Mwema likiwa na makala tatu, zote dhidi ya Zitto Kabwe. Wakati
makala ya ndugu Mbwambo ilikuwa inahusu suala nyeti sana la rasilimali za taifa na ni makala
nzuri yenye mafundisho, makala mbili nyingine zilikuwa ni za siasa dhidi ya
Zitto. Mwandishi Mayage Mayage aliandika makala yenye kichwa cha habari “Zitto,
Urais 2015 kwa chama gani?” na Mwanasafu wa gazeti hili la Raia Mwema, Evarist
Chahali aliandika makala yenye kichwa cha habari “Rais Kikwete anapofikiri kama Kabwe Zitto.”
Namwambia Mayage akasome vizuri historia ya
ujenzi wa CHADEMA. Yeye anadhani CHADEMA imeanza mwaka 2010. CHADEMA kimejengwa
na watu, si mtu mmoja. Wanaoamua mgombea wa chama si watu wachache anaowadhani
yeye Mayage bali ni wanachama wa CHADEMA kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania ,
ikiwamo Munanila, mkoani Kigoma anapotoka Mayage.
Huyu Chahali anasema ananijua sana . Inawezekana
ananijua kuliko mimi ninavyojijua. Lakini mimi simjui na wala sijawahi kumwona
ana kwa ana, nimekuwa nikimwona tu kwenye mitandao ya kijamii akinizushia,
kunitukana na kunisema. Sikushangaa kusoma makala yake ya wiki iliyopita. Wote
wawili nawakumbusha msemo wa Mahatma Gandhi aliposema; “Kwanza
wanakudharau, kisha wanakucheka, kisha wanapambana na wewe, kisha
unashinda".
Sasa nirejee kwenye makala ya ndugu Mbwambo.
Prof. Muhongo simjui, licha ya kwamba nimekuwa mmoja wa wabunge walioko mstari
wa mbele kuhakikisha utajiri wa nchi unatumika kwa manufaa ya nchi, sikuwahi
kumsikia Prof. Muhongo mpaka alipoteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Sikuwahi kusikia akipaza sauti yake dhidi ya
mikataba mibovu ya madini licha ya kwamba yeye ni msomi aliyebobea katika
masuala ya miamba. Wakati Bunge la tisa, chini ya Spika Samuel Sitta, likiwa
limecharuka kutaka mikataba mibovu ipitiwe na kubadilishwa tulitarajia sana kupata ushauri wa
wataalamu wetu lakini hawakuonekana, "walikwina"?
Walikuwa waoga kusema maana wangeharibu
uhusiano kati yao
na watawala. Tulihangaika wenyewe bila maarifa yoyote kuhusu sekta ya madini.
Wengine ilibidi kuacha kazi za ubunge na kwenda masomoni ili kuongeza ujuzi wa
masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusu sekta ya rasilimali (madini na mafuta).
Wasomi wetu hawakuwa nasi. Walichague
kuendelea kufanya kazi za ushauri kwa kampuni za utafutaji madini nchini. Leo
Mbwambo anawaona hawa ndiyo mawakala wa mabadiliko. Labda anasema kweli. Ila
mimi nimekata tamaa na mabadiliko kuletwa na watu waliomo serikalini, kwa
sababu kadhaa.
Moja, kama alivyosema ndugu Mbwambo,
nilipigia kelele sana
mkataba wa Buzwagi na mikataba mingine ya madini. Niliendelea kupiga kelele
mpaka sheria mpya ya madini ilipopitishwa na Bunge. Nimuulize Mbwambo kwamba,
licha ya sheria mpya kuandikwa imechukua miaka mingapi kampuni za madini
kufanya kazi zao kwa kutumia sheria hiyo mpya? Je, mikataba mingapi iliyopitiwa
imerekebishwa au hata kuvunjwa? Pengine niwasaidie kuwakumbusha taarifa kwamba,
hakuna kilichofanyika kwa mujibu wa sheria mpya, licha ya kufuatilia kwa kina
bungeni kupitia michango na hata maswali bungeni sambamba na makala mbalimbali.
Tangu Waziri Prof. Muhongo na timu yake
waingie ofisini ni maneno tu tunayosikia bila matendo. Hata suala la mgawo wa
umeme ambalo ndugu Mbwambo analisema kama
mfano, yeye anajua namna ambavyo wananchi wanalalamikia umeme kukatika hovyo,
tena bila taarifa wala maelezo. Muhongo alifanikiwa sana
kuaminisha watu wenye mawazo huru kama Mbwambo
wakamwona yupo sahihi kiasi hata cha kufumbia macho mgawo wa umeme usio na
maelezo, unaoendelea nchini.
Siwaamini mawaziri kwa sababu wanasema
lolote linalowajia midomoni mwao hata kama
wanaamini kuwa wanalosema haliwezekani kutekelezwa. Waziri wa Nishati na Madini
alisema kuhusu mikataba ya mafuta na gesi ili kufurahisha watu. Huo ni msingi
wa kwanza wa kauli yangu ambayo ndugu yangu Mbwambo ameitafsiri kuwa ni
dhihaka. Nilikuwa nasema ukweli mchungu kwamba, serikali haiwezi kufanya lolote
kuhusu mikataba. Nilitoa changamoto kuwa kama
serikali kweli imedhamiria, iweke mikataba hii wazi. Je, wameiweka wazi?
Pili, Waziri wa Nishati na Madini anataka
umma umwone kwamba anajua sana
masuala ya sekta kuliko Mtanzania mwingine yeyote. Nitatoa mfano mmoja
unaonihusu moja kwa moja. Katika mkutano wa Bunge uliopita, Tanzania
ilitembelewa na Waziri Mkuu mstaafu wa Urusi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi
ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Kirusi iliyonunua leseni ya kutafuta uranium kule
Selous. Kampuni ya UraniumOne iliyonunua leseni hii ya Mkuju River Project
kutoka Kampuni ya Mantra ya Australia ,
kwa dola za Marekani milioni 980.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitaka
ilipwe kodi ya ongezeko la mtaji (capital gains tax) kampuni hii ilikataa. TRA
wakaenda mahakamani kudai malipo ya kodi yenye thamani ya dola za Marekani
milioni 116 ambazo ni sawa na asilimia 20 ya thamani ya mauzo na kesi
inaendelea. Kwa mujibu wa sheria zetu kampuni zinapouziana leseni, lazima
Waziri wa Nishati na Madini atoe idhini ya mauzo hayo. Mgeni huyo kutoka Urusi
alikuja nchini kupigia debe idhini hii, ili itolewe leseni maalumu ya uchimbaji
(special mining licence).
Nikasimama kutoa taarifa bungeni kwamba
mawaziri wanakutana na huyu Waziri Mkuu mstaafu wa Urusi kuhusu leseni ya Mkuju
River Project na kuweka wazi kwamba Kampuni ya UraniumOne hawajalipa kodi ya
capital gains. Nilisimama kutoa taarifa baada ya majibu ya Waziri Muhongo kwamba,
kilichouzwa si kampuni ya Tanzania
bali Australia
na hivyo hakuna kodi.
Kwa makusudi kabisa niliacha habari ya kesi
ya TRA dhidi ya kampuni hii ili kuona umakini wa mawaziri wetu wapya kabla ya
kukutana na lobbyists (washawishi) wa kampuni hizi za madini. Waziri Muhongo
aliposimamishwa na Naibu Spika, Job Ndugai, akasema “Sisi tunajua zaidi kuliko
Zitto" Kwanza Waziri hakuwa anajua.
Ni makosa kabisa kujadili suala ambalo
mamlaka mojawapo ya nchi wamelipeleka mahakamani na linasubiri uamuzi. Lakini
suala la Waziri kutokuwa na taarifa lilidhibitishwa na ujio wa Naibu Waziri
George Simbachawene, aliponifuata na kuomba "details" kuhusu taarifa
niliyotoa. Kulikuwa na haja gani kwa Waziri kusema bungeni yeye anajua zaidi na
baadaye kumtuma Naibu wake kutafuta taarifa?
Huu ni udhaifu mkubwa sana wa uongozi. Kutojua si makosa,
inawezekana kuwa wengine hatukusomea miamba lakini tumesomea masuala ya kodi
kwenye madini na mafuta. Waziri makini anayejali nchi yake anawezaje kukutana
na mwekezaji anayekataa kukulipa kodi yako bila wewe hata kuulizia utalipwa
lini?
Unaulizwa bungeni unasema "ninajua
zaidi" na Mwandishi mahiri kama Mbwambo
anasema "mpeni nafasi atende"!
Nilipomsikia Waziri anasema ameagiza TPDC
(Shirika la Maendeleo la Mafuta) kupitia mikataba nikajua na hili nalo hajui.
Amesema tu ili watu wafurahi kwamba mikataba inapitiwa. Kupitia mikataba bila
kuchukua hatua dhidi ya mikataba mibovu ni nini kama
sio kutafuta umaarufu tu? Unapitia mikataba ili iwe nini kama
huwezi kuchukua hatua?
Kuna mikataba ambayo imeingiwa kwa rushwa,
sheria zetu zinasema kuwa mikataba iliyoingiwa kwa rushwa ni sawa na haipo.
Hata sheria za kimataifa za mikataba zinatambua hivyo. Waziri anaposema kuwa
tunapitia mikataba ili kuhakikisha kuwa mikataba ijayo inakuwa mizuri ni kichekesho.
Hivi tunajua vitalu vingapi vimegawiwa na vingapi vimebaki? Hivi sasa kuna
mikataba 29 na leseni 26. Vitalu vilivyobaki hivi sasa ni tisa tu.
Wizara inatuambia tunaangalia hii mikataba
29 ili kuboresha 9. Haya si mapitio bali ni kuangalia tu kama
nilivyosema katika sentensi iliyotangulia. Mapitio bora zaidi ni uwazi wa
mikataba yote tuliyoingia mpaka sasa na kuzuia kabisa mikataba mipya wala
kugawa vitalu vipya vya kutafuta mafuta na gesi.
Uporaji wa rasilimali ni wa namna mbili,
moja ni watu wachache na kampuni zao kupora kwa kupitia mikataba mibovu na pili
ni kizazi kimoja kunyonya rasilimali zote bila kujali kizazi kijacho. Katika
maandiko yangu nimeshauri kuwa tusigawe vitalu vipya mpaka tuone mafanikio ya
mikataba hii 29 na leseni 26 tulizonazo hivi sasa. Wito wangu ni mmoja tu,
uwazi wa mikataba. Kutaka uwazi si dhihaka. Uwazi ni uwajibikaji.
Suala la mapitio ya mikataba kwa jicho la
juu juu ni suala la kuunga mkono. Lakini ukitazama historia ya nchi yetu katika
masuala haya utabaini kwamba tunapaswa kufanya zaidi ya mapitio ya mikataba.
Tunapaswa kufanya jambo ambalo hatujawahi
kulifanya nalo ni kuiweka wazi mikataba hii kwa umma. Hii ndiyo hoja yangu.
Inawezekana kabisa kwamba maneno niliyotumia
yameudhi watu fulani lakini ikumbukwe mimi ni Mbunge wa Upinzani na ni wajibu
wangu kukosoa serikali kila inapowezekana. Bahati nzuri miaka yangu saba
bungeni hivi sasa imetumika kwa kiasi kikubwa sana katika kufuatilia kwa karibu sekta ya
madini, mafuta na gesi. Ni rahisi sana
mimi kuweza kuona suala linalosemwa na serikali linasemwa tu au serikali
inamaanisha? Katika suala la mapitio ya mikataba kwenye sekta ya madini na
mafuta kwa kweli serikali haipo makini. Watu wajuvi wa mambo kama
kina Mbwambo wanapaswa kwenda zaidi ya mapitio na kutaka mikataba iwekwe wazi
na kuchambuliwa kwa uwazi kabisa.
Waziri Muhongo anayo nafasi ya kufanya kazi
yake, afanye kazi yake bila bugudha. Mbwambo ajue kuwa Mbunge Zitto pia anayo
kazi yake kwa mujibu wa Katiba ibara ya 63 nayo ni "kuisimamia"
serikali. Niacheni nami nifanye kazi yangu.
Makala haya katika gazeti la Raia Mwema yaliyoandikwa na Kabwe Zitto,
Mbunge wa Kigoma Kaskazini ni majibu kwa makala iliyoandikwa na Mwanasafu wetu,
Johnson Mbwambo, katika toleo lililopita la gazeti hili la Raia Mwema, kupitia
safu yake ya Tafakuri Jadidi.
No comments:
Post a Comment