Na Hafidh Kido
Ripoti ya timu maalum iliyoundwa na Baraza la Habari
Tanzania (MCT) na jukwaa la wahariri Tanzania (TEF) kuchunguza mauaji ya mwandishi
wa habari Daudi Mwangosi alieuwawa Septemba 2 mwaka huu imegundua kuwa
kulikuwepo na mahusiano mabaya baina ya polisi wa mkoa wa Iringa na waandishi
wa habari.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo
asubuhi wakati wa kuzindua matokeo ya ripoti hiyo katibu mkuu wa MCT Kajubi
Mukajanga, alisema kuanzia mwishoni mwa mwaka jana mahusiano baina ya polisi na
waandishi wa habari mkoani Iringa yalikuwa mabaya kiasi cha kuwafanya waandishi
kupata mazingira magumu kufanya kazi na jeshi hilo.
“Uchunguzi wa awali wa hali ya mahusiano kati ya viongozi wa
Mkoa wa Iringa wakiwamo Polisi na waandishi wa habari kabla ya mauaji ya
Mwangosi ulibaini kwamba mahusiano hayakuwa mazuri na yanagubikwa na
kutoaminiana kati ya pande hizo mbili tangu robo ya mwisho wa mwaka 2011,”
alisema Kajubi.
Akifafanua njia walizotumia kufanya uchunguzi huo Kajubi
alieleza kuwa “Timu yetu ilihusisha watu watatu John Misenyi kutoka MCT upande
wa machapisho na utafiti, wa pili ni Haruna Shamte kutoka jukwaa la wahariri
pamoja na Simon Berege ambae ni Mhadhiri chuo kikuu cha Tumaini.
“Mchakato wa kukusanya taarifa hizi ulihusisha mbinu za
uandishi wa kiuchunguzi wa hali ya juu kwa kuhoji wananchi waliokuwepo katika
eneo la tukio, jeshi la polisi, viongozi wa chadema, waandishi wa habari
waliokuwepo eneo la tukio na majeruhi walioshiriki maandamano ya chadema,”
Kajubi.
Akitolea mfano wa matukio yaliyoashiria mahusiano mabaya
baina ya polisi na wanahabari mkoani humo Kajubi alisema ripoti inaonyesha kuwa
Novemba mwaka 2011, mwandishi Lauren Mkumbata wa ITV alipigwa vibaya huku vifaa
vyake vya kazi vikiharibiwa kwa makusudi na aliyekuwa mkuu wa polisi Iringa OCD
Mohamed Semunyu, wakati akiwa kazini.
Katika tukio jingine ripoti hiyo inaeleza kuwa katika ziara
ya makamu wa Rais Mohammed Gharib Bilal mkoani humo February 2011, waandishi
walilazimika kulala kwenye basi walilosafiria kutokana na viongozi wa mkoa na
jeshi la polisi kupuuza kuwapatia hoteli ya kulala pamoja na huduma nyingine.
Aidha ripoti hiyo yenye kurasa thalathini imebainisha kuwa
katika siku ya tukio la kuuwawa Mwangosi jeshi la polisi lilionekana kuwakwepa
waandishi wengine waliotoka mikoa tofauti na Iringa ambao waliletwa na chadema
katika mikutano ya vuguvugu la mabadiliko. Miongoni mwa waandishi hao ni
waandishi kutoka Dar es Salaam na mikoa mingine
lakini hakuna hata mmoja alieguswa, hivyo hiyo inadhihirisha ni namna gani
jeshi la polisi lilikuwa likijua mipango yao .
“Suala la kukosewa na kutotambuliwa Mwangosi halipo kabisa
kwasababu polisi waliwafukuza, kuwapiga, kuwajeruhi na hatimae kumuua mwandishi
ambae walikuwa wakimjua vizuri kabisa. Marehemu Mwangosi alizingirwa na kupigwa
na polisi wasiopungua saba na kuuwawa wakati polisi mmoja mwandamizi
alijeruhiwa vibaya.
“Matokeo haya yanathibitishwa na maelezo pamoja na ushahidi
uliokusanywa kwa kutumia picha za video na ushahidi mwingine muhimu wa taarifa
za vyombo vya habari,” ilisema taarifa hiyo.
Wakati huohuo mjumbe wa umoja wa vilabu vya habari nchini
(UTPC) Abubakar Karsan, alieleza masikitiko yake kutokana na tukio hilo na kudai kuwa sifa ya Tanzania
imeharibika kwani haijawahi kutoke katika historia ya Tanzania
mwandishi kuuwawa akiwa kazini.
“Kwa kuona hivyo tumeamua kumuenzi ndugu Mwangosi kwa
kuifanya tarehe ya kifo chake September 2, kuwa ndiyo ya mkutano mkuu wa UTPC
kila mwaka, kadhalika tutaanzisha tuzo ya uandishi uliotukuka tutakayoipa jina
la Mwangosi na mwisho tutaanzisha mfuko wa kusaidia waandishi wanaopata
matatizo wakiwa kazini na kuipa jina la Mwangosi fund,” Karsan.
Daudi Mwangosi ni mwandishi wa kituo cha Channel Ten cha
jijini Dar es Salaam ,
aliuwawa katika mvutano baina ya jeshi la polisi na wafuasi wa Chadema kijijini
Nyololo, Wilaya Ya Mufindi Mkoani Iringa mnamo Septemba 2 mwaka huu.
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM ,
TANZANIA
09/10/2012
NB: Nimefundishwa katika uanahabari kutokubali kushindwa, leo nimefanya kituko cha mwaka baada ya kusahau kuenda mjini na Kamera. Hivyo nilichofanya baada ya kurudi nyumbani nikaandika hiyo habari halafu nikaipiga picha hiyo ripoti. Sina picha ya viongozi wa MCT walioisoma hiyo ripoti....
No comments:
Post a Comment