Wagombea wa urais nchini Kenya katika uchaguzi mkuu wa
mwaka ujao, watashiriki kwa mara ya kwanza mdahalo wa urais kabla ya uchaguzi
huo wa mwezi Machi 2013.
Hii leo baraza la vyombo la habari limezindua mpango huo
likilenga kuwaweka wazi wagombea wa urais mbele ya wananchi kuweza kujibu hoja
za wananchi kuwahusu, kitu ambacho hakijawahi kufanyika nchini Kenya .
Mijadala hiyo mitatu, itaandaliwa kwa
ushirikiano wa vyombo vya habari chini ya baraza la vyombo vya habari na
kupeperushwa moja kwa moja kupitia runinga, redio na kwenye mitandao, kuanzia
Novemba 26.
Mdahalo
mwingine utaandaliwa kabla ya duru ya pili ya uchaguzi wa urais, iwapo
hapatapatikana mshindi katika raundi ya kwanza.
Mmoja
wa waandaliizi wa midahalo hiyo ni afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya habari ya
Nation, Linus Gitahi. Alielezea lengo la mijadala hiyo, " Kuna maswala kama vile elimu, usalama na miundo msingi. Tunataka
kuwaleta wagombea hawa pamoja, ili wanachi wapate fursa ya kuwajua viongozi
wao. Tunachotaka katika mijadala hii, ni watu watakaowaonyesha wakenya ni sera
zipi walizonazo. Hatutazingatia wewe ni wa kabila gani, au wewe ni kiongozi wa
kundi gani."
Huu
utakuwa uchaguzi wa kwanza nchini Kenya , tangu uchaguzi mkuu wa 2007
uliokumbwa na ghasia zilizosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,100 na maelfu
wengine kuachwa bila makao.
Wagombea
13 tayari wameelezea azma ya kumrithi Rais Mwai kibaki ambaye anastaafu mwaka
ujao baada ya kukamilisha mihula miwili ofisini.
Wagombea
hao ni pamoja na waziri Mkuu Raila Odinga, makamu wa rais kalonzo Musyoka na
naibu waziri Mkuu Musalia Mudavadi.
Naibu
mwingine wa waziri Mkuu Uhuru Kenyatta na Mbunge wa Eldoret Kaskazini William
Ruto, ambao wanakabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita katika mahakama ya
Kimataifa ya ICC, pia wameelezea azma ya kuwania kiti hicho cha urais, licha ya
kesi inayowakabili.
Mashirika
ya kijamii vilevile yamewasilisha kesi mahakamabni yakitaka Uhuru na Ruto
kuzuiwa kuwania urais katika uchaguzi huo, wakisema hatua hiyo inakiuka katiba
mpya ya Kenya .
Chanzo: BBC Swahili.
No comments:
Post a Comment