Saturday, October 6, 2012

Leo Bukoba hapatoshi mazishi ya Rugambwa...


KUELEKEA MAZISHI NA KUMBUKUMBU YA MIAKA 100 YA MWANAMWEMA LAUREAN RUGAMBWA, KADINALI WA KWANZA MWAFRIKA.

MAZISHI MAPYA.

Hii ni siku Adhimu kwetu wanaUkurasa, kwa kuwa leo tumepata Fursa hii adimu ya kumzungumzia Mtanzania Mwengine Mashuhuri Miongoni mwetu.

Tarehe 6 mwezi huu (yaani leo) itakuwa ni siku Rasmi ya Mazishi ya Mwadhama Kardinali Laurean Rugambwa ambaye alikuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Nchini Tanzania na pia Kadinali wa Kwanza Mweusi kutoka Afrika.

Katika siku hii kutakuwa na tukio kubwa la Kuzikwa Upya (wengine wanasema ndio mazishi Rasmi kwa kuwa Mwanzoni hakuzikwa bali mwili wake ulihifadhiwa tu kwa kwa muda) kwa Mabaki ya Mwili wa Mwadhama Kadinali Rugambwa ambaye alizikwa kwa muda katika Kanisa Katoliki la Kashozi mwaka 1997. Mazishi hayo mapya yatafanyika Katika Kanisa Kuu Jimbo Katoliki Bukoba (ambalo lilikuwa kwenye Ukarabati tokea Mwaka 1996) ikiwa ni kufuata Wosia wake yeye Mwenyewe wa kutaka Azikwe hapo.

Mazishi hayo yatahudhuriwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Mawaziri Mbalimbali, Viongozi na Wafanyabiashara Mashuhuri, Wanadiplomasia, Wachungaji na Maaskofu pamoja na Wananchi mbalimbali kutoka ndani ya Nchi na Nje ya Nchi. Laurean Mwigamba ni Mtu Mashuhuri, ni muhali tukio hili kupita bila kuyajadili Maisha yake yenye Changamoto na mafundisho Mengi. Keshi itafanyika Misa Maalum ya kumbukumbu ya miaka 100 tokea kuzaliwa kwake.

UZAO WENYE UTAKASO, "MASHUHURI" JINA LAKE.

Laurean Rugambwa Alizaliwa katika Kijiji cha Bukongo - Kamachumu, Parokia ya Rutabo, Wilayani Bukoba katika Mkoa wa Kagera tarehe 12 Julai 1912. Mazazi yake yalikuwa ni ishara njema wa Utumishi wa kutukuka wa Kadinali Laurean kwa wanaadamu wenzake na kwa Bwana Mungu wa Mbingu na Nchi. 

Laurean Rugambwa alikuwa Mtoto wa Bwana Domitiani Rushubirwa katika Ndoa yake na Mkewe Mpendwa Bi Asteria Mukaboshezi ambao wote walitokea katika Ukoo wa Kitemi ambapo wazazi wake hao walimpa Jina la "Rugabwa" ambapo kwa Lugha ya Kihaya lina maana ya "MASHUHURI" ikiwa ni kielelezo chema juu ya Maisha yake ya Umashuhuri mbeleni.

MWITO WA KIROHO, UBATIZO NA UVUMILIVU.

Miaka ile Kardinali Rugambwa akikua, Kiongozi Mkuu wa Kimila wa eneo la Kamachumu alikuwa amekataza Harakati zozote za Kidini katika eneo lake hivyo kwa kuwa Mtoto "Mashuhuri" Rugambwa alielekea kupenda mambo ya dini ilimbidi atembee umbali mrefu wa zaidi ya Kilometa 20 kila siku kwenda kwenye Parokia ya Kagondo kupata Mafundisho ya Kiroho.

Rugambwa hakukwaza wala hakuacha uvumilivu juu ya kutembea kwake umbali wote huo kwa kuwa ni dhahiri ndani ya moyo wake wito wa utumishi ulishaanza kushamiri pamoja na umri wake mdogo tu.

Tarehe 21 Machi 1921 Kijana wa miaka 9 Rugambwa alibatizwa na Faza Emil Verfurth ambaye alikuwa Mmishenari wa Afrika kupitia Shirika la White Farther, kuonyesha Baraka ya Ubatizo wa Rugambwa mwaka huo huo ambao yeye alibatizwa ndio mwaka ambao Chifu wa Kamachumu alitoa ruhusa ya uanzishwaji wa shughuli za kidini katika eneo hilo ambapo Parokia ya Rutabo ilianzishwa.

ELIMU NA UFUNUO.

Mara baada ya Kubatizwa Rugambwa alianza masomo yake ya awali katika Shule ya Msingi ambayo ilikuwepo kwenye eneo lao ambapo ilipofika mwaka 1926 alichaguliwa kujiunga Shule ya Kati ya Rubya ambapo alisoma mpaka 1933.

Mwaka 1933 Kardinali Rugambwa alijiunga na Shule na Shule ya Seminari ya Juu ya Katigondo Nchini Uganda, ambapo akiwa huko Katigondo walimu wake wake walikuwa ni Wamishionari wa Shirika la White Farther ambao walikuwa wakitoa huduma hiyo Bukoba na huko Uganda. Miongoni mwa Walimu wake Shuleni hapoa alikuwa Joseph Kiwanuka ambaye baadaye alikuja kuwa Askofu wa Masaka.

PADRI LAUREAN RUGAMBWA, KUJITOA NA UTII.

Tarehe 12 Desemba 1943 akiwa na Umri wa miaka 31 Kardinali Rugambwa alitawazwa kuwa Padri, Sherehe ya Kutawazwa kwake ilifanyika kwao Rutabo ambapo aliyemtawaza alikuwa Mchungaji Burchard Huwiler. Mara baada ya kutawazwa huko aliteuliwa kwenda kuhudumu katika Parokia ya Kagondo kisha baadaye kupelekwa katika Parokia ya Rubya.

Historia ya maisha ya Kadinali Rugambwa inamuonyesha namna alivyoipenda kazi yake ya kiutumishi, ambapo mara nyingi alitembea umbali mrefu ili kuwafikia Waamini mbalimbali waliohitaji huduma yake. Wakati akiteuliwa kuwa Padri alibahatika kuwa na Baiskeli ambayo aliitumia kwenda umbali mrefu wa zaidi ya Kilometa 50 ili kuwafikia waumini zaidi.

Mwaka 1948 Padri Laurean Rugambwa alihamishiwa katika Parokia ya Kashozi (mahali ambapo alizikwa kwa muda kabla ya kuzikwa rasmi kesho) ambayo ndiyo Parokia ya Mwanzoni zaidi katika Dayosisi nzima.

Uhuduma wa Upendo, Utu na kujitolea ambao aliutoa kwa Wanaparokia ya Kashozi ni jambo ambalo haliwezi kusahauliwa milele, upole, utii na unyenyekevu wake vikiwa ndiyo vipambo vyake vikuu ambavyo vilimfanya apendwe na watu wote parokiani hapa na kuwa mfano wa kuigwa kwa watu wote.

RUGAMBWA MASOMONI ROMA, MATAYARISHO YA VIKA YA KITUME.

Katika wakati huo Makao Makuu ya Kanisa Katoliki huko Roma yalikuwa na Mpango wa kuigawanya Vika ya Bukoba ikiwa ni jaribio la pili la Mgawanyo wa Vika katika Nchi za Waafrika Weusi ambayo ingeongozwa na Mwafrika mara baada ya mgawanyo wa kwanza wa Vika ya Masaka nchini Uganda.

Padri Rugambwa alichaguliwa kwenda Masomoni Mjini Roma kwa ajili hiyo ya kuja kuiongoza Vika ya Bukoba mara baada ya kumaliza Masomo. Wakati akiwa Roma kwa Masomo yake katika Chuo cha Mtakatifu Peter pia alijiunga na Masomo ya Sheria za Kanisa Katoliki (Canon Law) katika Chuo cha Pontifical Urban ambavyo kwa uwezo wake mkubwa aliweza kufanya vizuri katika masomo yake kwenye vyuo vyote hivyo.

ASKOFU RUGAMBWA, KAZI NIEMA YA UTUMISHI.

Mwaka 1948 Askofu Burchard Huwiler wa Bukoba alifikisha Umri wa Miaka 80, kwa kuwa hali yake ya afya ilianza kudhoofika kwa sababu ya Umri wake Mkubwa aliamua kustaafu kazi yake ya Utumishi na kupisha mtu mwengine aendeleze pale ambapo yeye aliishia. Askofu Ttrault alichaguliwa kushika nafasi yake ambapo kwa bahati mbaya mara baada ya miaka miwili hali ya kiafya ya Askofu Burchard ilizidi kudhoofika na ilipofika mwaka 1951 aliiaga dunia na kuacha huzuni kubwa kwa jamii ya Watu wa Kagera.

Katika hali hiyo maandalizi ya kuigawanya Vika ya Bukoba yalikuwa yamepamba mmoto mno, ambapo wakati Padri Rugambwa aliporudi kutoka Masomoni Roma mara baada ya Mahafali yake ya kutunikiwa Shahada ya Uzamivu ya Sheria za Kanisa (Doctorate in Canon Law) aliteuliwa kuhudumu Rubya kwa muda kisha akarudishwa tena Kashozi.

Tarehe 13 Desemba 1951 Laurean Rugambwa alisimikwa kuu Askofu Mkuu wa Vika Mpya ya Kitume wa Kagera kusini, Alipewa rasmi daraja takatifu hiloo tarehe 10 Februari 1952 na askofu David Mathew. Eneo alilokabidhiwa likafanywa jimbo la Rutabo tarehe 25 Machi 1953 na tarehe 21 Juni 1960 likabadilishiwa jina kuwa Jimbo Katoliki la Bukoba.

UKARDINALI WA KWELI KUTOKA AFRIKA NDIO HUU, RUGAMBWA NI HESHIMA YA WATU WEUSI.

Aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Baba Mtakatifu Papa Yohane XXIII alimteua Laurean Rugambwa kuwa kardinali tarehe 28 Machi 1960 na akamkabidi Kanisa lake la Mtakatifu Francesco Assisi. Uteuzi Husika ulimfanya Kadinali Rugambwa kuwa kardinali wa kwanza asiye Mzungu.

Uteuzi wake huo uliibua hamasa na heshima kubwa kwa Afrika na Mataifa yake na ulikuwa ni ufunguo mwema wa mabadiliko ya Mtazamo juu ya nafasi ya Waafrika weusi katika anga za dunia, heshima ambayo Rugambwa alililetea Bara la Afrika kwa uteuzi wake haimithiliki.

Mara baada ya kuteuliwa kuwa kardinali alitembelea nchi za Ulaya na Marekani ambako alipokelewa vizuri sana na kwa heshima zote za kiserikali. Ikumbukwe kwamba wakati huu ulikuwa bado wakati wa ukoloni katika nchi karibu zote za Afrika. Kupitia kwake mtu mweusi aliheshimiwa na kukubalika kwa wote. Ulaya hasa Italia, Ugerumani, Uholanzi, Ubelgigi na Austria alipokelewa na viongozi wa juu wa serikali. Ujerumani alionana na Rais, Waziri Mkuu na kuiongelea Bundestag ambalo ndilo bunge la Ugerumani. Hii ilikuwa heshima kubwa sana ambayo hawapewi hata wakuu wa serikali.

Huko Marekani alihutubia katika vyuo vikuu vingi vilivyomtunuku shahada za juu za udaktari wa heshima. Alikutana na vingozi wa wamarekani weusi ambao walijionea sifa sana kwake. Katika yeye walijivuna kuwa weusi na kukumbuka kwamba wao ni watoto wa Afrika. Kwa mara ya kwanza wamarekani weusi walimwona mwafrika aliyepata cheo kikubwa kama hicho, hata na wazungu wa marekani ingawa waliwadharau watu weusi walimheshimu sana. Makardinali weupe wa Marekeni kama Kardinali Cushing, walimkaribisha majimboni kwao kwa heshima kubwa. Hivyo wote walimwona kama ishara ya uwezo wa mtu mweusi katika harakati zao za kupigania usawa huko marekani. Walianza kujihusisha na kanisa la Afrika.

MTOTO WA MFALME WA KANISA, NYAKUTUNUNTA KARDINALI MASHUHURI.

Heshima ambayo Mwadhama Kardinali Rugambwa aliipata na kupewa Roma na Vatikani ndio iliyofanya wengi waelewe ukubwa wa kardinali kulinganisha na jinsi alivyotendewa hapa kwetu ndicho kitu kilichotambulisha unyenyekevu wake. Bukoba na Tanzania kwa ujumla watu hawakujua wamwiteje ndipo wakatengeneza maneno ya 'Nyakutununta' kwa kihaya na Mwadhama kwa kiswahili.

Kardinali katika Kanisa Katoliki lenye waumini zaidi ya bilioni moja, ni mmoja wa watu bawaba au wa msingi 130 katika kanisa hilo. Kikanisa yeye yuko juu ya maaskofu, maaskofu wakuu, balozi wa Baba mtakatifu na wengine. Kidiplomatia hupokelewa kama Mwana Mfalme. Yeye hushiriki katika uchaguzi wa Baba Mtakatifu, (Rugambwa ameshiriki kuwachagua Baba Watakatifu watatu). Mwaka 1992, Baba Mtakatifu Yohana Paulo II akiwapokea maaskofu wa Tanzania alimwita mwana wa kwanza wa kanisa la Afrika. Aliwaambia maaskofu kwamba anamheshimu sana kwa sababu alimtangulia kama Kardinali. Rugambwa alikuwa mjumbe katika kamati na tume mabali mbali huko Vatikani ikiwemo ile ya Liturugia na ile ya Uenezaji Injili.

Kama Kardinali alipewa kanisa lake la kudumu Roma, kanisa la zamani sana la Mtakatifu Fransisco wa Ripa. Mwaka 1992 akisherehekea miaka 40 ya Uaskofu aliweza kuwaalika maaskofu wa Tanzania katika kanisa ambako walipokelewa vizuri na waumini wake. Waumini hao walimpenda na kujivunia kuwa na kardinali wa kwanza wa Afrika kama kardinali wao wa pekee.

Tarehe 19 Desemba 1968 alihamishiwa kwenye jimbo kuu la Dar-es-Salaam aliloliongoza hadi alipojiuzulu kutokana na uzee tarehe 22 Julai 1992.

RUGAMBWA KIUNGO NA MPATANISHI WA WOTE, KIONGOZI WA MAASKOFU WA AFRIKA.

Rugambwa alikuwa askofu wa tatu mwafrika na kardinali wa kwanza wa bara la Afrika. Maaskofu wa Afrika walimtambua na kumkubali kama kiongozi wao. Wakati wa Mtaguso Mkuu wa Vatikano II (1962-65) uliohudhuriwa na maaskofu zaidi ya 3,000 yeye alikuwa askofu mwafrika pekee aliyepewa fursa ya kuhutubia maaskofu wote kwa pamoja katika ukumbi mkuu katika miaka yote mitatu ya mkutano huo. Hata wazungu ni wachache sana waliopewa fursa hiyo.

Wakati wa mtaguso huo aliwaita pamoja maaskofu wote kutoka Afrika (wengi wao wakiwa wamisionari wazungu) na yeye akiwa mwenyekiti wao zilianza harakati za kuundwa umoja wa maaskofu wa Afrika, (SECAM). Vivyo hivyo Rugambwa alikuwa kiuongo cha kusaidia kuunda umoja wa maaskofu wa Afrika ya Mashariki, zikiwemo nchi za Eritrea, Ethiopia, Somalia, Sudan, Kenya, Uganda, Tanzania, Malawi na Zambia, (AMECEA). Mpaka alipofariki alikuwa bado baba mlezi wa umoja huo. Kwa sababu hiyo alikuwa mjumbe wa kudumu wa kamati tendaji, pamoja na kuwa vile vile baba mlezi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika ya Mashariki.

MCHANGO WAKE MKUU KWA TANZANIA.

Mwadhama Kardinali Rugambwa ana Mchango mkubwa sana kwa Taifa hili, mafanikio makubwa ya Kanisa Katoliki kati nynja za utoaji elimu, sekta ya Afya na huduma nyingi za kijamii yametokana na misingi yake mikuu aliyoiasisi tokea alipokuwa kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo.

Upeo wake wa elimu ulikuwa ni wa kumwelimisha mtu mzima, kijamii, kifamilia, na kitaifa. Kutimiza hilo alianza umoja wa 'St. Augustine Social Guild' katika umoja huu aliwaweka pamoja vijana na watu wazima wenye uwezo na kuwaendeleza kwa pamoja. Wale waliokuwa na akili aliwatuma sehemu bbali mbali kwa masomo ya juu hata Ulaya na Marekani.

Kwa kiasi kikubwa amechagiza maendeleo makubwa ya kielimu kuanzia katika eneo la kwao alipozaliwa mpaka katika kila ncha ya nchi hii, maendeleo ya kieleimu ambayo hayakubagua dini ya anayepewa hiyo elimu na yakatoa kipaumbele kikubwa sana kwa wanawake ambao mila na tamaduni zetu viliwafanya wawe nyuma sana kielimu.

Katika kupigania elimu ya wanawake labda ya kukumbukwa kuliko zote ni ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Rugambwa. Wakati huo hata kiulimwengu haja ya kuwasaidia wanawake ilikuwa bado haijapata msisitizo. 

PUMZIKA KWA AMANI RUGAMBWA

Apumzike kwa amani Rugambwa kwa kazi yake kubwa alioifanya, Mwonekano wake wa heshima, mtulivu, wa kitawala. Inatakiwa kujua na kukumbuka anatokana na damu na familia gani. Lakini hata akiwa Kardinali wa kwanza katika Afrika Nyeusi ya zama zetu, alidumu wa kawaida, halisi, wa kweli, na uthabiti wa hali ya juu.

Hakuongea sana, lakini alikuwa na nguvu ya kueleza mengi kwa alama na kwa ishara mbadala. Hakuwa mwepesi sana kuwaendea watu, lakini alipenda kuwaalika na kuwaashiria wengine wamsogelee kushirikishana mawazo, na hata kuwataka wawe pamoja naye.

Alikuwa na upendo wa pekee kwa nchi yake ya Tanzania: Mapenzi yake makubwa kwa masuala ya kitaifa, yalikuwa bayana kwa msukumo wake chanya wa kusonga mbele na maendeleo. Unyofu wake na uhalisia wake uliwavutia pia watu wa Roma, kwa nanma ya pekee wanafunzi Waafrika, kwa sababu kila alipokwenda alipata malazi katika Kolejio ile aliyokaa wakati wa masomo yake, na kule hakuwa na madai ya pekee, alikula pamoja na wanafunzi bila kutaka kitu cha kipekee, alishukuru kwa kila aina ya huduma aliyopewa, alimpokea kila aliyemwendea, na juu ya yote, alidumu ni mtu wa sala na wa imani ya kina.

Ingawa aliwahi kukutana na watu mashuhuri wengi, wakiwemo Mababa Watakatifu (wengine aliwachagua, kama Paulo V, John Paulo I na John Paulo II), Makardinali, Marais na viongozi wengine wa nchi Afrika, Ulaya, Amerka na Asia na Australia, akapewa na Shahada na nishani kadhaa, Kardinali Rugambwa hakujiona kama mtu mkubwa. Alikaa mtu wa watu wote bila ubaguzi.

Mpaka kustaafu kwake Bukoba na Dar es Salaam, Kardinali aliacha kumbukumbu kubwa sana za UPENDO NA UNYENYEKEVU wake mkuu kwa Majimbo hayo na Taifa letu hata Kanisa dunia kwa ujumla.

Mwaka 1992 kwa sababu ya Uzee aliamua kustaafu uongozi wa Kanisa akiwa na umri wa miaka 80 ambapo bado alibaki kuwa Mchamungu, Mnyenyekevu, Mwenye Upendo na Utii na pia mwenye ushirikiano kwa wote. Alifariki Dunia JIjini Dar es Salaam tarehe 8 Desemba 1997 akiwa na umri wa miaka 85 ambapo mwili wake ulihifadhiwa kwa muda katika Kanisa la Kashozi ambapo leo ndipo atawekwa rasmi kwenye nyumba yake ya milele.

Mola amlaze Pema Mtanzania Huyu Mashuhuri, Pumzika kwa Amani Mwadhama Kardinali Rugambwa.

Chanzo: Ukurasa wa watanzania mashuhuri...

No comments:

Post a Comment