Afisa kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa Nchini (TFDA) ambaye hakutaka jina
Na.
Aron Msigwa –MAELEZO.
10/10/2012,
Dar es salaam.
Serikali
imewasimamisha kazi mkurugenzi mkuu wa Bohari ya Dawa nchini (MSD) ,Mkuu wa
kitengo cha Udhibiti na Ubora na Afisa Udhibiti Ubora wa ohari
hiyo ili kupisha uchunguzi dhidi yao kufuatia kuruhusu kusambazwa kwa dawa
bandia za kupunguza makali ya UKIMWI aina ya TT –VIR 30 katika vituo mbalimbali vya kutolea
huduma za afya nchini.
Aidha
imepiga marufuku usambazaji na matumizi ya dawa aina ya TT –VIR 30 toleo na 0C
.01.85 inayotengenezwa na kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd
(TPI) kufuatia dawa hiyo kutengenezwa chini ya kiwango na kutofaa kwa
matumizi ya binadamu.
Akizungumza
leo jijini Dar es salaam Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi
amesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa mara baada ya kubaini kuwepo kwa dawa
bandia ya kupunguza makali ya Ukimwi katika hospitali ya wilaya ya Tarime
kufuatia ukaguzi uliofanywa na Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Chakula na
Dawa nchini (TFDA).
Amesema
kuwa ukaguzi na uchunguzi wa kimaabara dhidi ya dawa hiyo isiyokidhi viwango
ulibainia kuwa nyaraka zilizopo kuhusiana na dawa hizo unaonyesha kuwa Kiwanda
cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPI) waliiuzia Bohari ya Dawa (MSD)
dawa hiyo bandia toleo namba 0C. 01. 85 iliyotengenezwa
nchini mwezi Machi 2011 na kuonyesha mwisho wa matumizi yake mwezi Februari
2013.
Amefafanua kuwa dawa hiyo bandia ilikua na
dawa zenye rangi mbili tofauti njano na nyeupe na kuwa na viambata tofauti
vilivyopaswa kuwepo aina ya Efaverenz badala ya Niverapine, Lamivudine na
Stavudine na kuongeza kuwa vidonge vilivyokutwa kwenye vifungashio vya dawa
husika vilikua tofauti na vifungashio vilivyosajiliwa na TFDA.
Dkt. Mwinyi
amesema kuwa serikali inahakikisha kuwa dawa zenye ubora unaotakiwa za kupunguza
makali ya UKIMWI zinaendelea kupatikana katika vituo vya kutolea huduma kote
nchini na kuwaagiza waganga wakuu wa mikoa, wilaya na kamati za dawa na Tiba katika vituo
vya huduma za afya kuhakikisha kuwa zinapokea, kuhakiki na kusimamia kikamilifu
ubora na matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba nchini.
Kuhusu
upatikanaji wa dawa hizo amewatoa hofu wananchi na kuwahakikishia kuwa dawa za kutosha zenye
viwango stahili zitaendelea kupatikana katika
vituo vya kutolea huduma za afya nchini na kuwataka wananchi kutoa kushirikiana
na mamlaka husika kwa kutoa taarifa pale wanapobaini kuwepo kwa dawa zenye
ubora wenye mashaka au uvunjifu wa sheria inayosimamia ubora na usalama wa dawa.
No comments:
Post a Comment