Ndugu zangu,
Si vema leo mwanamapinduzi na mjamaa mwenzangu anatimiza mika 13
tangu kutangazwa kifo chake halafu ninyamaze bila kusema chochote. Sidhani ni
ustaarabu.
Sijajiandaa kuandika makala katika gazeti lolote mwaka huu kama nilivyozoea kufanya hivyo miaka sita iliyopita kila
mwaka. Si kwasababu ya kuizoea siku yenyewe wala si sababu ya uvivu, bali
nadhani inatosha tuliyoyaandika kuhusu Mwalimu Nyerere. Inafika wakati mada na
mijadala inajirudia mpaka kupoteza ladha na lengo.
Nina ushauri, kwanini tusiache kumuandika Mwalimu kutokana na
nafasi za kisiasa ama ukombozi wa bara la Afrika alizowahi kuzishika. Badala yake
tuanze kuangalia sehemu ya pili ya maisha yake ambapo sehemu hiyo haina
washabiki wengi; hata sijui sababu ni nini.
Nataka kumuangazia Mwalimu katika anga ya uandishi wa vitabu na
uanafalsafa. Naam hayati Julius Kambarage Nyerere alikuwa mwanafasihi mzuri sana . Akiamua kuyaweka
mawazo yake katika maandishi nafsi yako itafurahi. Nimebahatika kusoma kitabu
chake kinachohusu UJAMAA.
Hakika nimepata maana pana na faida ya kutosha kuhusu ujamaa wa
kiafrka ‘African Socialism’. Mwalimu katika kitabu hiki amechambua maana nzima
ya itikadi ya ujamaa, amejibu maswali yaliyokuwa yakiulizwa katika jamii juu ya
sera ya ujamaa na kujitegemea.
Watanzania wengi mwanzoni mwa miaka ya 60, baada ya uhuru
walishindwa kumuelewa Mwalimu katika sera hii ya ujamaa na kujitegemea. Wengi walitafsiri
moja kwa moja ‘ujamaa’ ni umoja, umajumui, kushirikiana. Na ‘Kujitegemea’ ni
ubinafsi, kufanya mambo kwa kujiamulia mwenyewe bila kutaka ushauri ama msaada
wa aina yoyote kutoka upande wa pili.
Hivyo wengi walikanganywa na maneno haya mawili, lakini katika
kitabu kile Mwalimu alichambua vizuri na watu wakaelewa. Hivyo nawashauri
watanzania na waafrika kusoma vitabu vilivyoandikwa na baba wa taifa hili. Uzuri
vipo kwa lugha mbili, kizungu na Kiswahili.
Kwa upande wa falsafa, sitopata wapinzani wengi katika hili. Maana
Mwalimu alikuwa na kipaji cha kuelezea jambo kwa kina na likaeleweka, hata liwe
na utata namna gani.
Wakati wa mwanzo wa utawala wale kulikuwa na utata juu ya
kuanzishwa vijiji vya ujamaa. Na lawama zikamshukia Waziri Mkuu wake Mzee Rashid
Mfaume Kawawa. Mwalimu aliacha kwanza wananchi wamalize hasira zao, baadae
alitafuta muda na kuanza kuelezea faida za vijiji vya ujamaa. Leo hii fada yake
inaonekana, vijiji vingi ambavyo baadae viligeuka miji vimetokana na vile
vijiji vya ujamaa.
Sina haja ya kuumiza kicha katika hili, yapo mambo mengi ambayo
hata hayahitaji ufafanuzi wala msomaji kuwa na elimu ama umri mkubwa kuweza
kutambua na kufahamu kuwa Mwalimu alikuwa mwanafalsafa wa kiafrika wa wakati
wake.
Tazama matatizo ya muungano alivyoyajadili kiasi kila upande
ukajiona namna walivyofanya makosa. Kifupi alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kuzungumza, na si
kuzungumza tu bali kueleweka katika mazungumzo yake.
Hivyo, ushauri wangu kwa watanzania ndiyo huo, someni sana maandishi ya
Mwalimu. Tafuteni vitabu vilivyochapisha hotuba zake musome namna alivyojua
kucheza na akili za wasikilizaji wake, wazungu wanaita ‘inspirational speaker’
Naomba niishie hapa kwa leo…..
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM ,
TANZANIA
0713 593894/ 0752 593894
14/10/2012
No comments:
Post a Comment