Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewataka wananchi kuendelea na shughuli
zao kama kawaida na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimedhibiti hali ya
ulinzi na imeimarishwa katika maeneo yote ya Zanzibar.
Taarifa ya
Serikali iliyotolewa leo usiku na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais, Mohammed Aboud Mohammed imesema Zanzibar bado ni shwari na inaendelea
kuwa katika hali ya amani na utulivu. Akizungumzia tukio la vurugu zilizofanywa
na wananchi wachache, Waziri Mohamed Aboud alisema vikundi vya vijana
vinavyosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Sheikh Farid Hadi walifanya vurugu hizo
katika mitaa ya Darajani, Michenzani, Muembeladu,Magomeni,Amani wakidai Sheikh
wao haonekani na kudhani amekamatwa na vyombo vya Dolan a kuwekwa ndani.
Waziri Mohamed Abud
alisema Serikali imewasiliana na vyombo vya Dola ikiwemo Polisi,Jeshi la
wananchi wa Tanzania, Idara ya Usalama wa Taifa, Vikosi vya Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar,KMKM,JKU,Chuo cha Mafunzo,Zimamoto na Valantia ambapo vyombo
vyote hivyo vimeeleza kutoelewa chochote kuhusu Sheikh Farid.
Waziri huyo alisema
kwamba Jeshi la Polisi limepokea taarifa ya kutoonekana kwa Sheikh Farid ambapo
kwa sasa Jeshi hilo linaendelea kumtafuta na
kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo
ili kupata ukweli wake na kuchukua hatua zinazofaa. Alisema kwamba wakati Jeshi
la Polisi likiendelea na upelelezi wake, wananchi wameombwa kutoa taarifa
kuhusu tukio hilo kwa vituo vya Polisi au kupitia Masheha, Ofisi za Wilaya na
Mikoa katika maeneo yao.
Waziri Mohamed
Aboud amesema Serikali inawasihi wwananchi waache kujiingiza katika vitendo vya
fujo na vurugu kwani kutenda hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria na Serikali
haitovumilia vitendo hivyo. Katika tukio la leo mchana, vijana hao wanaosadikiwa
kuwa ni wafuasi wa Sheikh Farid Hadi walifanya vitendo vya vurugu ikiwemo
kuchoma moto Maskazini za CCM,kuvunja maduka,kupora mali za watu na kuharibu
miundombinu ya barabara na kusababisha hasara kubwa.
IMETOLEWA NA:
IDARA YA HABARI(MAELEZO) ZANZIBAR 17/10/2012 ZANZIBAR,TANZANIA
No comments:
Post a Comment