Sunday, October 7, 2012

Maziko ya Rugambwa yavuta hisia za wengi mjini Bukoba.

 Jeneza lililobeba mabaki ya Kardinali Rugambwa likiwa limebebwa na vijana watiifu kuelekea katika kaburi lake la pili.

 Hapa akishushwa katika kaburi lake la pili ambalo ndilo litakuwa la kudumu katika kanisa alilolisimamia kujengwa.

 Hili ndilo kanisa kuu la Kikatoliki mjini bukoba na Mkoa wa Kagera kwa ujumla. Lipo Bukoba mjini njia ya kuelekea ziwani.


 Hili ndilo kanisa la Kashozi ambapo alizikwa kwa muda mwaka 1997 mjini Bukoba.


Na Reginald Miruko, Bukoba

SHUGHULI zote zilisimama mjini Bukoba jana na polisi walipata wakati mgumu kuhakikisha maandamano ya msafara wa mazishi rasmi ya Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa yanafanyika salama katika kanisa kuu la katoliki mjini hapa.
Msafara uliokuwa na magari yanayokadiriwa kuwa zaidi ya 500 uliongozwa na pikipiki na gari la polisi, ukitoka katika Kanisa la Kashozi, ulipokuwa umehifadhiwa mwili wa Rugambwa kwa miaka 15, saa 8.00 mchana na kuwasili mjini Bukoba saa 9:15.

Katika maeneo ya vijiji vya Igombe, Nyakato na Nshambya wananchi walikusanyika pembeni mwa barabara kushuhudia mwili wa Rugambwa ukisafirishwa kwenda kuzikwa rasmi ndani ya Kanisa Kuu alilolichagua, lililokuwa linafanyiwa ukarabati kwa miaka 17.

Ulipofika mjini Bukoba msafara huo wa magari ulikutana na umati mkubwa wa watu kandokando ya barabara huku wengine wakiwa wamepanda juu ya magari na hata kwenye mapaa ya nyumba, hali iliyowalazimu polisi waliokuwa wanaongoza msafara na wengine waliokuwa mjini, kufanya kazi ya ziada kuwazuia wananchi waliokuwa wanakimbia kulifuata gari lililokuwa na mwili wa Mwadhama Rugambwa.

Sehemu kubwa ya watu waliokusanyika pembeni mwa barabara walikuwa wameshiba bendera zenye picha ya Rugambwa na Kanisa Kuu ambalo alitarajiwa kuzikwa ndani yake.

Wengine walipunga mikono huku baadhi wakichukua matukio kwa kamera na simu zao za mkononi.

Msafara huo ulipofika katika kanisa hilo, ulilakiwa na bendi za Seminari ya Rubya na Shule ya Msingi Kolping zote za Kanisa Katoliki.

Katika gari hilo lililobeba masalia ya marehemu Rugambwa pia walipanda maaskofu watatu, Nestory Timanywa wa Bukoba, Almachius Rweyongeza wa Kayanga na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius
Nzigilwa.

Kabla ya maandamano hayo ilifanyika ibada katika Kanisa la Kashozi iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Askofu Yuda Thedeus Rwa’ichi na maaskofu 26 wa kanisa hilo pamoja na mapadri na
watawa zaidi 1,000.

Katika makanisa yote mawili waumini waliobahatika kuingia kanisani ni chini ya robo, wengine kwa maelfu walibaki nje ya makanisa hayo walisikiliza kupitia vipaza sauti vilivyowekwa nje, na skrini ndogo.

Hata hivyo, vifaa hivyo havikusaidia sana hali ambayo ilizua manung'uniko kwa kuwa vilishindwa kukata kiu ya waumini kushuhudia hatua kwa hatua shughuli hiyo.

Viongozi mbalimbali wa kiserikali walioshuhudia tukio hilo ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, Waziri Mstaafu wa Kilimo na Ushirika, George Kahama na Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage.

Kuhamisha mwili wa Rugambwa
Rugambwa ambaye alikuwa Kardinali wa kwanza Mwafrika alifariki dunia Desemba 8, 1997 na mwili wake kuhifadhiwa katika Kanisa la kwanza la Katoliki mkoani Kagera, Kashozi, ili kusubiri kuzikwa rasmi katika Kanisa Kuu la Bukoba alilochagua yeye.

Wakati waumini wanawasili katika Kanisa la Kashozi jana asubuhi, masalia ya mwili huo yalikuwa yamekwishawekwa kwenye jeneza jipya tayari kwa ibada na taratibu nyingine za mazishi.

Baada ya kuondolewa mwili huo, kaburi la muda ndani ya Kanisa la Kashozi lilibaki likiwa limefunikwa na mifuniko ya zege, na kwa mujibu wa Paroko wa Kashozi, Padri Anthony Rugundiza, jeneza la awali litaendelea kuhifadhiwa humo ndani kama kumbukumbu.

Mahali alipozikwa

Masalia ya mwili wa Rugambwa yalizikwa ndani ya Kanisa Kuu, sehemu ya ndani nyuma ya madhabahu, maarufu kama Sakristia, ambako maaskofu na waandishi wa habari peke yao ndio walioruhusiwa kuingia. 

Ibada ya mazishi iliongozwa
na Askofu Rwa'ichi, ikishuhudiwa na Mwadhama Emmanuel Kardinali Wamala
wa Uganda.Kaburi la Rugambwa limenakshiwa kwa vigae na kuwekewa mfuniko wa zege ulionakshiwa pia kwa vigae, ukiwa umegawanywa katika vipande vitatu ili kurahisisha ubebaji.

Pembeni mwaka kaburi la Rugambwa, kushoto na kulia, yapo mengine mawili, ambayo awali yalielezewa na Askofu Kilaini akisema ni ya akiba kwa ajili ya kusubiri maaskofu wengine watakaofariki dunia.

Kardinali Rugambwa alizikwa ndani ya Kanisa Kuu kulingana na utaratibu wa kanisa hilo, kuwa askofu yeyote wa jimbo anapofariki dunia akiwa madarakani, huzikwa ndani ya Kanisa Kuu, lakini ikiwa amekwishastaafu, huchagua Kanisa Kuu lolote katika maeneo aliyoyaongoza.

Rugambwa alichagua kuzikwa katika Kanisa Kuu la Bukoba kwa sababu ndilo kanisa kuu alilolijenga yeye alipokuwa askofu wa Jimbo la Bukoba kati ya mwaka 1963-1968.

Leo itafanyika shughuli ya kutabaruku upya Kanisa Kuu la jimbo hilo baada ya kukamilika ukarabati wake wa miaka 17, ulioanza mwaka 1995.

Matukio hayo mawili yatakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Marehemu Rugambwa Julai 12, 1912.

Chanzo: Mwananchi.

No comments:

Post a Comment