WEDNESDAY,
OCTOBER 17, 2012
Mwanzoni mwa wiki tarehe 15 Oktoba 2012 niliwasilisha kwa Katibu
wa Bunge kusudio la kuwasilisha Muswada Binafsi wa Sheria ya Marekebisho ya
Sheria ya Sheria za Hifadhi ya Jamii (The Social Security Laws (Ammendments)
Act wa mwaka 2012 kwa hati ya dharura kwa mujibu wa Kanuni ya 81 ya Kanuni za
Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007) iwapo Serikali haitatoa kauli kwa umma ya
ratiba ya kupata mapendekezo toka kwa wadau wa hifadhi ya jamii pamoja na
kamati husika ya kudumu ya Bunge kwa kuzingatia kuwa vikao vya kamati za kudumu
za bunge vimeanza tarehe 15 Oktoba 2012 bila suala hilo kuzingatiwa.
Nimefikia uamuzi huo kwa kuwa mpaka sasa ikiwa zimebaki siku
chache Mkutano wa Tisa wa Bunge kuanza tarehe
30 Oktoba 2012 ambao Serikali iliahidi kuwa italeta marekebisho ya Sheria ya
Hifadhi ya Jamii, mpaka sasa Serikali haijaitisha mkutano na wafanyakazi pamoja
na wadau wa jamii kupokea mapendekezo hali ambayo inaashiria upo uwezekano
muswada huo usiwasilishwe kwa wakati.
Lengo la Muswada huo ni kufanya marekebisho yenye kuboresha
mfumo wa utoaji wa mafao nchini ikiwemo kuwezesha kutolewa kwa fao la kujitoa
(withdrawal benefits) na mafao mengine muhimu ambayo hayatolewi katika
utaratibu wa sasa wa mifuko mbalimbali ya hifadhi ya jamii.
Kwa upande mwingine kufutwa kwa mafao ya kujitoa msingi wake
haupo kwenye marekebisho ya sheria yaliyofanyika tarehe 13 Aprili 2012 pekee
bali ni udhaifu katika mfumo mzima wa kisera na kisheria wa hifadhi ya jamii
nchini hali ambayo inahitaji wadau kutaka mabadiliko makubwa.
Hivyo, Waziri wa Kazi na Ajira kutoa kauli kwa umma kuhusu
maelekezo aliyoyatoa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya
Jamii (SSRA) baada ya mkutano wa nane wa Bunge kufuatia mapendekezo niliyotoa
bungeni ya kuitaka Wizara husika kutoa muongozo wa kisera wa kutengua taarifa
kwa umma iliyotolewa ya kueleza kuwa “kufuatia kuanza kutumika kwa Sheria hiyo
(ya 13 Aprili 2012) maombi mapya ya kujitoa yamesitishwa kwa kipindi cha miezi
sita hadi pale miongozo itakapotolewa ili kuwezesha Mamlaka na Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii kutoa elimu kwa Wadau”.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi:
John Mnyika (Mb)
15/10/2012
No comments:
Post a Comment