Hizi ni moja ya bidhaa zake.
Maafisa ubalozi wakiwa makini kuandika kila walichoona ni muhimu kutoka katika hadithi tamu ya mama huyu.
Hapa akionyesha baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa kwa kutumia mikono kutoka katika kampuni yake.
Balozi Demetrios Marantis akimuuliza swali mama Joyce wakati alipokuwa akijieleza mbele yake.
Bidhaa nyingine hizi.
Hapa Balozi Demetrios akizungumza na mama Joyce wakati walipoingia katika banda la uchoraji na utengenezaji mabatiki.
Hapa wafanyakazi wa Foot Loose wakimpa zawadi balozi huyo baada ya kufurahishwa na maneno yake.
Leo kidojembe nilihudhuria
kibanda cha mjasiriamali mama Joyce Mbwette, kulikuwa na ziara ya mtu mkubwa
kutoka serikali ya marekani ambae alitaka kujua kuhusu wafanyabiashara wa
kitanzania na namna ambavyo wanaweza kuuza bidhaa zao nchini Marekani.
Kibanda hicho cha
mjasiriamali mama Joyce kinaitwa Foot Loose Tanzania Limited, anajihusisa na
uchongaji vinyago, uchoraji picha za tingatinga, mabatiki na vikapu. Zipo
bidhaa nyingi ambazo nikianza kuzitaja mojamoja sitoweza kuzimaliza; ila ibakie
tu kuwa anafanya biashara ya kuuza mapambo ya kiafrika.
Naibu mwakilishi wa biashara
kutoka nchini Marekani au kwa kizungu cheo chake unaweza kukiita ‘US Deputy
Trade Representative’ Balozi Demetrios Marantis, anafanya ziara nchini Tanzania na inadaiwa atatembelea baadhi ya
wafanyabiashara ndogondogo za kijasiriamali jijini Dar es Salaam na mjini
Unguja kwa lengo la kuongeza nguvu mahusiano ya kibiashara baina ya Tanzania na
Marekani.
Ikumbukwe nchi ya Marekani
ipo katika kuhangaika kutafuta namna ya kushindana kibiashana na nchi ya China , kwa maana China
wameshatangaza sera yao ya mambo ya nje ni
tunakwenda Africa ‘We are going to africa ’.
Sasa wameamua kutengeneza bidhaa rahisi ili ziweze kununuliwa kwa wingi na
waafrika maskini.
Hivyo Marekani kwakuwa hawawezi
kutengeneza bidhaa rahisi wameamua kuja wenyewe ili kungalia namna ya kuwainua
wajasiriamali wa kiafrika na kuona ni namna gani wataweza kufanya nao biashara
bila kupoteza lengo na sera zao za mahusiano kwa mataifa ya nje.
Nimefarijika sana
na maelezo ya mama Joyce mbele ya mgeni wake, alijieleza vizuri sana kwa lugha ya
kikoloni ‘english’ mpaka ndugu balozi alionekana kuvutiwa na hadithi yake ya
mafanikio katika biashara.
Mama Joyce anaeleza kuwa
alianza biashara hiyo mwaka 1999, mpaka kufikia sasa ameweza kutengeneza
kampuni yeye na mume wake. Ametembea mataifa mengi yakiwemo Marekani, Ujerumani , Japan ,
Sweden
na Uingereza kuhudhuria matamasha na mikutano mbalimbali inayohusu
wajasiriamali.
“Nilianza biashara hii mwaka
1999 baada ya kuacha kazi katika benki ya bishara ya taifa NBC. Mafao yangu
niliongeza na baadhi ya vijisenti nilivyohifadhi na kuamua kufungua kampuni hii
kipindi hicho ikiwa changa sana ,”
anaeleza mama Joyce kwa furaha.
Yeye na mume wake wamepata
bahati kubwa sana ya kusaidiwa na serikali ya Tanzania kwa
kuingizwa katika baadhi ya misafara ya Rais nchi za ulaya na Marekani hivyo
kupata nafasi ya kujitangaza na kutengeneza marafiki na wateja wapya kila siku.
Anasema kampuni yake
inachangia kutoa ajira zipatazo 700, ingawa si moja kwa moja. Maana akipokea
maombi ya bidhaa nyingi kutoka ulaya ama Amerika huita watu mbalimbali wenye
utaalamu wa masuala ya uchoraji, ufinyanzi, uchongaji na ususi kisha huwapa oda
ya vitu anavyotaka na tarehe ya mwisho kuleta bidhaa hizo. Hivyo kwa mtindo huo
idadi kubwa ya vijana na kinamama hupata ajira ingawa si ya kudumu.
“Mara nyingine naweza kupokea
oda ya makontena mawili ya bidhaa mbalimbali kama
vikapu na picha za tingatinga ninachofanya ni kuita watu na kuwapa kazi hiyo
halafu mimi ninanunua kutoka kwao. Ila mara nyingi nikipokea oda kubwa kama hiyo nawaomba wateja wangu watume wawakilishi
watakaosimamia viwango vya bidhaa hizo ili isijekutokea baada ya kutuma mzigo
kwa gharama kubwa matokeo yake unakuwa chini ya kiwango na kurudishwa,”
alimuleza balozi Demetrios.
Kwa upande wake balozi
Demetrios alimsifia mama Joyce kwa kumwambia hachoki kumsikiliza kwani
anazungumza vitu ambavyo binaadamu yeyote mpenda maendeleo atatamani kusikiliza
zaidi na zaidi.
“Siwezi kuacha kusikiliza
hadithi yako ya kuvutia kuhusu biashara hii. Inaonekana wewe ni kiigizo chema
‘role model’ kwa wanamama wa kitanzania, ninapenda kupitia kwako wanamama wa
kitanzania waone namna nchi ya Marekani inavyoweza kutoa nafasi za kufanya
biashara na Tanzania
hivyo ni vema kuzichangamkia nafasi hizo,” alieleza balozi huyo.
Haya ndiyo yalikuwa majibu
yake, “leo nimeonana na mwanamke wa shoka kitu kilichonishitua kutoka kwake na
sikutegemea kukisikia ni namna alivyoweza kuwasaidia watanzania wenzie kupata
ajira. Kampuni ndogo kama hii kuzalisha ajira 700 ni kitu cha kuvutia na
kushangaza sana ,
hakika nimeshangazwa hii ni hadithi ambayo nitaikumbuka mpaka nikirudi
nyumbani.”
Waswahili wanasema ‘halifai
lakini lapumbaza’ yaani nchi ya Marekani inasemwa inanyonya nchi changa lakini
mbali ya kuwa ni mbaya lakini inasaidia kwa upande mwengine waafrika tunapumbazika
kwa misaada yake na ‘vita ya panzi furaha ya kunguru’ yaani vita ya kibiashara
baina ya China
na Marekani inatusaidia hata sisi wachanga tunakumbukwa. Tazama mtu mzito kama
huyu ambae ameteuliwa na Rais Obama na kupitishwa na maseneta ameikumbuka nchi
kama Tanzania
na kuona ni watu ambao anaweza kushirikiana nao katika biashara.
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM , TANZANIA
0713 593894/ 0752 593894
16/10/2012
No comments:
Post a Comment