Friday, October 19, 2012

Tamko la mkuu wa mkoa DSM...



MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM ATOA TAMKO NA KUSEMA SHERIA NA KANUNI ZA NCHI LAZIMA ZIFUATWE, MIHADHARA IMESIMAMISHWA MPAKA HALI ITAKAPOKUWA SALAMA NA JESHI LA POLISI LIMEJIPANGA VEMA KATIKA KUKABILIANA NA VURUGU ZITAKAZOJITOKEZA.
 Na:  Adrophina Ndyeikiza-Ofisi ya Mkuu wa Mkoa DSM 
 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Said Meck Sadiki amekutana na waandishi wa habari leo asubuhi katika Ofisi yake na kutoa tamko kuhusu vurugu zinazoendelea kujitokeza katika Mkoa wa Dar es Salaam. 

Mhe.Mkuu wa Mkoa amesema kuwa kumeibuka vitisho vya hapa na pale katika Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kukamatwa kwa Sheikh Issa Ponda ambaye anajulikana kama Katibu wa Baraza kuu na Taasisi za Jumuiya ya Kiislamu.

 “Mpaka sasa wametoa taarifa kuwa kutakuwepo na maandamano ya kuelekea Ikulu ili kushinikiza kuachiwa huru kwa Sheikh Issa Ponda na wafuasi wake”.Alisema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

 Maandamano hayo hayana kibali chochote kile ni kutaka kuibua vurugu na uvunjifu wa amani kwa wana Dar es Salaam,hivyo basi nawaomba wananchi wa Dar es Salaam kutokushiriki katika maandamano hayo kwani kwa kufanya hivyo sheria kali zitachukuliwa dhidi ya waandamanaji kwani maandamano hayo ni Haramu na hayana kibali wala tija kwa Taifa letu.

Alisisitiza Mkuu wa Mkoa. Aidha,Mkuu wa Mkoa alisema kuwa lazima tufike mahali tuishi kwa kufuata misingi ya taratibu na sheria za taifa letu kwani Sheikh Ponda hakukamatwa kama Sheikh bali kama mchochezi wa vurugu na kuwashawishi wafuasi wake kuidharau Serikali na vyombo vya usalama.Hivyo amekamatwa kama mtuhumiwa mwingine yoyote anayeweza kukamatwa. 

Hivyo basi yatupasa tuwe na subira na kufuata taratibu husika kwani kama Sheikh Issa Ponda hana hatia basi ataachiwa na kama ana hatia basi atahukumiwa kama ilivyo kawaida kwa mtuhumiwa yoyote yule akipatikana na hatia.

Hivyo basi lazima tujue kuwa nchi yetu inaongozwa kwa misingi ya taratibu na sheria na hakua aliye juu ya sheria.Sheria ipo na lazima ifuatwe. 

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema Mihadhara yote ya kidini kwa sasa imesimamishwa kwa kipindi hiki kigumu mpaka hapo hali itakapokuwa shwari. 

NAYE SHEIKH WA MKOA WA DAR ES SALAAM- Sheikh Alhadi Mussa amewataka waumini wa dini ya kiislamu kuwa na subira katika kulitatua suala hili na wasijipange kufanya vurugu ya aina yoyote kwani suala hilo limeshafika katika vyombo vya sheria hivyo tuviachie vyombo hivyo vifanye kazi yake na haki itakuja kujulikana. 

Aidha Sheikh huyo amesema kuwa ameridhishwa na maneno ya maaskofu katika kuwataka waumini wao kuwa na utulivu na si kulipiza kisasi kwani.Lakini pia amewataka waislamu nao watulie katika hilo. 

NAYE PADRI ANTHONY MAKUNDE –Katibu Mkuu wa Balaza la Maaskofu(Tech) amesema kuwa anaungana na viongozi wengine wa makanisa katika kuwasisitiza viongozi wa Dini ya Kikristo kuendelea kuwa na subira katika kipindi hiki kwani njia pekee na sahihi ya kutafuta suluhu na amani ni njia ya mazungumzo. 

KWA UPANDE WA KAMANDA WA POLISI WA MKOA WA DAR ES SALAAM- Suleimani Kova amesema kuwa Jeshi la Polisi limeungana na Mhe.Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika kukabiliana na vurugu zitakazojitokeza katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Aidha mtu yeyote akifanya kosa anachukuliwa kama mharifu kwa sababu sheria haibagui wala kuchagua yenyewe inakata kotekote haiangalii kama ni Padri au Sheikh. 

Kuhusu maandamano hayo yaliyopangwa Kamanda kova amesema kuwa Jeshi la Polisi limejipanga vema katika kukabiliana na hilo hivyo mtu yeyote akitaka kuandamana ajitahidi kutafakari mara mbili mbili itakuwaje baada ya hapo kwa yeye na familia yake.

Mwisho kabisa kamanda Kova amewataka watu hawa wajisalimishe wenyewe kwa jeshi la polisi ama sivyo sheria itachukua mkondo wake. -Mukadam Salehe -Kondo Juma -Saaban Mapeo -Jaffary Mneke -Rajabu Katimba -Amani Moshi.

No comments:

Post a Comment