Saturday, October 6, 2012

Naibu Katibu mkuu CUF Zanzibar ajiuzulu....


TAARIFA YAKE KWA VYOMBO VYA HABARI

“Leo asubuhi nimewasilisha kwa Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mheshimiwa Profesa Ibrahim Lipumba barua ya kuomba kujiuzulu nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) kwa upande wa Zanzibar , uamuzi ambao nimeomba uanze kutekelezwa rasmi tarehe 10 Oktoba, 2012. “Nimechukua uamuzi huu baada ya kuzungumza na kushauriana na viongozi wangu wa juu wa Chama ambao ni Mwenyekiti, Profesa Lipumba, Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Machano Khamis Ali na Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad takriban miezi miwili iliyopita. Nawashukuru baada ya kunitaka niwape muda wa kulitafakari walinikubalia lakini wakaniomba nibakie hadi tutakapokamilisha baadhi ya shughuli muhimu za Chama katika kipindi hichi. “Sababu kubwa zilizonisukuma kukiomba Chama kiniruhusu niachie nafasi hii ni kutokana na muda mrefu sasa kuhisi kwamba majukumu niliyo nayo ya kuwa msimamizi mkuu wa utendaji wa Chama kwa upande wa Zanzibar na wakati huo huo kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe hakunipi fursa ya kujifaragua na kutumikia nafasi zote mbili kwa ufanisi unaotakiwa. Nataka kuona kazi ya kuibana Serikali ndani na nje ya Baraza ili iwajibike zaidi kwa wananchi inaimarika zaidi. “Sambamba na sababu hiyo ni kwamba nimekusudia kutumia muda mwingi zaidi kutoa mchango mkubwa zaidi katika harakati za wananchi wa Zanzibar zinazoendelea za kuhakikisha kuwa Zanzibar inarejesha mamlaka yake kamili kitaifa na kimataifa itakayofuatiwa na kuwepo kwa Muungano wa Mkataba kati yake na Tanganyika yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa. “Harakati zinazoendelea Zanzibar kwa njia za amani na za kidemokrasia kwa kutumia mchakato wa Katiba Mpya zinahitaji kuungwa mkono na kupewa msukumo wa dhati na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochaguliwa na wananchi wa Zanzibar kwenda kusimamia maslahi yao na ya nchi yao. Nimetafakari na kuona kwamba nikiwa sina majukumu mengine ya kiutendaji nitakuwa na muda kutosha wa kulifanya hili mimi na Wawakilishi wenzangu tunaotoka CUF na CCM, vyama viwili vya siasa vilivyomo Barazani. “Nafurahi kwamba leo nimetimiza azma yangu hiyo. Pamoja na uamuzi huu, naendelea kubaki kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa. “Nawahakikishia viongozi na wanachama wenzangu wa CUF kwamba tutaendelea kushirikiana pamoja katika shughuli nyengine zote za kisiasa za Chama na kwa pamoja tutafanya kazi kuyatimiza malengo tuliyojiwekea. Naahidi kumpa ushirikiano kikamilifu mwanachama yeyote atakayeteuliwa kujaza nafasi ninayoiwacha.” HAKI SAWA KWA WOTE ISMAIL JUSSA Zanzibar 05 Oktoba, 2012 Mkandara, takashi

No comments:

Post a Comment