WEDNESDAY, OCTOBER 10, 2012
Kuanzia leo Oktoba 8 mpaka 14 vijana bila kujali itikadi
tunapaswa kuungana kote nchini kuadhimisha wiki ya taifa ya vijana. Hata hivyo,
toka wiki hii ilipoanzishwa na Serikali mwaka 2003 imekuwa ikiadhimishwa bila
mwitikio wa kiasi cha kutosha katika ngazi mbalimbali isipokuwa katika maeneo
ambayo wiki hii imekuwa ikiadhimishwa kitaifa kwa kufanya maonyesho ya namna
mbalimbali. Hivyo, nia ya taarifa hii ni kuhimiza vijana, serikali na wadau
mbalimbali ili maadhimisho ya mwaka huu yawe na hamasa na maana zaidi kwa
maisha ya vijana wa Tanzania na Taifa kwa ujumla.
Aidha, maadhimisho ya kila mwaka ya wiki ya vijana yamekuwa
yakichanganywa pamoja na kilele cha mbio za Mwenge na Maadhimisho ya siku ya
Mwalimu Nyerere kitaifa. Matokeo yake wiki ya vijana imekuwa ikifunikwa na
shamrashamra za mbio za Mwenge na hatimaye kupoteza malengo ya msingi ya
kushughulikia masuala yanayowagusa vijana moja kwa moja.
Pia zaidi ya maadhimisho yanafanyika kitaifa Shinyanga ni vyema
mkazo ukawekwa katika kufanya maadhimisho katika ngazi mbalimbali hususani
wilayani. Hivyo maafisa maendeleo wa vijana wa wilaya walau mwaka huu
wajitokeze kutembelea vikundi vya vijana, kuratibu matukio ya asasi za vijana
na kuhamasisha mijadala ya vijana kuhusu mustakabali wao na taifa kwa ujumla.
Natoa mwito kwa vijana nchini kushiriki kikamilifu katika
maadhimisho ya wiki ya taifa ya vijana ya mwaka huu iliyoanza Oktoba 8
ambayo kilele chake kitafikia Oktoba 14. Kila kijana wa Tanzania afanye walau
kitu kimoja katika wiki hii kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya jamii-kama ni
kusaidia wasiojiweza, kufanya usafi wa mazingira, kufanya majadiliano kuhusu
mustakabali wa vijana na taifa, kuonana na viongozi kuzungumza nao kuhusu
maendeleo katika maeneo yao kuhusu masuala ya elimu, ajira, afya, ukuzaji wa
vipaji vya vijana, michezo, ushiriki wa vijana katika uongozi na mengineyo.
Wiki hii ni muhimu kwa sababu kwa upande mmoja, vijana ndio kundi linaloathirika zaidi na mabadiliko ya
kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayojiri nchini kwetu na duniani kwa ujumla. Kwa
upande mwingine vijana ndio chachu ya mabadiliko katika taifa lolote duniani
kutokana na nguvu, ubunifu, na uwingi wetu.
NB: Maelezo haya kwa sehemu kubwa
yalikuwa sehemu ya Taarifa kwa Umma niliyoitoa tarehe 5 Oktoba, nayasambaza leo
kuwakumbusha kwa ajili ya hatua kila mmoja kwa nafsi na nafasi yake.
Maslahi ya umma kwanza.
No comments:
Post a Comment