SALAAM ZA MAASKOFU WA KKKT KWA WATANZANIA WOTE KUHUSIANA NA
MATUKIO YA KUCHOMA MOTO MAKANISA YA KIKRISTO ENEO LA MBAGALA – DSM.
Wapendwa Katika Bwana, Waumini wa KKKT, Wakristo Wote na Watanzania kwa Ujumla. Neema na Iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba na Bwana wetu Yesu Kristo, Amina. Sisi maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la KilutheriTanzania
(KKKT), tumepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za matukio ya uchomaji wa makanisa
katika eneo hili la Mbagala. Tumekuwa katika mkutano wetu wa Mwaka wa Lutheran
Mission Cooperation (LMC) huko Moshi pamoja na vyama vyote vya Kimissioni vya
Ulaya na Marekani. Tumelazimika kukatisha mkutano huo ili kufika hapa Mbagala.
Tumekuja kwa madhumuni makubwa matatu: Tumekuja kuwapa pole na kusimama pamoja
nanyi katika uchungu mkubwa mlio nao. Machozi yenu ni machozi yetu. Machozi
yetu ni machozi ya Kristo mwenyewe aliye Bwana wa kanisa linaloteswa. Jipeni
moyo kwa kuwa yeye aliushinda ulimwengu (Yohana 16:33). Tumekuja kuonyesha
majonzi yetu makubwa kwa vitendo vya uvunjifu wa amani, kuporomoka kwa umoja na
mshikamano wa watanzania. Huu ni msiba mkubwa, na wenye msiba ni watanzania
wote, wenye dini na wasio na dini. Tumekuja kushiriki pamoja nanyi kupokea
matumaini ya Tanzania
mpya. Katika majivu haya yaliyotokana na kuchomwa kwa madhabahu ya Mbagala , Tanzania
mpya itazaliwa. Majivu haya na machozi yenu ni rutuba ya Tanzania mpya
itakayojali upendo, uvumilivu, ustahimilivu, umoja, mshikamano, uhuru wa
kuabudu na dola isiyo na dini. Katika ujio huu wa maaskofu hapa Mbagala,
hatukuja hapa kufanya haya yafuatayo: Hatukuja kuwahukumu hata kama
hatukubaliani na wanaokashifu dini za wenzao, wawe na ruhusa kutoka mamlaka
zilizo juu au kama wanajituma wenyewe.
Hatukuja kuwahukumu hata kama hatukubaliani na
wanaodhalilisha misahafu ya dini; wawe wametumwa, kutegeshewa na mamlaka zozote
au kwa misukumo ya utashi wao binafsi ili kupata kisingizo cha kugombanisha
madhehebu ya dini. Hatukuja kuwahukumu hata kama hatukubaliani na wanaochoma
makanisa na kuiba mali
za makanisa kwa kisingizio cha kumtetea Mungu. Kisasi cha dhambi hiyo
tunamwachia Mungu mwenyewe aliyedhihakiwa na walionajisi madhabahu yake.
Wapendwa wana KKKT na watukuka sana, wana na mabinti wa Tanzania ya Julius
Kambarage Nyerere; kilichotokea Mbagala katika wiki ya kuadhimisha siku ya Baba
wa Taifa, ni kebehi si kwa Baba wa Taifa bali ni kebehi kwetu sisi wenyewe
tunaokalia kiti alichokalia Baba wa Taifa. Yeye amelala baada ya kazi njema.
Apumzike kwa amani na tunu zake zifufuke katika majivu haya yaliyotokana na
kuchomwa kwa amani na mshikamano wa Tanzania aliyoijenga. Kilichotokea
Mbagala ni mateso ya kimbari, yaani mateso ya Kanisa (Persecution). Mateso haya
ni matokeo ya mbegu ya magugu iliyopandwa katika bustani njema na sasa magugu
hayo yanazaa matunda machungu. Dalili za mateso ya kimbari kama
ilivyo kwa mateso ya kanisa; zilianza kitambo na hazikushughulikiwa na
waliomrithi Baba wa Taifa. Dalili hizo ni kama
hizi zifuatazo: Uchochezi wa wazi kuwa taifa hili linaendeshwa na unaoitwa
“mfumo Kristo”, na kuwa Baba wa Taifa alaaniwe kwa yote aliyolitendea taifa
hili. Ubishi usio na tija juu ya idadi ya waumini wa dini mbalimbali hapa
nchini na hata kudiriki kushawishi na kugomea zoezi la sensa ya watanzania.
Lengo la ubishi huu ni mbegu inayoweza kuratibisha na kurasmisha mateso ya
kimbari na mateso ya kanisa. Matumizi mabaya ya baadhi vyombo vya habari,
vyenye lengo la kujenga hofu ya kudumu na migawanyiko ya kidini miongoni mwa
watanzania Ukimya wa vyombo vya dola juu ya vitendo vya uvunjaji wa sheria ya
matumizi ya vyombo vya habari. Kwa vyovyote vile, uvumilivu wa dola hauna
maslahi mapana kwa mustakabali wa taifa letu na ni mateso ya kimbari, mateso
kwa kanisa, na kwa wantanzania wote; wawe wengi dhidi ya wachache au wachache
dhidi ya wengi. Madai yasiyo ya kawaida na ya mara kwa mara kwa serikali
inayodaiwa kutokuwa na dini. Madai hayo ni kama :
Kulazimisha uvaaji wa alama za kidini katika taasisi za umma ili kurahisisha na
kuratibisha tofauti za watanzania. Tunajiuliza: Likitokea la Mbagala katika
mashule yetu na vyuo vya umma, watachomwa wangapi na kuuawa wangapi? Madai
yanayojirudiarudia kutaka balozi za nchi fulani kufungwa hapa nchini. Madai
haya yanaashiria kutaka balozi za nchi fulani tu ndiyo ziwe hapa nchini. Madai
na mashinikizo ya Uanzishwaji wa mahakama za kidini hapa nchini Mashinikizo ya
kidini yanayoingilia mifumo ya kitaaluma na kisheria. Mashinikizo ya kidini juu
ya mfumo wa uteuzi wa watendaji wa serikali na katika ofisi za umma, Kuhoji na
kupotosha juu ya ushirikiano wa serikali na mashirika ya dini katika utoaji wa
huduma za kijamii hususan afya na elimu hapa nchini Wapendwa wana KKKT na
Wapendwa watanzania wote. Hata kama wanaofanya mambo haya ya kusikitisha
wametunukiwa hadhi ya kuitwa kuwa ni “wana harakati”, tofauti na wanaharakati
wanaotambuliwa na watanzania walio wengi, tunawiwa kuonya kwa uvumilivu wote
kuwa uana harakati wao usitumike kuvunja nchi na sheria za nchi. Tanzania yenye
amani na mshikamano ni tunda la dini zote, makabila yote, itikadi zote za
vyama, rangi zote na hali zote za kiuchumi. Hata wasio na dini wanachangia
amani ya nchi hii. Kwa macho na masikio yetu, tumeendelea kushuhudia vitendo
vya uchomaji makanisa huko Zanzibar, Mwanza, Mdaula, Mto wa Mbu, Tunduru,
Rufiji, Kigoma na sasa Mbagala. Wakati wote uvumilivu wa wakristo huenda
umetafsiriwa kuwa ni unyonge na woga. Ikumbukwe kuwa hata wanyonge na waoga,
hufika wakati wakasema “sasa basi” pale wanapodhalilishwa kupita kiasi.
Hatuombei wakristo wafikishwe hapo. Tumeshuhudia wizara zetu zikivamiwa mchana
kweupe na kushinikiza kuachiwa kwa watuhumiwa wa uhalifu; tumeshuhudia vituo
vya polisi vikichomwa moto; mahakama zikilazimishwa kufunga shughuli zake,
misikiti ikitekwa, uhai wa viongozi wa dini ukitishiwa hadharani na viongozi wastaafu
wakizabwa vibao hadharani kwa sababu ya zinazoitwa harakati za kidini.
Tumefikia kuhoji, watu hawa wavamie nini ndipo hatua zichukuliwe? Wachome nini
ndipo viongozi wenye dhamana ya kulinda mali na uhai washtuke? Wamwue nani
ndipo iaminike kuwa watu hawa ni tishio kwa usalama wa taifa letu? Sisi
tulioitwa kwa njia ya nadhiri na viapo vitakatifu, tunawasihi sana waumini wa
dini zetu na watanzania kwa ujumla, wenye wajibu wa kututii na wasiolazimika
kututii, kuzingatia kuwa Mwenyezi Mungu analipenda taifa hili na watu wake.
Kamwe hawezi kuliacha liangamie. Kwa Wakristo wote, huu ni wakati wa kuendelea
kufunga na kuomba kwa ajili ya amani ya taifa hili. Mkristo wa kweli ni yule
aliye tayari kuteswa kwa ajili ya Kristo na kanisa. Wakristo hatuko tayari kuua,
kutesa, kulipiza kisasi ili kumtetea Kristo. Mungu wetu hatetewi kwa kuua
wengine na kuchoma madhabahu ya dini nyingine. Katika mateso haya, kanisa
litaimarika zaidi; na katika majivu haya ya Mbagala , Tanzania
mpya itazaliwa na ukombozi wa kweli utapatikana. Tunawataka wakiristo wote
kusamehe na kuendelea kuwa raia wema. Kushiriki kikamilifu katika kuleta
mabadiliko ya kweli kwa kupitia njia sahihi zilizowekwa. Wakati wengine
wanaweka mikakati ya kuchoma madhabahu, wakiristo tuweke mikakati ya kuomba na
kushiriki vema katika haki zetu za uraia. Pamoja na kuwa wapole kama njiwa,
imetupasa pia kuwa na busara kama nyoka
(Mathayo 10:16).
Daima tukumbuke kuwa,
“KUSHINDANA KWETU SISI SI JUU YA DAMU NA NYAMA BALI NI JUU YA FALME NA MAMLAKA, JUU YA WAKUU WA GIZA HILI, JUU YA MAJESHI YA PEPO WABAYA KATIKA ULIMWENGU WA ROHO” (Waefeso 6: 12).
Ni sisi Maaskofu wenu kwa Neema ya Mungu
Wapendwa Katika Bwana, Waumini wa KKKT, Wakristo Wote na Watanzania kwa Ujumla. Neema na Iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba na Bwana wetu Yesu Kristo, Amina. Sisi maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Daima tukumbuke kuwa,
“KUSHINDANA KWETU SISI SI JUU YA DAMU NA NYAMA BALI NI JUU YA FALME NA MAMLAKA, JUU YA WAKUU WA GIZA HILI, JUU YA MAJESHI YA PEPO WABAYA KATIKA ULIMWENGU WA ROHO” (Waefeso 6: 12).
Ni sisi Maaskofu wenu kwa Neema ya Mungu
No comments:
Post a Comment