Wiki mbili zilizopita
kulitokea matukio mawili yaliyoongozana utadhani yalipangwa, moja lilitokea
mjini Dar es Salaam
maeneo ya Mbagala kwa kijana wa miaka 14 kuinajisi Quran. Tukio la pili
lilitokea mjini Zanzibar
baada ya kiongozi wa Uamsho Sheikh Farid kudaiwa kupotea katika mazingira ya
kutatanisha.
Matukio haya mawili ukiyapima
kwa umakini hayakupasa kutokea ikiwa Serikali yetu ingeyachukulia kwa uzito
wake na kuyaamua kwa kutumia hekima kitu ambacho hata jamii ya waislamu
walishindwa kukifanya.
Upungufu wa hekima ndicho
kilema kilichosababisha machafuko yote Zanzibar
na Bara. Pia kutumika kisiasa na mataifa ya nje hasa ya kiarabu limeonekana kwa
asilimia kubwa kuwa ni chanzo kingine. Na hili ni kwa mujibu wangu wala
sijasikia kwa mtu yeyote. Bali ni namna
matukio yalivyotokea.
Tuanze na sheikh Ponda Issa
Ponda, huyu ni katibu wa jumuiya na taasisi za Kiislamu Tanzania . Yeye
alikamatwa kwa tuhuma za kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani nchini.
Sababu kuu mbali ya vurugu za
mbagala zilizosababisha makanisa matatu kuchomwa na kuharibiwa vibaya baada ya
kijana mmoja kukojolea kitabu cha Quran ikiwa ni ubishani wa kitoto na mwenzie
ambae inadaiwa alikuwa muislamu. Alimwambia kijana huyo wa kikristo kuwa mtu
yeyote akikojolea kitabu hicho kitukufu atageuka panya au maelezo mengine
yanasema atageuka nyoka.
Sababu nyingine ya kukamatwa
kwa Sheikh Ponda ni uvamizi wa kiwanja namba 311/3/4 kilichopo Chang’ombe
karibu na uwanja wa taifa mali
ya kampuni ya Agritanza.
Nilitangulia kusema hekima
ingetumika balaa hili lisingetokea ni kuwa mtoto yule (alieidharau Quran)
tayari alikuwa mikononi mwa polisi. Kisheria ni mhalifu, maana kwa mujibu wa
katiba yetu mtu hatakiwi kudharau dini ya mwenzie kwasababu kila mtu anao uhuru
na mipaka ya kuabudu ingawa serikali haina dini. Kundi la watu kuenda kumtoa mhalifu
katika kituo cha polisi ni kosa kisheria hata huko Makka na Madina dini ya kiislamu
ilipoanza tendo hili lisingeweza kukubalika.
Simaanishi tendo la kunajisi
Quran, bali kitendo cha wananchi kuvamia kituo cha polisi na kutaka kumtoa mhalifu
mkamuhukumu mnavyojua nyinyi.
Kitu cha pili maandamano ama
vurugu zinavutia watu wengi, waislamu na wasio waislamu. Wezi na wastaarabu,
wenye akili timamu na wendawazimu. Hivyo inawezekana kabisa walioharibu
makanisa si waislamu bali ni wahuni tu
ambao wametumia mgongo wa maandamano kutimiza dhamira zao chafu.
Mafundisho ya dini ya
kiislamu hayakubali wizi (kitu ambacho kilifanyika). Mafundisho hayakubali
uharibufu wa mazingira katika vita (kitu ambacho kilifanyika) hapa nitafafanua.
Dini ya kiislamu
imefaradhisha (kukubali) vita na wasio waislamu ikiwa watawanyanyasa na kuwatoa
katika majumba yao .
Lakini katika vita hivyo Mungu na Mtume wake wamesema haitakiwi kwa Muislamu
kukata miti, kuchoma nyumba za ibada. (Tena hili hata Sheikh Basaleh imamu wa
msikiti wa Mtoro ambae sikumsikia kushiriki vurugu zile, aliwahi kulizungumza
kuwa Uislamu unaheshimu nyumba za ibada na haifai kuharibiwa hasa ikiwa wao
hawajaharibu za kwenu). Sasa elimu hii ya kuchoma makanisa imetoka wapi?
Kitu cha pili katika
kunajisiwa kitabu cha Mungu wa kweli (Quran), sikusikia kiongozi hata mmoja wa
kanisa kutoa tamko la kudharau ama kuafiki kitendo kile. Sasa kuchoma makanisa
ni kudhihirisha hasira kwa yule kijana mdogo ambae alishawishiwa na kijana
mwenzie wa kiislamu ama ni hasira kwa ukristo?
Kitu kingine yule kijana
alietoka na msahafu nyumbani kwao na kumuamuru rafiki yake aukojolee ambapo
atageuka mnyama yeye yupo wapi? Maana kama ni makosa wametenda pamoja kutokana
na utoto wao.
Hapa naomba nieleweke,
siafiki hata kidogo kitendo kile, hata kingefanywa na motto mchanga basi
ningekuwa upande wa wailsamu na si vinginevyo. Ila hatua zilizochukuliwa
kutokana na kitendo kile ndizo zinazonitatiza.
Kuhusu tukio la pili la
kuvamia kiwanja makosa ni ya BAKWATA, baraza la Waislamu Tanzania ambao kisheria
wanatambulika na Serikali. Wao waliuza kiwanja kile ambacho kisheria kilikuwa
Waqfu (Waqfu, ni mali
yoyote ambayo inawachwa kuwa urithi kwa waislamu wa eneo ama nchi. Wapo
Waislamu matajiri ambao wanakufa hawana ndugu, wanaamua mali zao
wanazitoa kwa waislamu, hiyo ndiyo waqfu).
Ikiwa bakwata ndiwo waliouza
kiwanja kile na mikataba ilishawekwa kisheria, haikutakiwa mtu msomi na mwenye
uelewa wa mambo kama Sheikh Ponda kutenda
mambo yale.
Ilitakiwa vurugu hizo
akazifanyie bakwata ambae ndie alieuza, kwa maana tayari mali ile
imeshakuwa ya mnunuaji, kumvamia ni kuingilia uhuru wa mtu. Anaweza kukuita
jambazi ama mwizi na mahakama ikakuhukumu bila mwanasheria yoyote aliekubuhu
kuweza kushinda kesi hiyo.
Kwasababu mnunuzji tayari
alikuwa na hati na mikataba yote ya kuimiliki mali ile kisheria na kitaratibu
tayari ni yak wake. Kumvamia ni uchokozi na kukosa busara.
Kosa la tatu ni pale Sheikh
Ponda alipokamatwa halafu waislamu wakaanza kuishinikiza Serikali kumwachia
kinguvu. Ni upuuzi kuingilia uhuru wa mahakama. Na huu ni ujanja mpya wa
Serikali ya Tanzania .
Wanapogundua wameteleza mahala haraka wanakimbilia mahakamani, hivyo kimsingi
waislamu walishachelewa kuitaka serikali kumuachia sheikh wao, maana mtu amabe
ameshasimama mahakamani hawezi kutolewa tena. Maana hata hiyo serikali haina
uwezo kwani mahakama ni mhimili wa dola unaojitegemea.
Kosa la nne lililofanywa na
waislamu ni pale waliposhindwa kuitumia nafasi pekee waliyokuwa nayo kuiduwaza
serikali na vyombo vyake likiwemo jeshi la polisi.
Kamanda Suleiman Kova, mkuu
wa jeshi la polisi kanda maalum Dar es
Salaam , alitamka siku ya jumatano iliyopita kuwa mtu
yeyote ambae anaona yupo chini ya Sheikh Ponda basi ajisalimishe haraka kwa
jeshi la polisi. Misikiti yote jijini Dar es Salaam ilitangaza baada ya sala ya
ijumaa kuwa watakwenda kujisalimisha kwa Kova.
Lakini cha ajabu asubuhi ya
siku hiyo mambo yakabadilishwa na kusema wanakwenda ikulu kuonana na rais
ilhali wengi walikuwa wakijua rais hayupo nchini alikuwa ziarani nchini Oman.Maana
waliona wakienda kujisalimisha serikali haitawaandama kwa mabomu kwani mtu
anaejisalimisha hatakiwi kupigwa. Na hapa ndipo ninapoamini waislamu wa Tanzania wanatumiwa na watu walio nje ya nchi
kwa maslahi yao .
Kwani watu wakiuwawa na jeshi la polisi ama kuumizwa kwao hiona ndiyo njia
sahihi ya kuionyesha jamii kuwa wanaonewa.
Ningekuwa mshauri wa waislamu
nchini ningewataka kusimamia msimamo wao uleule wa kuenda kujislaimisha kwa
Kova. Jiulize Tanzania ina
waislamu wangapi, sote tuamue Tanzania
nzima tunakwenda kujisalimisha kwa kamanda Kova kwa amani bila vurugu. Unadhani
Dar es Salaam itakalika? Wote wavae kanzu zao nyeupe huku wanataja jina la
Mungu na Mtume wake kiutulivu bila ghasia. Hilo vipi?
Wakiulizwa mnataka nini,
wajibu sisi ni wafuasi wa sheikh Ponda tumekuja kujisalimisha tunataka
kupelekwa mahakamani. Nikitaja idadi ndogo tu ya waislamu Tanzania ambao wataunga mkono wazo hilo mathalan waislamu milioni kumi wajisalimishe, sidhani
serikali itaweza kuwahudumia mahabusu milioni kumi wakati wakiendelea
kusikiliza kesi yao .
Lazima Sheikh Ponda angeachiwa huru tu hata kwa kupindisha sheria.
Tukiachana na hapa bara
tuhamie Zanzibar , sheikh wa uamsho ana lake jambo .
Maana sikubaliani na ukweli kuwa alitekwa maana jambo hili limefanyika
kimaajabu sana
hata wenye akili wameshaanza kubaini baadhi ya makosa ya kimkakati yaliyofanywa
na kikundi hicho cha wanauamsho kwa uongo walioufanya kuwa ni kweli.
Haiwezekani mtu aliekamatwa
kwa ajili ya mahojiano mazito kama hayo ya
kuhujumu nchi halafu asirudi na alama hata ya kufinywa. Mimi si mwana usalama
lakini wanausalama nawajua, hasa wanapokuwa na mtu mkaidi kama
Sheikh Farid.
Sheikh huyo anasema siku ya
tukio alipigiwa simu na mtu aliejitambulisha ni mwanafunzi wake, hakuwa akimjua
wala kuwahi kuonanan na huyo mtu aliempigia simu. Kwa Sheikh wa kikundi kama
uamsho kuenda sehemu aliyoitwa na mtu asiemfahamu tena bila ulinzi kwa kipindi
hiki ambacho Tanzania
alishatekwa kiongozi wa madaktari na kuteswa vibaya si jambo la kuingia
akilini.
Na hata maelezo ya kutekwa
kwake hayaingii akilini kwabisa. Maana anasema alipofika katika eneo la Mbweni
karibu na msikitimdogousiotumika na watu wengi aliamua kushuka na kumwamuru
dereva wake akanunue umeme, nae alikwenda msikitini kwa ajili ya haja ndogo.
Yaani ni kitu cha ajabu sana unamruhusu mtu wako wa karibu kuondoka eneo ambalo
unakwenda kukutana na mtu ambae humjui, tena kwa dharura ndogo kama ya kununua umeme kitu ambacho ungekifanya hata
wakati unarudi nyumbani.
Halafu kitu cha pili taarifa
za kupotea Sheikh huyo zilisambaa haraka zikiambatana na vurugu za kuchoma na
kuharibu maskani za CCM. Kwanini CCM?
CCM ni chama tu kama vyama
vingine, CCM si serikali, kama hasira zao
zilikuwa ni dhidi ya serikali kwanini hawakuchoma moto na kuharibu majumba ya
chama cha wananchi CUF? Maana Zanzibar sasa inaongozwa na vyama viwili CCM na
CUF ambapo inaitwa Serikali ya umoja wa kitaifa.
Halafu kupotea kwake kwanini
kunasibishwe na kutekwa? Kwanini wasingefanya subira japo baada ya siku mbili
ama tatu ndipo wakaanza kuonyesha hasira zao? Jibu ni rahisi, tayari wanauamsho
walishakuwa na hofu ya kutekwa kiongozi wao siku yoyote, sasa kwanini Sheikh
wao huyo hakuchukua hadhari mapema?
Hapa pana kitu kilitakiwa
kifanyike, vurugu zilipangwa na hata kutekwa kwa sheikh huyo pia kulipangwa na
ndiyo maana amerudi nyumbani bila mchubuko. Usifanye mchezo na chombo cha dola,
wasingekubali kumshikilia mtu kwa siku nne halafu wamuachie akatoe siri za
maswali aliyoulizwa.
Kamakweli wanataka kuitia ila
serikali ya Dk Shein rais wa Zanzibar
basi wasome historia za ukatili wa rais wa kwanza wan chi hiyo ambae alikuwa
akimkamata mtu kinachopatikana ni mwili wake tena ukiwa mfu ama una kilema cha
kudumu.
Naomba leo niishie hapa,
lakini kichwa changu kina mambo mengi sana
ya kuzungumza ambayo nimejifunza kutokana na wiki mbili hizi za vurugu. Waislam
tumeingia do asana kwa kuonekana ni wakorofi na hatuna simile.
Mathalan, wapo waislamu amabao
walitaka kuandamana mpaka ikulu ili kumsemarais kwanini amewapa pole wakristo
na kuenda kutembelea makanisa yaliyoharibiwa huko mbagala.
Sijui kama hao waislamu
wanajua walichokuwa wakikidai, jeshi la polisi lipo chini ya rais ambae ni
muislamu pia. Tayari kijana alieidharau Quran alishafika mikononi mwake rais,
hamkumpa muda afanye maamuzi mkaandamana mpaka kituo cha polisi kutaka kumpora
kijana huyo ili mumuadhibu mnavyojua nyinyi, matokeo yake badala ya kutoa
adhabu kwa muhalifu mkaamua kufanya uhalifu kwa kuharibu mali .
Ni rais wa aina gani
atakaesimama mbele ya umma ambao yeye ni kiongozi abariki uhalifu na kukiukwa
sheria za nchi? Sitaki kuamini kama wapo waislamu walitegemea baada ya wao
kuvuruga amani na kuharibu mali
asubuhi yake rais Kikwete angesimama na kusema ‘sawa sawa mmefanya kazi nzuri sana waislamu kwa kuharibu makanisa hawa wakristo ni
washenzi sana ’.
Sijui labda akili yangu haijui kufikiri lakini laiti Kikwete angezungumza
maneno hayo…..
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM , TANZANIA
0713 593894/ 0752 593894
22/10/2012
No comments:
Post a Comment