Friday, October 19, 2012

Ghasia Dar es Salaam...


Ghasia zimekumba mji mkuu wa Tanzania Dar es Salaam kufuatia maandamano kuhusiana na kukamatwa kwa kiongozi wa dini ya kiislamu sheikh Ponda Isa Ponda.
Waumini wa dini hiyo wamekabiliana na polisi punde tu baada ya sala ya ijumaa.
Ghasia zilitokea katika mtaa wa Simbazi eneo la Kariokor na kupelekea maduka kufungwa huku watu wakitawanyika kukimbilia usalama wao.
Mwandishi wa BBC mjini humo Eric David Nampesya alisema kuwa polisi walitumia gesi ya kutoa machozi ili kuwatawanya watu kadhaa waliokuwa wamekusanyika wakitishia kuandamana hadi katika eneo la Kidongo Chekundu kudai malalamiko kadha wa kadha.
Kikosi cha jeshi la polisi kilishirikiana na polisi mjini Dar Es Salam kukabiliana na waandamanaji waliokuwa wamesema watafanya maandamano baada ya sala ya Ijumaa.
Sheikh Ponda alikamatwa kwa madai ya uchochezi.
Kwingineko kisiwani Zanzibar polisi walipambana na makundi ya vijana waliokuwa wanataka kuachiliwa kwa kiongozi wa kidini Farid Adi, aliyetoweka siku ya Jumanne usiku. Serikali imesema kuwa haijahusika kivyovyote na kutoweka kwa sheikh Adi.
Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kutawanya makundi ya vijana waliokuwa wanafanya vurugu.
Afisa mmoja wa polisi aliuawa katika ghasia zilizofanyika siku ya Jumatano baada ya taarifa za kutoweka kwa sheikh Adi kutolewa. Polisi wamewakamata watu kadhaa kuhusiana na vurugu hizo.
Chanzo: BBC Swahili.

No comments:

Post a Comment