Monday, October 1, 2012

Kunguru weusi kuangamizwa na wizara ya maliasili na utalii.


Wizara ya Maliasili na Utalii itaendesha zoezi la kuwaangamiza kunguru weusi katika mikoa ya Tanga na Pwani kuanzia tarehe 2 Oktoba hadi 1 Novemba 2012 kwa kutumia sumu tulivu aina ya DRC 1339. Zoezi hilo limehamia katika mikoa hiyo baada ya kukamilika mkoani Dar es Salaam ambako liliendeshwa kwa mwezi mzima tangu tarehe 27 Agosti 2012 hadi 25 Septemba 2012.

Katika zoezi hilo jumla ya kunguru 41,487 waliuwawa Jijini Dar es Salaam. Aidha, tangu Mradi wa kudhibiti kunguru weusi uanze Mwezi Julai 2010, hadi Septemba 2012 jumla ya kunguru weusi 807,961 wameshauawa kwa kutumia sumu hiyo ya DRC 1339 na mitego katika Mikoa ya Dar es salaam, Morogoro, Pwani na Tanga. Ingawaje sumu hiyo haina madhara makubwa kwa binadamu, wananchi hasa watoto, wanatakiwa kutochezea mizoga ya kunguru ambao watakuwa wamekufa kutokana na sumu hiyo.

Endapo mtu atakuwa ameishika mizoga hiyo anatakiwa anawe kwa sabuni. Kunguru weusi wanauwawa kwa lengo la kupunguza idadi yao ili wasiendelee kusababisha kero kwa wananchi kwa kupokonya chakula na vitu mbalimbali. Aidha, kunguru wamekuwa wakieneza vimelea vya magonjwa mbalimbali kwa binadamu na kuku. Wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano kwa vikosi ambavyo vitakuwa vinaokota mizoga ya kunguru, kwa kuonyesha iliko.

Pia wanatakiwa kutoa taarifa pale watapogundua kuwa kuna idadi kubwa ya ndege hao sehemu yoyote ili hatua za kuwaangamiza ziweze kuchukuliwa. Taarifa zipelekwe katika ofisi za Maliasili za Mikoa, Wilaya, na Manispaa. Pia wanaweza kupiga simu 0716 129120 kwa Mkoa wa Pwani na 0757 585358 kwa Mkoa wa Tanga. Zoezi la kuwaangamiza kunguru weusi litahamia mkoani Morogoro tangu tarehe 5 Novemba 2012 ambako litaendeshwa kwa muda wa mwezi mzima.

Baada ya kumalizika kwa zoezi katika mkoa huo Wizara itafanya tathmini ili kuona mafanikio ya operesheni hii. Tathmini katika mikoa yote minne (Dar es Salaam, Pwani, Tanga, na Morogoro) itafanyika kwa pamoja kwa kuwa kunguru wanaoonekana katika mkoa mmoja ndiyo walewale ambao huzungukia mikoa yote inayopakana nao.

George Matiko, MSEMAJI WIZARA YA MALIASILI NA UTALII 1 Oktoba 2012 Simu : +255 784 468047

No comments:

Post a Comment