Na Hafidh Kido
Nchi nyingi za kiafrika
zimekuwa zikiingia katika machafuko ya kisiasa mara baada ya kugundua utajiri
wa mafuta na gesi asilia.
Sababu zinaweza kuwa ni
usimamizi mbovu wa mikataba na mgawanyo wa rasilimali hiyo kwa wananchi
kunakoibua chuki za wananchi wanapobaini kuibiwa rasilimali zao na wazungu
ambao hawawanufaishi chochote zaidi ya kuendelea kuwadidimiza katika umaskini.
Kibaya zaidi hawa wanaojiita
wafadhili hawaishi kuzinyooshea nchi za kiafrika kidole cha lawama kuwa hawana
usimamizi bora wa rasilimali zao ilhali wao kwa namna moja ama nyingine hushirikiana
na makampuni ya kibepari kuchota mafuta katika nchi maskini huku
wakichonganisha makundi katika nchi hizo ili yatokee mapigano ambayo huwapa
mwanya wa kuja tena kama wasuluhishi.
Mwanzoni mwa mwaka huu waziri
mwenye dhamana ya nishati na madini nchini Prof. Sospeter Muhongo, alitangaza
habari njema ya kupatikana mafuta na gesi kilomita 80 kutoka pwani ya Lindi
katikati ya bahari.
Makampuni mawili ya Marekani
na Norway
(Statoil na Exxan Mobil) yaliyopewa kazi ya kutafuta mafuta kwa miaka mitatu
walitoa habari njema kwa kueleza kuwa kuna gesi inayofikia zaidi ya futi za
ujazo trilioni 20.
Prof. Muhongo, aliendelea
kueleza kuwa takriban makampuni 19 yalikuwa yakitoa ushirikiano katika
utafutaji huo, na kubainisha kuwa kisima kimoja kimeigharibu Serikali dola za
Kimarekani milioni 100 mpaka 150 katika kufanya upembuzi yakinifu.
Hatua ya pili ambayo
watanzania walikuwa wakiisubiri kwa hamu kutoka Serikalini ni namna rasilimali
hiyo itakavyochimbwa na kuinufaisha nchi.
Ni kama Serikali imeligundua hilo na kutangaza rasmi kuwa leseni za uchimbaji
hazitotolewa mpaka hapo Serikali itakapojipanga katika sera na sheria
zitakazoelekeza namna gani wataingia mikataba na makampuni ya uchimbaji mafuta
na gesi bila kupata hasara ama mikanganyiko kama
wanayoipata katika madini mengine hasa Dhahabu, almasi na tanzanite.
Kituo cha sheria na haki za
binaadamu nchini wakishirikiana na asasi nyingine za kiraia za SIKIKA na Hakielimu
waliweka wazi msimamo wao kwa kuitaka Serikali kutosimamisha kwa muda bali
wasitishe kabisa mchakato wa uchimbaji mafuta na gesi ili wajipange.
Mkurugenzi wa SIKIKA Irenei
Kiria, alisema katika nchi nyingi duniani mafuta na gesi vimekuwa na msaada
mkubwa katika kuinua uchumi lakini kwa Tanzania hali itakuwa tofauti ikiwa
hatua stahiki hazitofuatwa.
Kilio kikubwa cha Kiria
kiliegemea upande wa wataalamu wazalendo na namna ya ukusanyaji kodi, mirabaha
kutoka kwa makampuni ya kigeni ambayo mara nyingi wao ndiwo wanaojihusisha na
uchimbaji huo hasa ikizingatiwa shughuli hizo zinahitaji mitaji mikubwa na ujuzi
wa hali ya juu.
“Tusifanye maamuzi yasiyo na
tija, bado hatujajiandaa kwa wataalamu wa kutosha juu ya masuala ya mikataba na
usambazaji mafuta na gesi. Serikali imesitisha suala hili kwa muda lakini sisi
tunasema isimamishe kabisa mpaka hapo nchi itakapojitosheleza kimkakati juu ya
rasilimali hizi.
“Kwa hivyo mchakato mzima wa
utafutaji, uchimbaji na usambazaji gesi asilia na mafuta sambamba na mikataba,
leseni, usimamizi, ukusanyaji kodi na mirabaha lazima isimamiwe vyema kwa uwazi
na ushirikishwaji wa hali ya juu ili kila mwananchi ajiridhishe na kuona
upatikanaji wa rasilimali hizi ni faida kwa nchi na maendeleo kwa ujumla,”
alisema Kiria.
Aidha muungano wa taasisi hizo
tatu ulisisitiza uundwaji wa sera na sheria zitakazolinda mchakato wa upatikanaji
gesi na mafuta ili kuhakikisha nchi haiingii katika matatizo kama mifano
inavyoonekana katika nchi nyingi za kiafrika ambapo upatikanaji wa mafuta umekuwa
na laana badala ya baraka.
Kwa upande wake meneja wa
utafiti na sera Hakielimu Godfrey Boniventure, alisema Tanzania mpaka
sasa haijaandaa hata mzalendo mmoja kuweza kupata nafasi ya kutoa huduma katika
uzalisahji na usambazaji mafuta na gesi. Hii ikijumlisha wataalamu wa
uchimbaji, usambazaji na hata watu wa kawaida watakaotumika kama
washauri juu ya rasilimali hizo adimu duniani.
“Hatutaki kusikia hadithi ya
kasungura kadogo, huu ni wakati wetu watanzania tunatakiwa kuitumia nafasi hii
kujinufaisha kiuchumi na kijamii. Serikali ipange mikakati na kuhakikisha
tunapata sera na sheria muafaka kulinda rasilimali hizi,” alisisitiza
Boniventure.
Hivi karibuni, Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango ambaye pia ni
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe alikaririwa na vyombo vya
habari akisema kitu hichohicho kuwa Serikali inapaswa kusitisha utoaji wa
leseni za utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta kwa miaka 10 ili ijipange na
kuweza kumudu kusimamia yenyewe uvunaji wa rasilimali hiyo.
Nilipozungumza na Zitto kwa
njia ya simu alinieleza kuwa Serikali lazima iwe makini sana
katika suala la mafuta maana rasilimali hii ni ya watanzania tofauti na madini
ambapo makampuni ya uchimbaji yanapopewa vibali madini yanakuwa ni yao .
“Watu hawajui kitu kimoja,
mafuta ni mali
ya taifa tofauti na madini mengine. Makampuni yanapokuja kuchimba mafuta ama
gesi wanachopata kutoka kwetu ni tozo la shughuli ya uchimbaji ila
kinachopatikana ni mali
ya Serikali.
“Kwa mfano ikiwa kampuni
itatumia gharama ya dola 20 kuchimba pipa moja, hicho ndicho kiasi
wanachotakiwa walipwe labda na faida kidogo lakini mafuta yetu hawayagusi hata
tone. TPDC na TRA wanachotakiwa kufanya ni kuhakikisha wanasimamia mikataba na
kuwabana wawekezaji wababaishaji ambao mara nyingi hutumia ujanja kuiibia
Serikali wakishirikiana na viongozi walafi, naamini sheri na sera zipo
kinachokosekana ni utekelezaji tu” alisema Zitto.
Nilichojifunza kutoka katika
kauli ama msimamo wa Zitto ni namna Serikali na vyombo vyake wanavyotakiwa
kujiandaa kukabiliana na ubabaishaji wa makampuni ya kigeni ambayo muda si
mrefu yataanza kutiririka kuomba nafasi ya kuchimba mafuta.
Ni muhimu sheria ya kusimamia
mafuta na gesi itungwe ili kuhakikisha
mgawanyo wa mapato unafikia malengo kwa kuelekezwa katika shughuli za ujenzi wa
barabara, hospitali, shule na mambo mengine muhimu ambayo yatainua uchumi ili
kila mwananchi aone kuna mabadiliko chanya mara baada ya kugundulika rasilimali
hii adimu duniani.
Zitto hakuishia hapo tu
lakini aliitaka Serikali kujenga chuo mkoani Mtwara ambacho kitapika wataalamu
wa uchumi na mikataba katika masuala ya gesi na mafuta.
“Si lazima tukawa na
wataalamu wa uchimbaji mafuta tu, mimi maoni yangu jamii ya watanzania ikodolee
macho sana
katika masuala ya mikataba na mahesabu ya uzalishaji mafuta. Hapa ndipo nchi
nyingi za kiafrika zinapoibiwa rasilimali zao, lazima tupate wataalamu
wazalendo ambao watakuwa wameiva katika uchumi wa mafuta na mikataba, tuwe na
watu ambao wanaweza kubishana na kung’amua ujanja wa makampuni haya ya kigeni.
Kujua nchi itapata asilimia ngapi na mchimbaji anapata ngapi hapo ndipo
tunapoibiwa, kadhalika gharama za kuchimba pipa moja na namna ya kuwalipa
wachimbaji, hapo ndipo tunapoibiwa.
“Unajua nimejifunza mambo
mengi sana katika makampuni haya ya kigeni,
wanatuibia sana
maana wana wataalamu wa hali ya juu katika masuala ya mikataba na uchumi, sisi
bado tupo nyuma na hapo ndipo wanapotuibia.
“Vilevile tutumie nafasi hii
kuwapa ajira vijana maana katika uchimbaji mafuta baharini kunatumika meli
ambazo zinahitaji mabaharia. Kwa mfano kwa sasa kule Mtwara kuna meli nne za
utafutaji mafuta na kila meli inaajiri wastani wa mabaharia 400 kwa mwezi 200
kila baada ya wiki mbili wanaingia kwa kupokezana. Lakini watanzania wapo
wachache sana wengi ni raia wa kigeni na hata
vyakula wanavyokula wakiwa melini vinatoka nchi jirani ya Kenya
watanzania tumelala tu,” alisisitiza.
Nimeielewa mantiki ya kauli
yake, ni kuwa si wataalamu waliosoma tu lakini hata ambao wana elimu ya chini
wanaweza kupata ajira katika uchimbaji mafuta, mathalani mafundi mchundo
wanaweza kupata ajira melini na kuchomea mabati ya meli, ama wapishi na hata
wauza vyakula kwa wafanyakazi wa meli za uchimbaji mafuta.
Serikali inaweza kuweka
sheria ya kuwabana wageni kutojihusisha na shughuli ndogondogo kama hizo. Kama watakuja
wataalamu wa utafutaji na uchimbaji mafuta basi wasije na wafanyakazi bali
wafanyakazi watoke hapahapa.
Na hivi ndivyo nchi za
kiarabu zilivyofanikiwa katika uchumi wao, ni kwa njia hii hii ya kuwabana
wageni wasifanye shughuli ambazo wazawa wanaweza kuzifanya tena kwa uwezo
mkubwa kuliko wao.
Leo ukienda nchi yoyote ya
kiarabu ama kirusi katika machimbo ya mafuta huwezi kupata kazi kirahisi,
unaweza kukuta mtaalamu mkuu wa uchimbaji ni mzungu lakini wasaidizi wake wote
ni waarabu. Maana yake baada ya miaka kadhaa ijayo hawatahitaji wataalamu
kutoka nje bali watakuwa na wataalamu wao wazalendo walioiva, nchi inapata
faida na wananchi wanapata ajira.
HAFIDH A. KIDO
DAR ES SALAAM , TANZANIA
0713 593894/ 0752 593894
03/10/2012
No comments:
Post a Comment