"MZIGO MZITO APEWE MNYAMWEZI".
Historia ya Tanzania
ina mengi na ina wengi ambao hawajazungumzwa, kiasi ambacho kuna mambo
yakizungumzwa basi yanaweza kukusisimua na kukufanya ujisikie fahari sana kuwa Mtanzania.
Leo tunamzungumza Mzee wetu Mashuhuri Ameen Kashmiri. Askari Mstaafu wa Jeshi
la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambaye historia ya maisha yake inatupa mafunzo
na kutufamamisha mengi sana
ambayo hatukuwa tukiyajua.
Ameen Kashmiri alizaliwa tarehe 31 mwezi Oktoba mwaka 1935 huko Mjini Tabora
wakati huo kukijulikana kama Jimbo la Magharibi, sehemu kubwa ya maisha yake ya
utottoni ameyatumia huko wakati Baba yake ambaye alikuwa Mfanyakazi wa Shirika
la Reli la Tanganyika
alipokuwa kwenye Tawi hilo
la Tabora.
Maisha ya Wafanyakazi wa wakati huo yalikuwa ya kuhamahama sana
jambo ambalo lilimfanya Mzee Kashmiri asikae sana Tabora. Alihamishiwa Mkoani Dodoma,
kisha Dar es salaam ambako nako hakukaa sana kabla ya kuhamishiwa
Jimboni Tanga ambako ndipo sehemu alitumia sehemu kubwa ya maisha yake na ndipo
Elimu na Mafunzo ya Mwanawe Ameen yalipopatikana.
WITO WA KUTUMIKIA UMMA, UBAGUZI KWA WATANGANYIKA.
Mwaka 1956 Bwana Ameen Kashmiri alihitimu Elimu yake ya Upili (Sekondari)
katika Skuli Maarufu Jijini Tanga iliyojulikana kwa jina la Shule ya Karimjee
(Sasa hivi ikijulikana kama Shule ya Sekondari Usagara), ambapo kwa wakati wake
alikuwa mmoja ya wanafunzi wenye uelewa mkubwa sana.
Tokea Shuleni yeye na baadhi ya Wenzake walivutiwa sana na habari na masimulizi
ya Ushujaa, Ujasiri na kusisimua ya wazee wengi wa Tanga ambao walikuwa Sehemu
ya Jeshi la Wakoloni wa Kiingereza lililokwenda Burma na Somalia wakati ule wa
Vita Kuu ya Pili ya Dunia, na hivyo kuwafanya wavutiwe sana na wawe na wito wa kuwa
Maaskari Jeshi.
Mara tu alipomaliza Shule alifanya jitihada mbalimbali za kuomba kujiunga na
Jeshi lakini mara zote alikataliwa. Pamoja na kuwa alionekana mweupe kwa rangi
tofauti na Watanganyika wengine lakini bado alibaguliwa na Maofisa wa Kikoloni
kwa kuwa Rangi yake haikuondoa Utanganyika wake au kubadili lafudhi yake ya
Kiswahili safi, kwa wakati husika Askari wa Jeshi la Kikoloni la Tanganyika
(Kings African Rifles) hawakuwa wakipenda sana kuwaingiza vijana wa
Kitanganyika Jeshini kwa sababu mbalimbali.
Akiwa kakatishwa tamaa kwa kukataliwa kwake kuingia Jeshini, Ameen alikataa
kuomba nafasi mbalimbali za kazi ambazo zilikuwepo kwa watu wa kiwango chake
cha elimu kwa wakati huo. Baada ya Ushauri na kubembelezwa sana
na baba yake aliamua kukubali ajira ya Uhasibu katika Kampuni ya Tom Co. Ltd
kazi ambayo pamoja na kuwa hakuipenda lakini aliifanya kwa ufanisi sana kiasi kwamba baada
ya muda tu alipandishwa cheo na kuwa Mhasibu Mkuu wa Kampuni.
MCHAKAMCHAKA, ASKARI MKAKAMAVU AMEEN KASHMIRI.
Mwishoni mwa Mwaka 1957 Jeshi la Wakoloni lilifungua Milango kwa Vijana wa
Kitanganyika kujiunga nalo. Wakati huo wito na kampeni ilifanywa nchi nzima ili
kuwahamasisha na kuwasajili vijana mbalimbali ambao walitaka kujiunga na Jeshi
hilo nafasi ambayo Mzee Ameen hakuiacha impite hivi hivi, hivyo akawa miongoni
mwa vijana wachache wenye Elimu wa Kitanganyika wa wakati huo kukubali kujiunga
na Jeshi hilo.
Baada ya Maombi na Usaili mwezi Januari mwaka 1958 Mzee Ameen Kashmiri, Mrisho
Sarakikya na Alex Nyirenda walichaguliwa kujiunga na Mafunzo ya Juu ya Kijeshi
katika Chuo cha Royal Military Academy, Sandhurst, Nchini Uingereza ambapo
baadaye Mzee Mrisho Sarakikya aliachwa katika Orodha ya Wanafunzi waliotakiwa
kwenda Uingereza kwa sababu ya Ufaulu wake mdogo kwenye Somo la lugha ya
Kiingereza. kabla ya kwenda huko Nchini Uingereza kwa ajili ya Mafunzo yao ya Juu ya Kijeshi kwanza walipelekwa Nairobi Nchini Kenya na kisha Jinja Nchini Uganda kwaajili
ya Mafunzo ya kawaida ya Kijeshi.
Mafunzo ya Kijeshi yaliyokuwa yakifanyika Nairobi
na kisha Jinja Nchini Uganda
yalihusisha pia Vijana kutoka Kenya
na Uganda, ambapo wakati
wakimalizia mafunzo kule Jinja ni watu nane (8) tu katika kundi zima ambao
walichaguliwa kujiunga na masomo ya Juu ya Kijeshi ambapo watatu walitoka Kenya na Tanganyika alikuwa ni yeye na
Nyirenda tu baada ya kuondolewa kwa Sarakikya.
MAFUNZONI, JASIRI AMEEN KASHMIRI ALIYEWEKA MSINGI.
Mzee Ameen na vijana wenziwe walipokelewa vizuri tu Nchini Uingereza, lakini
Bodi ya Uchaguzi wa Jeshi la Uingereza iliwachagua yeye na kijana wa Kizungu
kutoka Kenya moja kwa moja
kwenda Chuoni Sandhusrt na wale wenzao waliobakia (akiwemo na Nyirenda)
walipelekwa katika Chuo cha Mafunzo cha Makuruta cha Mons kabla ya kurudisha kujiunga na kina
Ameen miezi sita (6) baadaye.
Mwezi Juni mwaka 1960 alimaliza mafunzo na kufaulu kuwa Askari Jeshi Luteni
mwenye Nyota Mbili (Second Lieutenant) ambapo alikuwa mtu wa kwanza kufaulu
chuoni hapo kutoka katika Nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Mara baada ya kumaliza Mafunzo yake Ameen Kashmiri alirudi Tanganyika na
kujiunga na kikosi Namba sita cha King's African Rifles katika Kambi ya Calito
(sasa Lugalo).
KIKOSI CHA BENDERA, MZALENDO AMEEN KASHMIRI.
Mwaka 1961 Tanganyika
ilipata Uhuru wake kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza, Usiku wa kuamkia tarehe 9
Desemba mwaka 1961 kulikuwa na Shamra shamra nyingi sana
ikiwemo kitendo cha Mzee Nyirenda kuupandisha Mwenge wa Uhuru kwenda katika
kilele cha Mlima Kilimanjaro na matukio mengine mengi sana ya kusisimua.
Mzee Ameen Kashmiri alikuwa katika Kikosi cha Bendera kwenye Sherehe za Uhuru
zilizofanyika katika Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) Jijini Dar es
salaam asubuhi ya siku hiyo ya Uhuru. Ameen alibeba Bendera ya Uhuru ya Tanganyika (kama anavyoonekana pichani) ambayo
ilipandishwa Juu siku hiyo huku askari mwenzie akiwa amebeba Bendera ya
Wakoloni wa Kiingereza ambayo ilishushwa rasmi siku hiyo na Kiongozi wa
Harakati za Uhuru wa Tanganyika Mwalimu Julius K Nyerere kuashiria Uhuru kamili
wa Tanganyika.
MASHUHURI AMEEN KASHMIRI, MBEBA BENDERA YA MATUMAINI YETU.
Jukumu kubwa na zito la kubeba Bendera ya Tanganyika
katika siku ile ya kukumbukwa linaonyesha weledi, kuaminiwa, ujemedari na
uzalendo wake ambao haukuwa na mashaka kwa Taifa hili, tukio hilo
ni kiashiria na kielelezo cha umuhimu na mchango wake katika Historia njema ya Tanganyika.
Yeye binafsi siku zote anasema hawezi kulisahau kabisa tukio hilo mpaka kufa
kwake, kwake ni tukio lenye kubeba ufahari wa kitanzania, umashuhuri wa
kizalendo na ujemedari wa uaminifu wa kitumishi kwa umma wa Watanzania. Heshima
ambayo alipewa na wanawema wenziwe haina mithali kwake.
Tukio la Mzee Ameen Kashmiri kubeba bendera ile ya Matumaini ni jambo lenye
kusisimua sana nyonyoni mwetu watanzania wote mpaka leo hii, kumbukumbu njema
za tukio hilo kwa wale waliokuwepo siku hiyo ni jambo la kifahari na
linarithisha Uzalendo na kuipenda Nchi kwa sisi Vijana wadogo wa Kitanzania
ambao hatukuwepo wakati ule, ni tukio adimu lenye kumfanya Mzee Ameen Kashmiri
kuwa Mtu Mashuhuri sana nyoyoni mwetu.
MAASI YA KIJESHI, USULI WA "AFRICANIZATION".
Usiku wa kuamkia Januari 21, 1964, Jeshi la Tanganyika liliasi na kushikilia
serikali kwa muda, tukio ambalo Baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, alilielezea kuwa ni “siku ya aibu sana kwa Taifa”. Wakati jeshi hilo likiasi siku hiyo hiyo, na saa hiyo hiyo, majeshi ya Kenya na Uganda nayo yaliasi kwa staili hiyo
hiyo. Maasi yote ya nchi tatu hizo yalizimwa na majeshi ya Uingereza siku moja
na wakati huo huo. Kwa Tanganyika, maasi haya yalitokea wiki moja tu baada ya
mapinduzi ya umwagaji damu ya Zanzibar, Januari 12, 1964; na usiku huo wa maasi
hayo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Zanzibar “Field Marshal” John Gidion Okello,
alikuwa na mazungumzo na Mwalimu Nyerere Ikulu, Dar es Salaam, katika hali ya
kubadilishana mawazo juu ya hali ya Zanzibar ambapo Mwalimu, alimshauri Okello
afanye kazi kwa imani na Rais Abeid Amani Karume.
Mara baada ya Uhuru Tanganyika
(sasa Tanzania
bara) ilirithi Jeshi kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza lililokuwa likijulikana
kama “Kings African Rifles” – (K. A. R) na baadaye kuitwa “Tanganyika Rifles”
(TR). Katika kipindi kufuatia uhuru, ili kukidhi matarajio ya Watanganyika,
zilitakiwa hatua za haraka kuhakikisha nafasi zote za juu serikalini na taasisi
zake (likiwemo jeshi), zinashikwa na Wazalendo. Huu ni utamaduni uliokuwa
umejengeka kwa nchi zote za Kiafrika zilizokuwa zikipata uhuru
Nyerere hakuwa na ujasiri wa kuchukua hatua haraka hivyo, kama
pia ambavyo Waziri wake wa Mambo ya Ndani wa wakati huo, Clement George Kahama,
hakuwa na ujasiri wa kuwatimua Waingereza katika nafasi za juu ndani ya Jeshi
la Polisi. Yakaanza malumbano ndani ya Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Tawala,
Tanganyika African National Union (TANU), kwamba Nyerere alikuwa anairudisha
Tanganyika katika enzi za Ukoloni, na hivyo kwamba “uhuru” haukuwa na maana kwa
Watanganyika kwa kushindwa kwake kuwapa vyeo Waafrika.
Ili kuepusha shari, na ili Chama kisifarakane, Mwalimu akaachia ngazi Januari
16, 1962 na kurejea kijijini kuimarisha Chama kama
Mwenyekiti wa Taifa wa TANU na Rashid Kawawa akachukua Uwaziri Mkuu. Naye Oscar
Kambona, ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Elimu, akawa Waziri wa Mambo ya
Ndani badala ya George Kahama. Wote wawili hao wakaachiwa kazi ya kuwaondoa
Wazungu katika vyeo walivyokuwa bado wanashikilia haraka bila visingizio.
Kazi ya kwanza ya Kambona ilikuwa ni kumtimua Kamishna wa Polisi Mwingereza, na
kumteua Bwana Elangwa Shaidi kuchukua nafasi hiyo, lakini hakufanya mabadiliko
kwa Jeshi (Tanganyika Rifles).
Zoezi hili la “Africanisation” lilifanywa kwa kasi ya kutisha kiasi cha
kuishitua jamii ya Kimataifa. Desemba 1962, ulifanyika Uchaguzi Mkuu ambapo
Mwalimu Nyerere alichaguliwa kuwa Rais Mtendaji wa kwanza. Kwa hiyo, Januari
1963, Mwalimu alirejea madarakani kama Rais wa kwanza wa Tanganyika na
kusitisha mara moja zoezi la “Africanisation” na kuchochea hasira ya viongozi
wa Vyama vya Wafanyakazi nchini, ambao waliapa kutolala usingizi, wala kuupa
nafasi uamuzi wa Mwalimu wa kusisitiza zoezi la kuwapa madaraka Watanganyika.
AMEEN KASHMIRI CHINI YA ULINZI, ASKARI WA KWANZA
WA CHEO CHA JUU KUKAMATWA.
Matata yalianza usiku wa Januari 20, kuamkia 21 usiku huo, siku ambayo Okello
alikuwa na mazungumzo na Mwalimu, Ikulu usiku. Mzee Ameen Kashmir anaikumbuka sana siku hii kwa kuwa
yeye ndiye Aliyekuwa Ofisa wa zamu wa wiki ile.
Saa 11 jioni alianza utaratibu wa kichunguza (routine inspection) kwa kuanzia
Eneo la Ikulu na kisha kupita katika maeneo yote nyeti ya Nchi ambapo kila kitu
kilionekana kuwa shwari na hakukuwa na vishiria vyovyote vya uwepo wa tukio la
Jeshi kuasi.
Mara baada ya ukaguzi huo kwenye maeneo nyeti ya Nchi aliamua kurudi katika
kambi kuu ya Colito ambapo alishangazwa sana
na hali ya kukuta taa zote za kambi zikiwa zimezimwa jambo ambalo halikuwa la
kawaida lakini aliondoa hisia mbaya na kuhisi labda kulikuwa na matatizo ya
umeme kambini hapo.
Wakati alipokuwa amevalia Sare zake maridadi za Jeshi alijitambulisha kama
Askari wa Zamu wa Jeshi wa wiki, ambapo mara baada ya Geti kuu kufunguliwa na
yeye kuingia alishangaa anawekwa Chini ya Ulinzi na Askari wenzie jambo ambalo
halikumshangaza kwa kuhisi ni utani tu.
Baada ya muda aligundua kuwa kilichokuwa kinatokea si utani tena na ni uasi
kamili wa Jeshi ambapo yeye alikuwa Afisa Mkuu wa Kwanza
kuwekwa ndani, kisha king'ora kilipigwa kambini hapo kuashiria kutakiwa kwa
askari wote kukusanyika katika uwanja, ambapo wasaa huo ndiyo ulitumika
kuwaweka chini ya ulinzi Askari wengine wa kizungu waliokuwa na vyeo vya juu.
Lakini ilipofika saa 7:50 alfajiri, Januari 21, Mkuu wa Kikosi cha kwanza cha
TR, Brigedia Patrick Sholto Douglas, aliamshwa nyumbani kwake na sauti ya
baruji (buggle) na ving’ora, karibu na kambi ya Jeshi ya Colito (sasa Lugalo
Barracks).
Alipotoka nje, aliona askari wake 12 wakikamatwa na wenzao wenye silaha na kutiwa
mahabusu. Ndipo alipofahamu kwamba, nusu ya askari 800 wa Kikosi hicho walikuwa
wameasi. Aliweza kutoroka yeye na familia yake hadi katikati ya jiji, akaiacha
familia kwa Balozi wa Australia,
kisha akakakimbilia kwa Afisa mwenzake, eneo la Oyster Bay na kutumia wasaa huo
kumjulisha kwa Simu Waziri Kawawa juu ya kinachoendelea. Mzee Ameen anawataja
askari wengine wa cheo cha juu waliofanikiwa kutoroka kuwa ni Meja Maricadi
pamoja na Mkuu mwengine mmoja ambaye amemsahau jina ambaye alijificha kwenye mapori
ya Kunduchi.
KASHMIRI UGHAIBUNI, HUZUNI YA KUKUMBUKA NYUMBANI.
Akiwa amefungiwa katika Mahabusu ya Jeshi katika kambi ya Colito, Mzee Kashmiri
anakumbuka sana kumuona Waziri Kambona akifanya
juhudi mbalimbali za kupoza na kutuliza maasi yale, Kama
moja ya matakwa ya Askari wale waasi ilimbidi Kambona akubali kuwasafirisha
mpaka Nairobi Viongozi wote wa Jeshi ambao walitiwa ndani (akiwemo Kashmiri) na
wale walioasi bila kipingamizi ambapo baadaye walisafirishwa kwenda Uingereza.
Anakumbuka vyema wakati akiwa ndani ya Gari wakitaka kusafirishwa namna mwenzie
Nyirenda alivyoulizwa "Wewe Mswahili nawe unakwenda wapi?", jambo
ambalo lilimhuzunisha sana
yeye kwa kuona ameachwa kwa kuwa yeye hakuwa Mswahili kama Nyirenda kwa
kudhaniwa naye ni mzungu tu kwa sababu ya rangi yake.
Maasi yale baadaye yalizimwa kwa msaada mkubwa wa Majeshi ya Kikoloni ya
Kiingereza na baadaye Kikosi cha Ulinzi cha Jeshi la Nigeria chini ya Generali Ochukwu
kilikuja kuchukua nafasi ya Jeshi la Uingereza, wakati huo Kashmiri alikuwa
tayari yuko Uingereza ambapo aliishi kwa muda wa miezi minne ya Upweke na
kutokupata mawasiliano yoyote na Serikali ya Taifa lake. Waingereza walijaribu
kumpa Ajira Mzee Kashmiri lakini aliwakatalia na kuwaambia kuwa yeye ni
Mwanajeshi wa Tanganyika
na hivyo hawezi kufanya kazi nyengine yoyote.
Mwezi April mwaka huo (1964) alipata simu ya maandishi (Telefax) kutoka kwa
Waziri Mkuu wa Tanganyika,
Mzee Rashid Mfaume Kawawa ikimtaka arudi nyumbani jambo ambalo lilimpa faraja
kubwa sana.
Kabla ya Maasi yale ya Jeshi alikuwa ameomba ruhusa Jeshini ya kwenda kusoma
Kozi Fupi ya Utawala wa Jeshi hivyo aliomba kutumia muda ule ambao yuko kule
Uingereza kusoma kozi hiyo ambayo aliimaliza Mwezi Julai mwaka huo huo kisha
akarudi nyumbani ambapo wakati huo haikuwa Tanganyika
tena bali Tanzania.
JWTZ, FAHARI YA WATANZANIA.
Mara baada kurudi Nchini Mzee Ameen Kashmiri alipewa Cheo cha Ukuu wa Utawala
na Uhandisi ambapo alifanya kazi nzito na ya kizalendo ya kujenga Jeshi Imara
la Wananchi wa Tanzania
kwa muda wa miaka minane.
Ilipofika Mwaka 1974 Mzee Kashmiri alikuwa amemaliza kazi yake ya kujenga Jeshi
lenye Askari Imara na wakakamavu zaidi ya 30,000 kutoka kati ya wale 400
waliobakishwa mara baada ya kuvunjwa kwa Tanganyika Rifles, ambapo anaelezea
namna ambavyo waliweza kusajili askari zaidi ya 2,000 kwa kila mwaka mpaka
kufikia kiwango hicho, ambapo alichangia kulijenga Jeshi hilo kuwa imara, lenye
nidhamu na lililo madhubuti zaidi katika Ukanda wote wa Afrika Mashariki.
MTUMISHI WA UMMA ASIYECHOKA.
Mwezi Januari mwaka 1974 Mzee Kashmiri alistaafu kwa heshima zote kutoka
Jeshini na kuwaachia nafasi vijana wapya ambao alishiriki kuwaunda washike
nafasi yake ili kuliendeleza na kuliimarisha zaidi Jeshi kutoka pale yeye
alipoishia.
Kama vile walivyo wazalendo wengine wote kustaafu hakuna maana kuwa hawezi tena
kulitumika Taifa lake, alirudi tena kwenye utumishi wa umma mara baada ya
kuombwa na Rais Nyerere kuwa Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Sukari (SUDECO),
kazi ambayo aliifanya kwa muda wa Miezi Miwili mpaka alipoondoka kwenye Ukuu
huo mwaka 1976 ambapo alirudi tena Jeshini wakati wa Vita vya Kagera.
RAFIKI WA KWELI NA MZALENDO
ANAYELIPENDA TAIFA
LAKE.
Mzee Ameen Kashmiri yu hai, japo siku hizi amekuwa mtu mzima sana na akijishughulisha zaidi na shughuli
zake binafsi katika sekta ya uchimbaji wa madini pamoja na kuwa karibu na
Familia yake.
Wakati wa Kilele cha Sherehe za Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Uwanja wa Uhuru
jijini Dar es salaam
mwaka 2011 Mzee Kashmiri alikuwa mmoja wa wahudhuriaji uwanjani hapo. Rais
Jakaya Mrisho Kikwete alipata nafasi ya kuzungumza naye na alimpongeza na
kummwagia sifa kwa kuwa mmoja wa mashujaa wachache wa Uhuru walio hai na
kuvutiwa naye kwa kulipenda Taifa lake
siku zote.
Wakati wa Maadhimisho ya Miaka Hamsini (50) ya Uhuru wa Tanzania Bara
(Tanganyika) Familia ya Marehemu Brigedia Alex Gwebe Nyirenda (ambayo Mzee
Kashmiri ndiye Baba Mlezi wa Familia hiyo) iliandaa tukio lililoitwa GWEMBE
NYIRENDA MEMORIAL KILIMANJARO EXPEDITION ambalo limepangwa kufanyika kila
Mwaka, tukio hilo likihusisha Upandaji wa Kuchochea Utalii na kuutangaza Mlima
wa Kilimanjaro kwa kukumbuka Tukio la Kuupandisha Mwenge wa Uhuru Mlimani hapo
lililofanywa na Nyirenda.
Mzee Ameen Kashmiri, Kaka na Dada Alex Foti Gwebe Nyirenda na Tima Gwebe
Nyirenda (WATOTO WA MZEE NYIRENDA), Mobeen Kashmiri (MTOTO WA MZEE KASHMIRI)
waliwaongoza ndugu jamaa na marafiki katika tukio hilo adhimu la kumkumbuka
rafikiye Nyirenda.
Mzee Kasmiri ni mtu mwenye Utu, Upendo na kujali kulikopita mipaka, miaka yote
amekuwa baba na mlezi mwema wa watoto hao wa Rafikiye wa kweli Nyirenda, kiasi
amewafariji na kuwafanya wajihisi kama vile baba yao yu hai bado. Yote hayo yakionyesha
sura halisi ya wema na umashuhuri wa Mzee wetu Ameen Kashmiri.
Chanzo:
ukurasa wa facebook ‘watanzania mashuhuri’