Mkuu wa harakati za kudumisha amani
wa Umoja wa mataifa Herve Ladsous ameliambia baraza la usalama la Umoja huo
kwamba waasi wameidhinisha kile anachokiita kuwa ni utawala wa kimabavu Mashariki
mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Bwana Ladsous amesema waasi wa M23
wanadhibiti idadi kubwa ya maeneo ya Mashariki mwa Congo na wanawatoza kodi
wananchi .
Umoja wa Mataifa unaishutumu Rwanda
kuwaunga mkono waasi wa M23. Wakati huo huo Maafisa wa Congo wanataka Rwanda
iwekewe vikwazo biashara ya madini .
Waziri wa Madini wa Congo,
ameziandikia nchi za Marekani na Uingereza akizitolea wito kampuni katika nchi
hizo ziache kununua madini kutoka Rwanda, ambayo mengi anasema yanachimbwa
katika ardhi ya Congo.
Zaidi ya watu 200,000 wameachwa bila
makao kufuatia mapigano Mashariki mwa nchi.
Mkutano wa maafisa wa ngazi ya juu
watakaojadili mzozo huo unatarajiwa kufanyika katika baraza la usalama la Umoja
wa mataifa mjini New York wiki ijayo.
"waasi wa M23 wako katika pembe
moja ya mkoa wa Kivu Mashariki ambao unapakana na Rwanda na Uganda'' alisema
bwana Ladsous wakati akiwahutubia waandishi wa habari mjini New York.
"ni kama ambao wanatawala kwani
wanawatoza kodi wenyeji wa mkoa huo , jambo hili halikubaliki hata kidogo''
aliongeza bwana Ladsous.
Wakati huohuo, maafisa wa utawala
nchini DRC wanataka vikwazo kuwekewa biashara ya madini yanayotoka nchini
Rwanda.
Wadadisi wanasema kuwa madini mengi
yanayotoka nchini Rwanda huenda yalitoka nchini DRC na kuchimbwa na makundi ya
waasi walio na uhusiano na Rwanda.
"namna tunavyoweza kukomesha
kabisa mzozo huu ni Rwanda kuwekewa vikwazo vya kibiashara kwa madini
yanayotoka nchini humo hadi tutakapoweza kupata suluhu la kudumu kwa mzozo
katika mikoa ya Kaskazini na Kusini ma Kivu.'' alisema waziri wa madini wa DRC
Martin Kabwelulu. .
Chanzo: BBC Swahili.
No comments:
Post a Comment