Friday, September 21, 2012

Binti mdogo wa miaka 19 awa mbunge nchini Uganda...




Msichana mdogo wa miaka kumi na tisa (19) nchini Uganda amekuwa mbunge wa kwanza mdogo katika historia ya nchi hiyo baada yua kushinda kiti hicho katika uchaguzi mdogo uliofanyika mapema mwezi huu.



Proscovia Alengton (19), amekuwa mbunge wa jimbo la Usuk, ameshika nafasi ya marehemu baba yake Michael Oromait ambae alikuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia chama cha NRM cha Rais Yoweri Museveni.


Proscovia aliingia madarakani kwa kishindo kupitia tiketi ya NRM baada ya kupata kura 11,059 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Charles Ojok Olweny wa chama cha IND aliepata kura 5,329.


Binti huyo wakati akiapishwa bungeni mjini Kampala jana mbele ya Spika Bibi Rebecca Kadaga, alishangiliwa kwa nguvu na wabunge wanawake na kuonekana ni mkombozi wa vijana wa nchi hiyo hasa ikizingatiwa Bunge la Uganda ni miongoni mwa mabunge yenye idadi kubwa ya wanawake katika mabunge ya Afrika ambapo linafikia asilimia 35, Mozambique 39.2 na Tanzania 36 wakati nchi ya kwanza ya Kiafrika yenye wabunge wengi wanawake ni Afrika Kusini yenye asilimia 42.  





Hata hivyo yapo malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali nchini Uganda wanaosema binti huyo atashindwa kuzungumza katika bunge hilo hasa ikizingatiwa elimu yake ni ndogo sambamba na umri kwani wabunge wengi huzungumza kwa jazba na mabishano makubwa.

Aidha wapo waliosema anaweza kuharibiwa na wala rushwa kwa kuonyeshwa mapesa mengi hivyo nae kuwa miongoni mwa watu watakaoingia katika orodha hiyo ya aibu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana binti huyo alisema haogopi kitu chochote na atahakikisha anatimiza ndoto za marehemu baba yake na kuwapa wananchi wake kile wanachostahili.

HAFIDH KIDO
KAMPALA, UGANDA
+256790836878/ +255752593894
21/09/2012
kidojembe@gmail.com

No comments:

Post a Comment