Wednesday, September 19, 2012
Tarehe
15 Septemba 2012 nilifanya mkutano wa hadhara Jimboni Ubungo kwenye kata ya
Makuburi ambapo pamoja na maswali mengine niliulizwa ni lini ujenzi wa Barabara
kwa kiwango cha lami kutoka Maziwa mpaka External ukiambatana na ujenzi wa
daraja katika barabara husika utaanza.
Pamoja
na kueleza hatua iliyofikiwa mpaka sasa nilitoa mwito wananchi wote ambayo
makazi yao yamewekewa alama ya "X" ikiwa si wavamizi wa barabara wawasilishe kwa Manispaa
ya Kinondoni maelezo na vielelezo vyao kwa kuzingatia Wakala wa Barabara Mkoa
wa Dar es es salaam (TANROADS) wao wana bajeti ya ujenzi pekee na madai ya
fidia kwa wenye uhalali yako chini ya Manispaa ya Kinondoni; tayari 17 Septemba
2012 baadhi ya wananchi wamewasilisha nyaraka zao.
Ikumbukwe
pia kuwa kwa kutambua umuhimu wa suala hili nilichukua hatua mbalimbali za
kibunge kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2011 ili barabara husika iweze kupandishwa
hadhi na kujengwa kwa kiwango cha lami kwa haraka zaidi kwenye mwaka wa fedha
2011/2012 kuliko ilivyopangwa awali.
Niliziandikia
mamlaka husika hususan Wizara ya Ujenzi na TANROADS kuzingatia barabara tajwa
katika bajeti kwa lengo la kuchangia katika kupunguza msongamano, Wizara ya Ujenzi
awali ilisema serikali kuu haiwezi kushughulikia barabara hiyo kwa kuwa iko
chini ya Manispaa ya Kinondoni. Lakini, nikaendelea kuchukua hatua zaidi kwa
njia za kibunge na za uwakilishi wa wananchi na hatimaye TANROADS ikaingiza
barabara hiyo katika vipaumbele vyake na kutenga fedha za ujenzi wa kiwango cha
lami kiasi cha shilingi bilioni 1.2.
Aidha,
pamoja na kiwango hicho cha fedha kilichotengwa na TANROADS, tarehe 5 Machi
2012 Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam alieleza kuwa amewasilisha maombi mengine kupitia
Mfuko wa Barabara (Road Fund) kwa ajili ya ujenzi wa daraja kubwa zaidi katika barabara hiyo
kwenye eneo la Ubungo Kisiwani/External suala ambalo pia kwa nyakati mbalimbali
nilihoji utekelezaji wake.
Izingatiwe
kwamba tarehe 21 Machi 2012 niliunganisha wananchi kuchangia hatua za dharura
za kufanya matengenezo ili kupunguza kero lakini nikasisitza kuwa suluhisho
muhimu zaidi ni kupanua daraja la External katika Eneo la Ubungo Kisiwani ili
kupunguza msongamano wa magari na kujenga barabara husika kwa kiwango cha lami
hatua ambayo sasa inaelekea kuchukuliwa kwa haraka.
John
Mnyika (Mb)
18 Septemba, 2012
No comments:
Post a Comment