Thursday, September 27, 2012

Uchungu wangu kwa watoto wa mitaani bado ipo palepale kila ninapokwenda Duniani.




Hawa watoto wapo mpaka wa Busia, Kenya na Uganda. Wanakaa hapo kuanzia asubuhi mpaka usiku kazi yao kubwa ni kuwaomba wasafiri wanaokwenda Kenya ama Uganda. Wengine wanaiba ama kuwalaghai wasafiri hasa wanawake nyakati za usiku.

Kwa maana unapofika mpakani ni lazima ushuke kwenye gari ukaguliwe na kugongewa muhuri katika pasi ya kusafiria 'visa', hivyo wanatumia mwanya huo kuwalaghai abiria wageni kwa kujidai wanawaomba lakini wakiona kitu kimekaa vibaya wanapora na kukimbia.

Katika kila mipaka ya nchi kuna eneo ambalo halimilikiwi na nchi yoyote katika nchi mbili zilizopakana, wazungu wanaita 'no man's land' Hivyo eneo hilo halikai askari kwa maana halina mtu. Wengi hutumia mwanya huo kukaa katika eneo hilo na kufanya uhalifu.

Wapo watoto ambao nilianza kuwaona tangu mwaka 2008 mpaka sasa wamekuwa wakubwa, wanakunywa ulevi na kuvuta gundi. Wachafu na wakorofi sana.

Lazima serikali za nchi mbili hizi zikae pamoja kujadili watoto hawa maana lazima watakuwa wanahusika katika moja ya nchi hizo mbili Kenya ama Uganda.

HAFIDH KIDO
DAR  ES SALAAM, TANZANIA
0713 593894/0752 593894
kidojembe@gmail.com
28/09/2012

No comments:

Post a Comment