Wednesday, September 19, 2012

Tamko la Serikali juu ya vurugu katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Bububu Zanzibar...



Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema hakuna mtu aliyefariki kutokana na vurugu siku ya Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Bububu uliofanyika Jumapili iliyopita kama ililivyodaiwa. na gazeti moja linalotolewa kila wiki hapa nchini.

Kwa mujibu wa Taarifa kutoka Afisi ya Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar na kutiwa saini na waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed imeeleza hadi sasa hakuna taarifa yoyote ya kifo kilicho sababbishwa na vurugu hilo iliyoripotiwa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa jeshi la Polisi lilipokea taarifa ya kujeruhiwa watu kutokana na vurugu za baadhi ya vitkundi vya wananchi vilivyojipanga kuwazuia wananchi wengine kwa makusudi kushiriki katika zoezi la kupiga kura.
Kuhusu tuhuma zilizo tolewa dhidi ya Makamo wa Pili wa Rais katika zoezi la upigaji kura taarifa hiyo ilieleza kuwa maelezo hayo siyo ya kweli na kwamba zinalenga kumchafulia jina Kiongozi huyo wa ngazi za juu

Kufuatia tuhuma hizo Serikali imemtaka Mharir wa Gazeti la FAHAMU kuthibitisha kwa maandishi tuhuma walizoandika dhidi ya Mheshimiwa Makamo wa Pili wa Rais au kumuomba radhi kwa maandishi kupitia Gazeti lake la FAHAMU katika kipindi kisichozidi siku saba(7) kuanzia tarehe ya taarifa hii. Vyenginevyo Serikali itachukuwa hatua zinazofaa dhidi ya wahisika wote.

Aidha taarifa hiyo imeeleza kusikitishwa kwake na taarifa zilizotolewa na kiongozi mmoja wa Ngazi za juu wa CUF kupitia gazeti hilo kwa kumtaja Makamo wa Pili wa Rais kuwa kiongozi wa juu wa serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar aliyejitosa kuharibu matokeo ya kura kwa kuingia katika baadhi ya vituo kama kiongozi wa Wawananchi.

Tuhuma hizo si za kweli na zisingepaswa kutolewa na Kiongozi wa juu wa chama cha siasa kwani kiongozi huyo anaelewa fika kwamba tuhuma hizo zinachafua jina la kiongozi huyo na kuhatarisha Umoja wa Taifa Letu.

          IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR 19/09/2012.

No comments:

Post a Comment