Thursday, September 20, 2012
Wanafunzi Kenya waandamana kuishinikiza Serikali iwaongezee mshahara wahadhiri wao...
Wanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi Kenya, wameandamana wakiitaka serikali kutatua mzozo wa mishahara wa wahadhiri wa vyuo vikuu nchini. Hatua ya wahadhiri hao kugoma kwa wiki tatu imezitatiza shughuli nyingi ikiwa ni pamoja na kuwazuia wanafunzi hao kufanya mitihani yao. Polisi hata hivyo waliwatawanya wanafunzi hao waliokusanyika mjini kwa kutumia gesi za kutoa machozi. Mapema leo serikali iliahidi kuwalipa wahadhiri hao shilingi za Kenya bilioni 7.8 ili waweze kurejea kazini Jumatatu wiki ijayo. Hata hivyo malipo hayo yataweza kutolewa kwa awamu mbili kuazia Januari mwaka ujao. Waziri wa elimu ya juu Margaret Kamar alitoa tangazo hilo akiwataka wahadhiri hao kurejea kazini Jumatatu. Hata hivtyo wahadhiri hao wamesema hilo bado ni pendekezo tu la serikali na itawabidi mwanzo kulidurusu kabla ya kufanya uamuzi wowote. Aidha wamesema wangali wanashauriana kabla ya kuamua lini watakapositisha mgomo wao. Wahadhiri waligoma wakishinikiza mikakati mipya ambayo itawawezesha kuongezwa mishahara maradufu na pia kuongeza marupurupu yao. Kwingineko, vuguvugu moja la wazazi limemutaka rais wa nchi hiyo Mwai Kibaki kuwafuta kazi waziri wa leba John Munyes na mwanasheria mkuu Githu Muigai kwa migomo ya wafanyakazi ambayo imekumba nchi hiyo. Chama cha kitaifa cha wazazi, kimemtuhumu waziri wa leba kwa kupuuza migomo ya waalimu na wahadhiri wa vyuo vikuu ambayo imekuwa ikiendelea sasa kwa zaidi ya wiki mbili. Chama hicho kimeelezea kughadhabishwa na hatua ya serikali kuendelea kuchezea maisha ya watoto wao. Chama hicho kinapanga kufanya maandamano makubwa wiki ijayo yatakayowahusisha wanafunzi na wazazi kuonyesha kero lao kuhusiana na serikali kujikokota kusuluhisha migomo ya walimu. Chanzo: BBC Swahili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment