Saturday, September 15, 2012

LIGI KUU BARA KUANZA KUTIMUA VUMBI LEO


 
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara 2012/2013 inaanza kutimua vumbi leo (Septemba 15,2012) ambapo timu zote 14 zitakuwa kwenye viwanja saba tofauti.

Mabingwa watetezi Simba wataikaribisha African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mjini Morogoro, Polisi Dodoma watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri wakati jijini Tanga, Mgambo JKT ambayo imepanda daraja msimu huu itaumana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Tanzania Prisons ambayo nayo imerejea VPL msimu huu itaialika Yanga kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya. JKT Ruvu na Ruvu Shooting zitapambana kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam huku Azam ikiwatembelea Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Katiba.

Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Toto Africans dhidi ya Oljoro JKT. Mechi zote zitaanza saa 10.30 jioni.

Viingilio katika mechi ya Simba na African Lyon vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani na bluu, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 viti vya VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000. Viingilio kwa mechi nyingine vitakuwa sh. 3,000 na sh. 10,000.

                                   Boniface Wambura
                                        Ofisa Habari
                   Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania

No comments:

Post a Comment