Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA mpya wa Yanga,
Ernstus ‘Ernie’ Wilhelmus Johannes Brandts, beki wa zamani wa kimataifa wa
Uholanzi na klabu ya PSV Eindhoven ya Holanzi, amewasili usiku huu (saa 3:45)
katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na ndege ya KLM
tayari kusaini mkataba na kuanza kazi katika klabu hiyo.
Brandts amepokewa na
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako na viongozi wengine, Abdallah Ahmad
Bin Kleb, Seif Ahmad ‘Magari’ na Majjid Suleiman na amesema anaijua Yanga ni
timu nzuri, kubwa hana shaka ataiwezesha kufanya vizuri katika medani ya soka
Afrika.
Yanga, imetimiza
malengo yake ya kuwa kocha mpya, kabla ya kucheza na wapinzani wao wa jadi, Simba SC ,
Oktoba 3, mwaka huu baada ya kumfukuza Mbelgiji, Tom Saintfiet, kutokana na
kuwasili makubaliano na Brandts, ambaye ataanza kazi mara moja kesho.
Mholanzi huyo
aliyefukuzwa APR ya Rwanda
baada ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Agosti mwaka
huu amepewa ukocha wa Yanga, baada ya Mbrazil Marcio Maximo kukataa nafasi hiyo
kwa mara ya pili.
Mtaalamu huyo,
alizaliwa Februari 3, mwaka 1956 mjini Nieuw-Dijk, Gelderland, mbali na PSV
Eindhoven, alichezea pia Roda JC Kerkrade, MVV Maastricht na De Graafschap.
Brandts aliichezea
mechi 28 timu ya taifa ya Uholanzi na kuifungia mabao matano na pia alicheza
Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978.
Katika fainali hizo,
Raundi ya pili kwenye mechi na Italia, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee
aliyezifungia mabao timu zote katika mechi moja kwenye fainali za Kombe la
Dunia.
Alianza kujifunga
dakika ya 18, kisha akaisawazishia Uholanzi dakika ya 50 katika mechi ambayo,
mchezaji mwenzake Arie Haan baadaye aliifungia timu yake bao la ushindi na
kutoka kifua mbele kwa mabao 2–1.
Alipostaafu soka akawa
kocha na katikati ya msimu wa 2007–2008, Brandts aliambiwa hataongezewa mkataba
NAC-Breda, licha ya matokeo mazuri ya kushika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu
Uholanzi (Eredivisie), ingawa uamuzi huo haukuwafurahisha mashabiki wa timu
hiyo na nafasi yake akapewa Robert Maaskant kuanzia msimu wa 2008–2009.
Akateuliwa kuwa Kocha
wa Rah Ahan mwaka 2009, kabla ya kufukuzwa Desemba 2009 na kuibukia APR ya Rwanda mwaka
2010, ambako ‘riziki’ yake imeisha miezi miwili iliyopita na sasa amepata
maisha mapya Yanga.
Akiwa APR, Brandts
alifungwa mechi zote mbili na Yanga iliyokuwa ikifundishwa na Mbelgiji Tom
Saintfiet katika Kombe la Kagame, moja ya makundi 2-0 na nyingine ya Nusu
Fainali 1-0. Yanga iliibuka bingwa, ikiifunga Azam FC 2-0 kwenye fainali.
Brandts atakutana na
wachezaji wake wa zamani wawili Yanga, beki Mbuyu Twite anayeanza msimu wa
kwanza katika klabu hiyo na kiungo Haruna Niyonzima anayeingia katika msimu wa
pili, ambao alifanya nao kazi APR.
Habari
na picha kwa hisani ya Bin Zubeir bongostaz.blogspot
No comments:
Post a Comment