Thursday,
September 20, 2012
Pamoja
na manispaa ya Kinondoni kutoa shilingi milioni moja na nusu tarehe 14 Septemba
2012 kwa ajili ya kufunga mita na kuanza kusukuma maji ya mradi wa Goba, tarehe
19 Septemba 2012 wakati wa Mkutano wa Baraza la Madiwani nimemtaka Mkurugenzi
wa Manispaa ya Kinondoni kuwawajibisha watendaji waliozembea na kusababisha
matatizo hayo kudumu kwa muda mrefu.
Izingatiwe
kuwa kiasi hicho ni nyongeza baada ya awali kutolewa milioni tatu na Mfuko wa
Maendeleo ya Jimbo la Ubungo (CDCF) kwa ajili ya kuwezesha huduma ya maji
kupitia mradi huo kurejea.
Ikumbukwe
kuwa mwezi Agosti 2011 maji yalikatwa kwenye kata ya Goba kutokana na DAWASCO kuidai
kamati ya mradi wa maji shilingi milioni 18 na katika kufuatilia deni hilo
nilipata taarifa za Kamati ya Maji kuwasilisha malalamiko DAWASCO ya
kutokukubaliana na kiwango hicho cha deni na pia kwa Manispaa ya Kinondoni
kuhusu matatizo ya kiutendaji na kifedha katika mradi huo wa maji ikiwemo ya
upotevu wa fedha.
Tarehe
5 Septemba 2011 niliwaunganisha wananchi kwa pamoja tukaandamana kwenda ofisi
ya DAWASCO makao makuu ambapo tulikutana na mtendaji mkuu wa kampuni husika na
kufanya mazungumzo ambayo yalisaidia baadhi ya hatua za msingi kuchukuliwa
ikiwemo DAWASCO kurejesha huduma ya maji katika bomba kuu baada ya sehemu ya
deni kulipwa na makubaliano kufikiwa kuhusu malipo ya kiwango kilichobaki.
Pia
tarehe 24 Oktoba 2011 niliandika barua kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni
kutoa mwito wa hatua za dharura kuchukuliwa ili kuhakikisha uhakiki unafanyika
wakati huo huo wananchi wengine wanaendelea kupata huduma ya maji; lakini
udhaifu wa kiutendaji umefanya hatua ziwe za kusuasua.
Hata
hivyo, pamoja na huduma ya maji kurejeshwa katika bomba kuu haikuweza
kusambazwa kwenye mabomba ya wananchi pamoja na vioski vya kutolea huduma kwa
sababu ya udhaifu wa utendaji katika ngazi ya kata na katika kamati ya maji
hivyo tarehe 26 Januari 2012 niliwaunganisha wananchi kufika Manispaa ya
Kinondoni kwa ajili ya hatua za haraka za Mkurugenzi wa Manispaa.
Kufuatia
hatua hiyo Mkurugenzi wa Manispaa Fortunatus Fwema alifanya ziara katika kata
ya Goba tarehe 31 Januari 2012 na kuagiza kwamba ndani ya tano maji yatoke
katika kata hiyo na kuagiza Mhandisi wa maji na timu yake waweke kambi katika
kata ya Goba mpaka maji yatoke kwa gharama za halmashauri ya Manispaa ya
Kinondoni.
Hata
hivyo, muda huo ulimalizika bila maji kupatikana na kikosi kazi kilikabidhiwa
jukumu tarehe 28 Februari 2012 kushughulikia kile kilichoelezwa kuwa ni kuanza
uchunguzi wa Bomba la Maji kuanzia Tanki Bovu hadi kwenye tanki la Matosa ili
kubaini wizi, upotevu wa maji na uharibifu wa miundombinu.
Katika
kipindi cha kati ya Februari mpaka Agosti 2012 nimefuatilia Manispaa kwa njia
mbalimbali na wakati wote maelezo yamekuwa kazi hiyo inachukua muda mrefu kwa
sababu ya urekebishaji wa miundombinu ambapo Manispaa ya Kinondoni ilikubali
kutoa mita 15 pamoja na stendi za bomba mpya kwa ajili ya kufunga katika bomba
kubwa kwenye njia zinazoelekea kwa wananchi ili kudhibiti wizi na upotevu wa
maji pamoja na kufanya marekebisho katika mabomba na gate-valves
zilizohujumiwa.
Ikumbukwe
kuwa matatizo ya maji kata ya Goba yanafahamika kwa mamlaka zote husika kuanzia
Wizara ya Maji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Manispaa ya Kinondoni na vyombo vya dola
kuanzia mwaka 2007 mpaka mwaka 2012 lakini hatua kamili hazijachukuliwa kwa
wakati.
Wananchi
wa Goba wamepoteza uvumilivu kwa kuwa hatua hazichukuliwi kwa haraka na
kutokana na hali hiyo mbunge kama mwakilishi wa wananchi nimeumua kuungana nao
katika kutaka uwajibikaji wa watendaji wote waliozembea na kusababisha matatizo
hayo kudumu kwa muda mrefu.
Nimefikia
hatua hiyo kwa sababu njia zote za kawaida kupitia vikao na mawasiliano ya
kiofisi zinaelekea kukwamishwa na uzembe, hujuma na urasimu na udhaifu wa
kiutendaji katika ngazi mbalimbali.
Katika
kushughulikia masuala la maji kwenye kata ya Goba, narudia kusisitiza hatua
zifuatazo kuendelea kuchukuliwa kwa haraka na mamlaka zifuatazo:
Mosi;
Mamlaka za Manispaa ya Kinondoni zikiongozwa na Meya na Mkurugenzi zinapaswa
kufuatilia kwa haraka kuhakikisha maji yanarejeshwa Goba. Hatua hii iende
sambamba na kupanua wigo wa maji Goba kwa kutekeleza kwa haraka upatikanaji wa
maji kutoka pia mradi wa maji toka Madale Kisauke.
Manispaa
izingatie matatizo yaliyopo kwenye miradi ya maji inayoendeshwa na manispaa
pamoja na kamati za wananchi au vyama vya watumia maji katika maeneo
mbalimbali. Hivyo, pamoja na kuchukua hatua kuhusu mradi wa maji wa Goba,
Manispaa ichukue hatua juu ya miradi iliyokwamba ukiwemo wa Mbezi Msumi na
Makabe. Pia, Manispaa ya Kinondoni inapaswa kufanya mabadiliko kwenye idara ya
maji kwa kuwa ina udhaifu mkubwa wa kiutendaji.
Pili;
Wizara ya Maji, Mamlaka ya maji safi na maji taka (DAWASA) na Kampuni ya maji
safi na maji taka (DAWASCO) zizingatie kwamba maeneo ya pembezoni ya Dar es
salaam ambayo awali yalikuwa vijiji sasa ni mitaa yenye wakazi wengi. Hivyo,
maeneo kama kata ya Goba na mengine ya pembezoni yanapaswa kuunganishwa moja
kwa moja na mtandao wa maji chini ya mamlaka husika kwa mujibu wa sheria
iliyounda DAWASA badala ya mfumo uliopo ambalo haulingani na mahitaji.
Tatu;
vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kushughulikia vyanzo vya migogoro badala
ya kusubiri mpaka matatizo yanapoibuka kwa kushughulikia kwa wakati malalamiko
yanayotolewa. Mathalani, Jeshi la Polisi (Ofisi ya DCI) na TAKUKURU wanapaswa
kutoa kauli kuhusu hatua zilizochukuliwa juu ya tuhuma za ufisadi na ukiukwaji
wa sheria katika mradi wa maji Goba ambazo zimetolewa na wananchi kwa mamlaka
husika kuanzia mwa 2007.
Mamlaka
husika zizingatie kuwa tarehe 27 Februari 2011 na 6 Machi 2011 nilifanya mikutano
na wananchi katika kata ya Goba ambapo risala ya wananchi pamoja na ripoti ya
ukaguzi wa mradi wa mradi wa maji Goba ya mwaka 2007 zilizosomwa ambazo
zilieleza bayana matatizo yaliyokuwepo kwenye kamati ya maji pamoja na mradi
kwa ujumla ikiwemo yaliyohusu upotevu wa fedha ambayo vyombo vya dola
vilipatiwa taarifa lakini hatua hazikuchukuliwa kwa wakati.
Kwa
nyakati mbalimbali nimeziandikia barua rasmi mamlaka husika kuhusu masuala haya
na mengine na kutokana na kutochukua hatua kwa wakati mwezi Agosti 2012
kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge nilikutana na Waziri Mkuu Mizengo
Pinda na kumweleza haja ya kuingilia kati ili ufumbuzi upatikane mapema.
John
Mnyika (Mb)
19/09/2012
No comments:
Post a Comment