Wednesday, September 19, 2012

Kuna wa kulaumiwa kwa maisha duni ya Wazanzibari?

Barazani kwa Ahmed Rajab

Ahmed Rajab
Toleo la 259
19 Sep 2012
IMEKWISHAPITA miaka miwili sasa tangu Zanzibar iwe na Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kwa sasa Wazanzibari na wasio Wazanzibari wanakubali kwamba hii fikra ya kuwa na serikali ya ubia ndiyo dawa mujarab ya kuondosha chokochoko na mizozano ya kisiasa iliyojitokeza mwanzo mnamo mwaka 1957 pale wakoloni Wakiingereza walipoanzisha mfumo wa siasa za vyama vingi Visiwani.
Wapo bado wakorofi wenye kujaribu kuirejesha Zanzibar kule ilikotoka na isikotaka kurejea. Walijitokeza Jumapili iliyopita wakati wa uchaguzi mdogo wa Bububu, Unguja. Matokeo yalikipa chama cha CCM ushindi kwa wingi mdogo wa kura.
Ingawa kweli ushindi ni ushindi lakini kuna shutuma kuwa huu ni ushindi ulioshinikizwa kwa wizi wa kura. Ikiwa shutuma hizo ni za kweli basi hilo ni jambo la kuvunja moyo ingawa inatia moyo sana kuona kwamba hapajazuka fujo baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.
Swali linaloibuka ni iwapo yaliyojiri Bububu ni matokeo ya njama za watu wachache au ni tabia ambayo CCM haiwezi tena kutengana nayo? Jibu naliwe liwavyo binafsi naamini kwamba mambo yanaweza kuwa tofauti katika uchaguzi mkuu ujao wa 2015.
Historia imetuonyesha jinsi mifarakano ya kivyama ilivyozusha uhasama mkubwa wa kisiasa miongoni mwa Wazanzibari na kuwafanya wafike hadi hata ya kuchinjana kwa sababu za kisiasa. Ilifika wakati walimwengu wakifikiri ya kuwa Wazanzibari hawawezi tena kuwa kitu kimoja na kwamba wataendelea kuzozana na kupigana mpaka akhiri dunia.
Mungu bariki Wazanzibari waliamka na wakatafakari kuhusu hali waliyojikuta nayo na watayoiachia vizazi vyao vijavyo. Haikuwa hali ya kuridhisha hata chembe. Bahati nzuri kuna baadhi yao waliojiamini na walioingiwa na shauku ya kuyatanzua wenyewe matatizo ya nchi yao bila ya kuingiliwa na watu wa nje. Waliamua kwamba matatizo ya Kizanzibari lazima yapatiwe ufumbuzi wa Kizanzibari, ufumbuzi utaoleta suluhu na kuwaunganisha tena Wazanzibari.
Hawakusita hapo tu bali pia walitaka Wazanzibari wawe na uwezo wa kuuamua mustakbali wao kwa kupitia mchakato ulio wa kidemokrasia na wa uwazi, mchakato ambao utawafanya wananchi waukubali ufumbuzi utaopatikana. Kwa kufanya hivyo walihakikisha kwamba ufumbuzi huo utakuwa wa halali na utahalalisha utawala wa kidemokrasia bila ya kundi moja la jamii kuhodhi peke yake madaraka ya utawala.
Hatari ya kundi moja la jamii kuhodhi madaraka peke yake ni kwamba walio katika kundi hilo na vizazi vyao hatimaye huwa watawala wa kudumu. Kwa hakika, baadhi ya familia hizo za kisiasa zilikuwa zimekwishaanza kuamini kwamba ni wao tu walio na haki ya kutawala daima dahari na hivyo kulikuwa na hatari ya kuanzishwa aina mpya ya usultani.
Majina yanayotajwa sasa ya wazalendo wa Kizanzibari waliojitolea kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya kisiasa ya nchi yao kutoka upande wa CCM ni Rais msataafu Amani Abeid Karume pamoja na Hassan Nassor Moyo na kutoka upande wa upinzani Katibu Mkuu wa chama cha CUF Maalim Seif Sharif Hamadi.
Wapo wengine pia waliochangia pakubwa katika kufanikisha juhudi za kupatikana suluhu baina ya vyama hivyo vikuu vya kisiasa Visiwani. Wenyewe wamejificha lakini pale historia ya kupatikana suluhu hiyo itapoandikwa kwa ukamilifu majina yao yataibuka na watatambulika kwa ujasiri wao wa kuziacha kando itikadi zao za kichama na kuiweka mbele nchi yao.
Walichofanikiwa kukifanya wote hao ni aina ya miujiza. Wote walikuwa wakunga wa kumzalisha mtoto mmoja: Maridhiano. Na hayo Maridhiano ndiyo yaliyowezesha kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Uundwaji wa serikali hiyo uliwafanya wengi wataraji mengi katika muda usio mwingi. Pengine wakitaraji miujiza mingine kutokea kwani kipindi hiki cha miaka miwili kisingeliweza bila ya miujiza kuyageuza mambo na kuwaridhisha wengi wa wananchi na wakazi wa Visiwani.
Maridhiano yalitanzua tatizo moja. Vilevile Maridhiano yaliimarisha ile iitwayo Ajenda ya Zanzibari inayoakisiwa ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na miongoni mwa wananchi. Na ingawa ni kweli kwamba bila ya Maridhiano pasingekuwako na umoja ndani ya serikali au hata miongoni mwa wananchi, ni wazi kwamba iko haja, tena kubwa, ya kuzitafutia ufumbuzi shida kubwa za kiuchumi na kijamii zinazowakabili wananchi wengi wa Zanzibar pamoja na zile za sekta za kimkakati kama vile ile ya elimu, ambayo ni muhimu sana kwa ufanisi wa mipango ya Wazanzibari kuhusu mustakbali wa nchi yao.
Kwa mujibu wa mfumo uliopo sasa wa kuundesha Muungano wa Zanzibar na Tanganyika, Zanzibar haina nguvu zinazohitajika kuyatanzua matatizo yote ya kimsingi yanayowakabili Wazanzibari.
Kwa sababu hiyo kuna ulazima kwamba pafanywe juhudi za pamoja kati ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na Serikali ya Muungano katika kuyatanzua matatizo hayo.
Kinachohitajika hasa ni kwa Serikali ya Muungano kutenda haki na kuipa nguvu Serikali ya Zanzibar ili iweze kuleta maendeleo bila ya kusubiri Katiba mpya au Mkataba wa Muungano. Nguvu hizo za kiutawala zitaiwezesha Serikali ya Zanzibar kuchukua hatua za dharura za kuirekebisha hali ya kiuchumi na kijamii inayozidi kudumaa.
Katika muktadha huu sioni sababu kwa mfano kwa nini Serikali ya Muugano haichukui hatua ya kuyaondosha kutoka orodha ya “Mambo ya Muungano” masuala yaliyo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii kama vile masuala ya mafuta na gesi asilia pamoja na elimu. Masuala kama ya mafuta na gesi asilia yanahitaji mkakati ulio makini na mipango yenye utaratibu mkubwa na hivyo utapita muda usio mdogo kabla ya Wazanzibari kunufaika kutokana na sekta hizo.
Ni muhimu pia kwamba Zanzibar ipewe nguvu za kiutawala kuleta mageuzi makuu yanayohitajika ili kuwasaidia Wazanzibari na watoto wao wapate elimu na mafunzo ya maana yatayowawezesha kuijenga tena nchi yao.
Ukweli haufichiki kwamba hadi sasa Serikali ya Umoja wa Kitaifa bado haikufanikiwa kuyakidhi mahitaji ya wananchi wake kwa kuwapatia huduma zilizo bora. Ukiichungua hali halisi ilivyo leo Zanzibar utaweza kudhani kana kwamba kwa muda wote huu serikali ya huko haikuwa na mipango yoyote ya mikakati ya kuziondosha shida zinazowakabili Wazanzibari.
Kadhalika inadhihirika wazi kwamba Wazanzibari walio ughaibuni na Jumuiya ya Kimataifa hawakupewa jukumu lolote la kusaidia kuyatanzua matatizo yaliyopo ingawa wameonyesha nia ya kusaidia.
Kuendelea kwa mchakato wa kulipatia taifa katiba mpya hakumaanishi kwamba serikali iahirishe shughuli zake za utawala au iusimamishe wajibu wake wa kuuhudumia umma hasa tukizingatia jinsi maisha yalivyo magumu hii leo Zanzibar.
Idadi kubwa ya vijana wa Kizanzibari hawana ajira na wengi wao kwa hakika hawana uweledi wa jambo lolote la maana na wanahitaji wapatiwe mafunzo ya fani mbalimbali na wapikwe wapikike ili Zanzibar iweze kujitosheleza katika upande wa wafanyakazi hata katika sekta kama ya utalii ambayo sasa ina wahudumu wengi sana wasio Wazanzibari.
Kusema kweli tunachokishuhudia hii leo Zanzibar ni kwamba Wazanzibari wenyewe wanatengwa na ajira kwa vile fursa nyingi za ajira zinachukuliwa na wageni. Waajiri wanapendelea kuwaajiri hao wageni kwa sababu wao ndio wenye elimu, ujuzi na uzoefu zaidi wa kazi kushinda wenyeji.
Kwa hivyo Serikali ya Umoja wa Kitaifa inawajibika kuchukua hatua za dharura za kuwapatia mafunzo vijana wa kiume na wa kike kwa kuunda taasisi za mafunzo zenye viwango vya kilimwengu ili kuwawezesha Wazanzibari washiriki katika soko la ajira la nchini kwao kwenyewe.
Jambo jingine linalohitajika ni kwa Wazanzibari wote kuiunga mkono serikali yao inapokuwa inatoa madai yaliyo ya halali kwa Serikali ya Muungano. Wakati wa kufanya hivyo umewadia sasa na pia wakati umefika kwa Serikali ya Muungano kushirikiana na Serikali ya Zanzibar kwa kulitumia jina jema ililo nalo Zanzibar ulimwenguni ili kuwapata wahisani wataoweza kuisaidia Zanzibar ikidhi mahitaji yake.
Na Zanzibar ina mahitaji mengi kwani shida zake za kiuchumi na za kijamii ni nyingi na shida hizo zitaweza tu kuondoshwa endapo patachukuliwa hatua za dharura za kuzikabili shida hizo.
Jambo moja li wazi. Juu ya shida zote hizo za kimaisha dalili zilizopo zinaonyesha kwamba Wazanzibari hawajavunjwa moyo bado na serikali yao ya ubia. Bado wangali wakitumai kwamba serikali yao itachukua hatua zinazostahiki zitazoiwezesha kuwahudumia ipasavyo wananchi wake na kuudhibiti ufisadi.
www.raiamwema.co.tz

No comments:

Post a Comment