Raia Mwema
Toleo la 258
12 Sep 2012
MWALIMU wangu wa nje ya darasa,
Profesa Issa Shivji, hugawa Watanzania katika madaraja matatu; walalaHoi,
walalaheri na walalahai akiwa na maana kwamba watu wenye kuishi kwenye dimbwi
la umasikini, watu wenye ahueni na matajiri. Katika mtandao wa kijamii (twitter)
wakati naandika makala hii, mdogo wangu Michael Dalali akaniongezea daraja
jipya ‘wakeshahoi’. Hawa wa mwisho nadhani ndio tunasema ‘masikini wa kutupwa’
kwa lugha ya mtaani. Sijapata fursa ya kumuuliza Michael ili afafanue hili
daraja jipya. Leo ninatafakari na wasomaji kuhusu madaraja mawili tu, walalahoi
(mafukara) na walalahai (matajiri).
Mwezi Juni, 2012 niliandika katika
lugha ya Kiingereza (The Bottom 30M, www.zittokabwe.com) kujibu
swali la kwa nini Watanzania ni masikini licha ya utajiri mkubwa uliopo nchini.
Katika makala hiyo ‘Mafukara 30M’ nilihitimisha kwamba Watanzania ni masikini
kwa sababu watawala wetu wameamua hivyo kwa kutunga na kutekeleza sera na
mikakati ambayo inanufaisha watu wachache katika tabaka la juu la maisha ambao
wengi wanaishi mijini na kuacha watu wengi wanaoishi vijijini wakiwa masikini
zaidi. Katika tafakuri ya leo nafafanua zaidi huu mtazamo. Watawala wetu
ninaamini wakiulizwa tena na wanahabari kwa nini Tanzania ni masikini
hawatajibu hawajui (Rais Kikwete na Waziri Mkuu Pinda wamenukuliwa zaidi ya
mara moja wakisema hawajui kwa nini nchi wanayoongoza ni masikini). Nimesema na
kuandika mara kadhaa sababu za umasikini kuongezeka nchini licha ya kwamba
uchumi unaonekana kukua kwa kasi.
Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa
wiki iliyopita amerudia tunayoyasema kila siku kwamba ukuaji wa uchumi Tanzania
haujapunguza umasikini. Tumekuwa tukisema kwamba mikakati ya kiuchumi
tunayotekeleza haimsaidii Mtanzania wa kawaida maana hatuoni tofauti ya maisha
yake. Serikali ikaendelea na inaendelea kutekeleza mikakati ile ile ikitegemea
kupata matokeo tofauti.
Dk. Mgimwa, Waziri wa Fedha,
anasema, “takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita uchumi
umekua kwa wastani wa asilimia saba lakini umasikini umepungua kwa asilimia 2.1
tu ambayo ni ndogo ikilinganishwa na asilimia ya ukuaji wa uchumi”. Akanukuliwa
akisema “umasikini umepungua kwa asilimia 2.1 kutoka asilimia 35.6 mwaka 2001
hadi kufikia asilimia 33.4 mwishoni mwa mwaka jana katika kundi la masikini,”.
Hakuna kauli mpya hata moja. Kinachosikitisha ni kwamba serikali imeendelea
kuona Mpango wa Kupunguza Umasikini na Kukuza Uchumi (MKUKUTA) ndio mkakati
pekee wa kuondoa umasikini nchini. Sera na mikakati ya serikali kuondoa
umasikini imeshindwa. Taarifa ya Shirika la SID ya mwaka 2012 imeonyesha kuwa
kati ya mwaka 2001 na 2011 Watanzania takribani milioni tano zaidi wameingia
katika dimbwi la umasikini. Kwa nini uchumi unakua kwa kasi kubwa lakini ukuaji
huu haupunguzi umasikini, unazalisha masikini zaidi? Taarifa za serikali pia
zinaonyesha kuwa ukuaji wa uchumi hautengenezi ajira kwa watu. Kwa nini hali
hii? Kama kawaida hatukosi majibu ya maswali haya. Tunayarudia majibu haya kila
wakati tunapopata nafasi ya kueleza. Kwamba sekta za uchumi zinazokua hazina
uhusiano wenye nguvu na wananchi wa kawaida – madini, utalii na mawasiliano.
Sekta yenye uhusiano mkubwa na wananchi – sekta ya kilimo - haikui kwa
kiwango kinachoweza kupunguza umasikini. Ili kupunguza umasikini Tanzania kwa
kiwango kikubwa, sekta ya kilimo inapaswa kukua kwa asilimia zaidi ya nane
angalau kwa miaka mitatu mfululizo na kuendelea kukua kwa wastani wa asilimia
sita kwa miaka 10.
Jibu lipo na limeshasemwa sana
lakini jawabu halisemwi. Labda tuulize tena. Kwa nini sasa sekta ya kilimo
haikui kwa kiwango kinachotakiwa ili kuondoa umasikini Tanzania? Jawabu langu
ni kwamba watawala hawataki. Watawala wetu wamechagua Watanzania wengi wabakie
mafukara. Umasikini wa Watanzania ni chaguo mahususi la watawala kwa kuamua
kutekeleza sera ambazo zinakuza kipato cha mwenye nacho na kufukarisha wananchi
wengi wa vijijini. Vile vile uamuzi wa watawala kushindwa kupambana na ufisadi
na ubadhirifu wa rasilimali za umma ni kitendo cha kumzubaisha katika ufukara
mwananchi wa vijijini ambaye anakoseshwa huduma za jamii na miundombinu ya
kumpa fursa ya kufaidika na shughuli zake za kiuchumi. Ufukara wa mamilioni ya
Watanzania ni matokeo ya chaguo la watawala kisera, kimkakati na kimatendo.
Ufukara ni tofauti na umasikini
ingawa tunatumia maneno haya tukiamini kuwa yana maana inayofanana. Wakati
umasikini (poverty) ni hali ya kukosa huduma za msingi kama elimu, afya,
chakula, maji safi na salama kunakotokana na kukosa kipato au kuwa na kipato
kidogo, ufukara (impoverishment) ni hali ya kukoseshwa huduma za msingi
za kibinadamu hata kama kuna juhudi za dhati za kufanya kazi kwa bidii
ili kupata uwezo wa kufikia huduma hizo. Umasikini unaweza kusababishwa na
masuala mbalimbali ikiwemo hali ya kuwa masikini tu (‘we are poor because we
are poor’) au jiografia na mengineyo. Ufukara unatokana na kufukarishwa.
Unatokana na uamuzi wa kisera katika taifa husika (au mataifa ya nje) ambayo
yananyonya juhudi za watu kupata maisha yenye kuwapa huduma zote za msingi kama
elimu, afya, maji na muhimu zaidi chakula cha uhakika. Mafukara wote ni
masikini, ila masikini wote sio mafukara. Nitafafanua.
Mwaka 1991 Watanzania masikini
wanaoishi Dar es Salaam walikuwa ni takribani asilimia 28.1 ya wakazi wote wa
Jiji. Miaka 16 baadaye, asilimia 16 ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam walikuwa
wanaishi kwenye umasikini. Kwa upande wa Watanzania wanaoishi vijijini, mwaka
1991 kulikuwa na masikini asilimia 40 ya wakazi wote wa Tanzania vijijini.
Mwaka 2007, miaka 16 baadaye, asilimia 37 ya Watanzania wa vijijini walikuwa
wanaishi kwenye dimbwi la umasikini. Takwimu hizi unazipata kutoka Ofisi ya
Takwimu na Shirika la Twaweza limerahisisha taarifa hizi kupitia chapisho lao “Growth
in Tanzania: Is it reducing poverty?”
Masikini wanaoishi Dar es Salaam na
miji mingine nchini wanaweza kujikwamua kutoka umasikini kutokana na fursa
zinazojitokeza mijini. Miundombinu ya usafiri na usafirishaji, viwanda vipya na
fursa za ajira zinajengwa zaidi mijini kuliko vijijini. Huduma za elimu na afya
zinaboreka zaidi mijini na hata walimu na manesi wanakimbilia kufanya kazi
mijini ambako wamerundikana kuliko vijijini ambako kuna upungufu wa kutisha wa
wafanyakazi wa sekta hizo. Masikini wa mijini sio mafukara.
Masikini wanaoishi vijijini licha ya
kufanya kazi kwa bidii na hasa kazi za kilimo hawana fursa za kuondokana na
umasikini. Mfumo wa uchumi wa nchi umejengwa kwa misingi kwamba watu wa
vijijini hupokea bei za kuuza mazao yao kutoka mijini na vile vile hupokea bei
za kununua bidhaa zinazotengenezwa mijini kutoka huko huko. Barabara za
vijijini zina hali mbaya au hazipo kabisa. Huduma za jamii kama elimu, maji na
afya ni mbaya. Huduma za nishati ya umeme hazipo kabisa katika vijiji 96 kati
ya vijiji 100 nchini. Masikini wa vijijini ni mafukara. Wamefukarishwa kutokana
na sera zinazonyonya jasho la kazi yao kwa upande mmoja na sera zinazowanyima
maendeleo ya miundombinu kwa upande mwingine. Asilimia 75 ya Watanzania
wanaishi vijijini hivi sasa na kwenye ufukara mkubwa sana. Kwa makadirio ya
idadi ya watu Tanzania, Watanzania milioni thelathini waishio vijijini ni
mafukara.
Kufunguliwa kwa miundombinu ya
vijijini kama barabara, maji na nishati ya umeme kunaweza kuwaondoa watu wa
vijijini kwenye minyororo ya ufukara kwenda kwenye umasikini na hatimaye
kutokomeza kabisa umasikini. Lakini watawala wanaogawa rasilimali ya nchi
hawataki. Wanasema hakuna rasilimali fedha za kutosha kusambaza umeme vijijini
ili kukuza viwanda vidogo na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kusambaza
maji safi na salama ili kuboresha afya na kumpunguzia mwanamke wa kijijini muda
wa kutafuta maji na kujenga barabara za vijijini ili wakulima wafikishe mazao
yao sokoni. Ikifika kujenga shule na zahanati na vituo vya afya wananchi wa
vijijini wanaambiwa wajenge wenyewe, wajitolee. Ni kweli hakuna fedha za
kuwekeza vijijini?
Ufisadi unatengeneza mabilionea
Itakumbukwa kwamba mwaka 2007, Bunge
la Tisa liliibua kashfa mbalimbali zinazoonyesha namna ambavyo fedha za nchi
zinavyoibwa na viongozi wenzetu wachache. Haina maana kwamba mabunge ya nyuma
hayakuwa na wabunge wenye uwezo au ujasiri wa kuibua masuala ya msingi kuhusu
fedha za nchi, lakini nadhani wakati au mazingira hayakuwa yanaruhusu. Tulishuhudia
ufisadi uliofanywa Benki Kuu ya Tanzania kwa kuibwa kwa zaidi ya shilingi
bilioni 133 za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), utoroshaji mkubwa wa
fedha zilizofikia dola za kimarekani milioni 136 kupitia mradi wa Meremeta
uliokuwa chini ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), uingiaji wa mkataba wa
madini ya dhahabu wa Buzwagi uliokuwa na thamani ya dola za Marekani milioni
400 bila kuzingatia uhitaji wa kuboresha mazingira ya nchi kufaidika na utajiri
wa madini na wizi mkubwa wa fedha za msaada wa kuagiza bidhaa kutoka Serikali
ya Japani (Commodity Import Support) ambapo zaidi za shilingi bilioni 40
ziligawiwa kwa viongozi kadhaa wa serikali na wafanyabiashara.
Kashfa chache zilijadiliwa sana
ikiwamo ile ya mkataba wa kununua umeme wa Richmond ambao sasa unelekea
kuliingiza hasara taifa ya zaidi ya shilingi bilioni 90 kutokana na hukumu ya
kampuni iliyorithi mkataba wa Richmond dhidi ya Shirika la Umeme (TANESCO), ile
ya Buzwagi ambayo ilisababisha kuundwa kwa Kamati ya Bomani na matokeo ya
kamati hiyo ni kuandikwa kwa sera mpya ya madini ya mwaka 2009 na Sheria mpya
ya Madini ya mwaka 2010 na ile ya EPA iliyosababisha baadhi ya watuhumiwa
kufikishwa mahakamani lakini kuacha kitendawili kikubwa kuhusu Kampuni ya
KAGODA ambayo ilikwapua zaidi ya shilingi bilioni 40 katika shilingi bilioni
133 zilizoibwa. Masuala ya MEREMETA na Import Support yamezimika na mshawasha
wa wafuatiliaji wa mambo kufuatilia masuala haya umepungua sana.
Masuala hayo machache yaliyoibuliwa
katika Bunge la Tisa yanaonyesha kwamba kuna rasilimali fedha nyingi katika
taifa ambayo ingeweza kutumika kuwekeza kwenye maendeleo ya watu wa vijijini.
Hata hivyo, rasilimali fedha hii inatumika kufanya Watanzania wachache kuwa
mabilionea kwa njia haramu za kifisadi. Bunge la Kumi, ninaamini, litaibua
masuala mengine zaidi yanayoonyesha namna ambavyo tumeamua kuwafukarisha
Watanzania wengi na kuwabilionesha wachache.
Matrilioni kutoroshwa kila mwaka
Katika Kitabu cha ‘Africa’s
Odious debts: How foreign loans and capital flight bled a continent’
waandishi Leonce Ndikumana na James Boyce wameonyesha kwamba katika kipindi cha
miaka 40 jumla ya dola za Marekani bilioni 11.4 zimetoroshwa kutoka Tanzania
kwa njia mbalimbali. Hizi ni sawa na wastani wa dola za Marekani milioni 285
kutoroshwa kila mwaka kuanzia mwaka 1970 mpaka 2010. Sehemu kubwa ya fedha hizi
zinatoroshwa na kampuni kubwa za kigeni zinazofanya biashara na kuwekeza hapa
nchini (utoroshaji mkubwa umefanyika mara baada ya Tanzania kuanza kuzalisha
dhahabu kwa wingi na kampuni kubwa za nje kuanza kutafuta mafuta na gesi asilia
kwenye pwani ya Tanzania katika Bahari ya Hindi) na sehemu nyingine ni
bakshishi wanayopewa maofisa wa serikali wanaofanikisha utoroshaji huu.
Watanzania hawa (wanasiasa, watendaji, maofisa wa jeshi na usalama wa taifa na
wafanyabiashara) huficha fedha hizi chafu kwenye benki za ughaibuni na hasa
Uswisi, Dubai, Mauritius, Afrika ya Kusini na maeneo mengine (Tax
Havens/Offshore/Treasure Islands). Wengine wamewekeza kwenye mali
zisizoondosheka kama nyumba na zinazoondosheka kama hisa kwenye kampuni
mbalimbali duniani.
Taarifa rasmi ya Benki ya Taifa ya
Uswisi inaonyesha kuwa Watanzania wameficha huko zaidi ya dola za Marekani
milioni 196. Uchunguzi unaoendelea unaonyesha kuwa takribani Watanzania 30
wameficha fedha zao katika benki za Uswisi. Hii ni bila kuhusisha wale ambao
wameficha fedha zao kupitia uwekezaji katika ujenzi wa nyumba na hisa kwenye
kampuni mbalimbali duniani na hasa katika nchi za Mauritius, Afrika Kusini na
Dubai. Uchunguzi pia unaonyesha kuwa Mtanzania mmoja ambaye hana rekodi yeyote
ya biashara zaidi ya utumishi wa umma ameficha takribani dola milioni 56 katika
benki mojawapo nchini Uswisi. Serikali ya Tanzania mpaka sasa imekataa kuchukua
hatua za kuwajua Watanzania hawa na kuhakikisha kuwa mabilioni haya
yanarejeshwa nchini na kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo vijijini. Serikali
ya Senegal hivi karibuni imetuma maombi rasmi kwa Benki ya Dunia kuisaidia
kufanya uchunguzi na kurejesha nchini mwao mabilioni ya fedha yaliyofichwa
kwenye benki za nchi za Ulaya na hasa Uswisi.
Ufisadi unafukarisha
Tanzania ina mtandao wa barabara wa
zaidi ya kilometa 85,000 zikiwamo za vijijini na wilaya zinazosimamiwa na
halmashauri za wilaya na za mikoa pamoja na barabara kuu (zinazosimamiwa na
TANROADS). Fedha zinazotoroshwa kila mwaka ni sawa sawa na kutorosha takribani
kilometa 800 za barabara za lami kila mwaka kwa kutumia gharama za sasa za
ujenzi wa barabara. Fedha hizi pia zinaweza kuunganisha umeme kwenye vijiji
1,300 (asilimia 10 ya vijiji vyote nchini) kila mwaka kwa gharama za sasa za
kuunganisha umeme tena kwenye mikoa ambayo haipo kwenye gridi ya taifa (REA
wanatumia takribani shilingi bilioni saba kusambaza umeme katika vijiji 16 vya
Jimbo la Kigoma Kaskazini). Fedha hizi pia zingeweza kuajiri walimu wengi zaidi
wa vijijini na kwa kuwa miundombinu ya umeme, barabara na maji ingekuwa
imeboreshwa walimu hawa wangekaa vijijini na kufundisha watoto wetu. Ufisadi
kama huu umekosesha nchi rasilimali za kuendeleza watu wake.
Rushwa na ufisadi inatengeneza
Watanzania wachache kuwa mabilionea. Mabilionea hawa ambao wana ushawishi
mkubwa katika kuunda sera za nchi na utekelezaji wake wanasababisha kuundwa kwa
sera na sheria zinazolinda utajiri wa walionacho na kuendelea kuhakikisha
masikini wanaendelea kuwa mafukara. Rasilimali za nchi zinaboresha maeneo
ambayo mabilionea na wasaidizi wao wanaishi na kusahau kabisa kwamba Watanzania
wengi wanaishi vijijini na huko ndipo kuna umasikini mkubwa. Umasikini wa
vijijini kwa kiasi kikubwa unatokana na sera na matendo yanayofukarisha
wananchi wengi.
Ukuaji wa uchumi unaoambatana na
ufisadi wa kiwango kinachotokea Tanzania unawafanya wenye nacho kupata zaidi na
masikini kuwa mafukara zaidi. Tofauti ya kipato katika jamii imezidi kuongezeka
na inaweza kuleta machafuko katika nchi. Takwimu za Pato la Taifa, kwa mujibu
wa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa 2011, zinaonyesha kwamba asilimia 30 ya
Watanzania (the richest 30%) wanamiliki asilimia 75 ya Pato la Taifa.
Tumeona kwamba Watanzania mafukara
wanaishi vijijini, asilimia 75 ya Watanzania, na hivyo takribani
Watanzania milioni 30 wanaoishi vijijini wanaishi katika dimbwi la umasikini.
Vile vile tumeona kwamba asilimia 30 ya Watanzania wanamiliki asilimia 75 ya
Pato lote la Taifa. Pato la Taifa mwaka 2011 lilikuwa shilingi 40 trilioni na
hivyo asilimia 30 ya Watanzania wanamiliki shilingi trilioni 30 katika jumla ya
shilinig trilioni 40. Kutokana na muundo wa uchumi wetu ambapo sekta ya huduma
(service sector) na ile ya viwanda (industrial sector) zinachangia zaidi ya asilimia
70 ya Pato la Taifa na ukweli kwamba sekta zinazokua kwa kasi ni pamoja na
mawasiliano, madini, ujenzi na utalii, ni dhahiri Watanzania na kampuni za
kitanzania wanaomiliki zaidi ya shilingi trilioni moja hawazidi thelathini na
kuna watu wanaweza kuwataja mmoja mmoja kwa majina yao au majina ya kampuni
zao.
Kwa hiyo Watanzania milioni
thelathini wamefukarishwa kwa kunyimwa fursa za kiuchumi na hivyo kumiliki
sehemu ndogo sana ya Pato la Taifa. Wanafanya kazi kwa bidii lakini mfumo wa
kinyonyaji unawaweka katika umasikini wa kudumu. Tumeona kuwa uchumi wa nchi
unazalisha kundi dogo la watu wenye utajiri mkubwa ambao sehemu kubwa
umepatikana kwa njia haramu. Watu hawa pia wanamiliki sekta za uchumi zinazokua
kwa kasi na hivyo utajiri wao unazidi kuongezeka. Hawa wanashirikiana na
Watanzania walio katikati (walalaheri) kuhakikisha wanaendelea kumiliki uchumi
wa nchi. Hawa watu wa kati ndio wanasiasa, warasimu serikalini, wafanyakazi wa
kada ya kati ya kampuni za matajiri hawa au zinazofanya biashara na matajiri
hawa. Badala ya watu wa kati kuweka sera madhubuti za kumkomboa Mtanzania wa
chini aondokane na ufukara, wanaweka mazingira mazuri kwa matajiri kutajirika
zaidi. Hatimaye tunajenga Taifa la Watanzania mafukara milioni thelathini na
mabilionea thelathini. Tukatae.
Tunaweza kujenga taifa la watu wenye
fursa sawa kwa kufanya uamuzi wa kubomoa mfumo wa kiuchumi wa kinyonyaji
tulioanza kuujenga tangu tupate uhuru kwa kuacha kubomoa mfumo wa uchumi wa
kikoloni licha ya Azimio la Arusha. Juhudi za kujenga taifa lenye watu sawa
ziliyeyuka mara baada ya kuamua kufuata sera za ubinafsishaji ambapo
zilitafsiriwa kwa kukabidhi mali za taifa kwa kundi dogo la watu na hivyo
kutengeneza mfumo wa kifisadi ambao sasa umeota mizizi. Kazi zilizofanywa kwa
miaka 20 ya kujenga uchumi wa viwanda ziliyeyushwa katika kipindi cha miaka
mitano tu na viwanda vyote viligawanywa kwa watu binafsi na vingi leo ni
maghala tu ya kuhifadhi bidhaa nyingine.
Ufisadi mkubwa ulishamiri kupitia
sera ya ubinafsishaji ambapo watawala waliokuzwa kwa ‘kanuni’ ya ‘kutosheka’
walijawa na tamaa kubwa na uroho wa mali na kuanza kukusanya chochote
kilichokuwa mbele yao. Hivi sasa nafasi yoyote ya uongozi imekuwa ni nafasi ya
ulaji na sehemu kubwa ya tabaka la watawala kuanzia kwa wenyeviti wa vijijiji,
madiwani, wabunge, mawaziri na hata marais wamekuwa ‘rent seekers’ yaani watu
ambao ni lazima kulimbikiza mali kutokana na nafasi za utawala walizo nazo.
Mfano wa wabunge kulilia nyongeza ya posho za kukaa kitako wakati walimu na
madaktari wanaishi katika mazingira magumu ya kazi ni moja ya tabia za
kutotosheka na tamaa zinazopamba viongozi wa kisiasa wa zama hizi.
Kutochukua uamuzi madhubuti wa
kutokomeza ufisadi na mfumo wake ni kufukarisha Watanzania kwa sababu
rasilimali inayopotea kupitia vitendo vya kifisadi ingeweza kuwekezwa katika
maendeleo ya watu wa vijijini, kwa kukuza shughuli za kiuchumi na kupanua
mapato ya wananchi. Hivi sasa vita dhidi ya ufisadi imekuwa ni turufu ya
kisiasa tu na sio mchakato maalumu wa kuondoa kabisa mfumo wa kifisadi. Ni
lazima kuondoka kwenye hali ya kwamba; ushujaa ni kutaja tu fulani na fulani ni
fisadi, hali ambayo imefikia hata watu wasio na chembe ya uadilifu kuchafua
wengine, na kwenda mbele zaidi kwenye hatua za kubomoa mfumo wa kifisadi.
Hata uchumi ukue kwa kasi ya namna
gani iwapo ukuaji huo unanufaisha kikundi kidogo cha watu hauna maana na ni
hatari kwa uwapo wa taifa lenyewe. Ni lazima kuchukua uamuzi wa kujenga taasisi
zenye nguvu ambazo zitaondoa hali hii ya uchumi kutajirisha wachache na
kufukarisha wengi. Taasisi na mfumo utakao hakikisha kuwa watawala wanawajibika
kwa umma kwa wanayoyatenda na wasiyoyatenda. Mfumo utakaohakikisha kuwa
rasilimali za nchi zinarudi kwa wananchi ili kujenga miundombinu vijijini ya
barabara, maji, nishati ya umeme na huduma za kijamii hasa elimu na afya.
Vinginevyo tutaendelea kuwa taifa vipande vipande kutokana na tofauti kubwa ya
kipato na fursa ndani ya jamii. Tanzania yenye mafukara milioni thelathini na
mabilionea thelathini haikubaliki
No comments:
Post a Comment