Saturday, September 15, 2012

Shigela awajia juu chadema....


 Katibu mkuu wa umoja wa vijana CCM Martin Shigela, akizungumza kitu katika mkutano wa kuchambua wanachama watakaoshiriki katika uchaguzi wa wagombea ngazi za mikoa na taifa mjini Dodoma katika ukumbi wa Chimwaga ama White House.. Wa katikati ni kaimu mwenyekiti wa umoja huo Benno Malisa na wa mwisho ni naibu katibu mkuu wa umoja huo.


UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), wamemaliza kikao cha baraza la umoja huo ambapo wamejadili ajenda mbalimbali za msingi kuhusu Uchaguzi na pia wamejadili juu ya hali ya siasa nchini na mfululizo wa matukio ya uvunjifu wa amani na mauaji, ambapo wamekinyooshea kidole Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kuwa vinara wa matukio ya mauaji, kitu ambacho ni hatari kwa Taifa.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi ya Katibu Mkuu, jengo la Mikutano (whitehouse) katika Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi, Dodoma.

Alisema kuwa,kumekuwa na matukio ya mauaji kwenye mikutano ya chama hicho katika mikoa ya Singida, Igunga, Tabora, Morogoro na Iringa hali ambayo imekuwa ikitishia Usalama na Amani ya Nchi.

“Tunalaani Chadema kuwa vinara wa vurugu zinazosababisha mauaji na kila tukio linapotokea viongozi wa Chadema wanakuwepo, hali inayoonyesha kuwa siasa wanazoendesha si za kistaarabu” alisema

Alisema kuwa Chadema wanachojenga ni hatari kwa Taifa na pia hatari kwa Umoja wa Vijana pia na kama wana mapenzi ya kweli na watanzania waache siasa zinazasababisha mauaji mara kwa mara.

Katika hatua nyingine, Shigela amesema kuwa,Kikao cha baraza Kuu kilimalizika jana na kufanya maamuzi baada ya kujadili na kupitisha majina ya wagombea na baadhi ya nafasi majina yatapelekwa halmashauri kuu ya taifa (NEC) ambacho ni chombo cha mwisho cha maamuzi katika Chama.

Amezitaja nafasi ambazo tayari zimetolewa maamuzi, kuwa ni nafasi ya mwakilishi mmoja kutoka UVCCM kwenda UWT, Mwakilishi mmoja kutoka UVCCM kwenda wazazi, Baraza Kuu taifa nafasi tano Zanzibar na nafasi tano Bara, na sasa orodha hiyo inaandaliwa ili majina ya waliochaguliwa yatangazwe rasmi.

Amesema kuwa,katika nafasi nyingine ikiwemo Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti tayari yamewekewa alama na yatapelekwa Halmashauri kuu ya Taifa (NEC).

Pia amewataka wagombea ambao tayari wamefanyiwa uteuzi waache siasa za kuchafuana na zile za makundi.

Aidha alisema kuwa Mkutano Mkuu wa taifa unatarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 20, mwaka huu na kutaka wajumbe wote kuhakikisha wanafika Dodoma Oktoba 19.

Shigela amesema kuwa, Baraza kuu lilipata nafasi ya kuwapongeza vijana wa Jumuiya kwa kuthibitisha kuwa umoja huo ni tanuru la kuoka viongozi kwa baadhi yao kuteuliwa nafasi mbalimbali serikalini na kwenye Chama na kulitaka Baraza kuu kuzingatia mahitaji ya vijana ili wapate fursa zaidi za kugombea ili umoja huo uweze kupeleka sura nyingi za vijana ndani ya chama.

Pia alisema kuwa wametapa nafasi ya kuitafakari taarifa ya kazi nzuri ya Serikali kwa kuwawezesha vijana katika suala la kuwapatia elimu na kuwawekea mikakati ya miaka mitano ya kusaidia vijana.

Shigela aliitaka Serikali kuwa na mipango ya kudumu ili kuweza kudhibiti majanga mbalimbali yanayotokea hapa nchini k.v mafuriko, kuzama kwa meli, mauaji n.k.

No comments:

Post a Comment