Jembe nikipita pembeni ya moja ya mabasi hayo ya kisasa yaliyomwagwa jijini Kampala. Yanavutia kweli.
Hiki ni kituo cha daladala cha New Tax Park. Kipo katikati ya jiji la Kampala. Hiace hizi tunazipeleka wapi?
Pikipiki ni usafiri maarufu jijini Kampala lakini una hatari moja, nayo ni ajali na nauli kubwa. Mabasi yamekuwa mkombozi wa wengi.
Moja ya Hiace zikiwa katikati ya jiji... Hazitakiwi tena hizi.
Kampala imeamua
kujikomboa katika matatizo ya usafiri kwa kuamua kuingia mkataba wa miaka
mitano na kampuni ya usafirishaji iitwayo Pioneer Easy Bus ambayo imeahidi
kuingiza mabasi ya kisasa yapatayo 522.
Jembe nilijionea
mabasi hayo na kuvutiwa kuandika chochote hasa ukizingatia jiji letu la Dar es
Salaam muda si mrefu litaingia katika harakati ya kupokea mabasi ya kisasa
zaidi kuwahi kutokea katika historia ya nchi yetu.
Lakini bado tatizo
lipo, ni namna gani meya wa Kampala Lord Lukwago ataweza kuyaondoa magari
madogo maarufu ‘hiace’ katika mji wa kampala ambayo yalikuwa yakitoa usafiri
kwa muda mrefu.
Nikiwa Kampala
mwanzoni mwa mwaka huu wakati huduma ya mabasi hayo ikianza, nilishuhudia
vurugu na kutoelewana baina ya madereva wa mabasi hayo na madereva wa ‘hiace’
maana hakika mabasi yameletwa ili kuja kupunguza adha ya usafiri katika jiji
hilo linalokuwa kwa kasi. Lakini na hawa waliokuwepo kwa muda mrefu
tunawasaidia vipi?
‘Hiace’ nauli ni
1000 ya Uganda, na haya mabasi mapya nauli ni 800, 200 pungufu. Unadhani abiria
atakubali kuenda kupinda mgongo katika ‘hiace’ tena kwa nauli ya juu wakati
anaweza kukaa kwa raha katika basi zuri kwa nauli pungufu?
“Lunaana, Lunaana
paka Zana.” Hiyo ni sauti ya kondakta wa basi kubwa akimaanisa ‘mia nane mpaka
zana’ Zana ni eneo la kampala, yaani kutoka Nakasero Kampala mjini mpaka zana
ni mia nane. Wakati ‘Hiace’ wanafanya elf moja.
Si hivyo tu hata
maeneo ya karibu viongozi wa serikali za mitaa ama wilaya za Kampala waliweka
ngumu kidogo kuukubali mradi huu wa mabasi mapya. Maana sehemu kama Wakiso,
Entebbe na Mukono walikuwa na ubishi mkubwa kuyakubali mabasi hayo.
Unajua sababu? Watakosa
pesa za kuiibia Kampala City Council. Maana huu mradi utasimamiwa na mtu
binafsi, hivyo pesa zitakuwa zinapelekwa jiji moja kwa moja. Na wao walishazoea
kuiibia Kampala City Council kwa kusajili ‘hiace’ hewa na baadhi ya vigogo
kuingiza magari yao halafu hawalipi kodi. Hatari kubwa hii.
Ilibidi bunge la
Uganda liingilie kati chini ya kamati ya usafiri na kuamua mradi huo uanze mara
moja mwanzoni mwa mwaka huu. Na kwa kuanza kampuni hiyo ya Pioneer Easy Bus katika
mwezi March iliingiza mabasi 60, halafu baadae ikaongeza mengine 40 na kufanya
mabasi 100. Na mengine 422 yanakuja kukamilisha idadi ya mabasi 522. Si raha
hii jamani?
Kampuni hiyo
imewekeza kiasi cha shilingi bilioni 23 za kiganda sawa dola za kimarekani
milioni 10.
Mabasi hayo
yatapita maeneo muhimu ambayo yalikuwa na tabu ya usafiri mjini Kampala ambayo
ni Mukono, Luzira, Bweyogerere, Ntinda, Mulago, Namugongo, Nakawa, Nateete,
Rubaga na Zana.
Mungu atawajaalia
kuweza kumaliza tatizo la usafiri katika mji unaokuwa kwa kasi sana Afrika
Mashariki na kati.
HAFIDH KIDO
KAMPALA, UGANDA
19/09/2012
+256790836878/
+255752593894
No comments:
Post a Comment