Friday, September 28, 2012
FILIKUNJOMBE ADAI YEYE, MKONO, LUGOLA WALIPONZWA NA PINDA, NAPE ATAKA WASIORIDHIKA WAKATE RUFAA, WASOMI WAPONGEZA
SIKU moja baada ya Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), kutangaza majina ya wagombea, baadhi ya vigogo walioachwa kwenye uteuzi huo wameeleza ya moyoni, huku Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe akisema anaamini ametoswa kwa sababu alitia saini ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Katika Bunge la 10 lililoketi Aprili mwaka huu, baadhi ya Wabunge wa CCM akiwamo Filikunjombe, Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono na Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, waliunga mkono hoja ya kutokuwa na imani na Pinda iliyokuwa imeanzishwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe wa Chadema.
Wabunge hao wa chama tawala, waliungana na wenzao wa upinzani kutaka kupiga kura za kutokuwa na imani na Pinda kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ameshindwa kuisimamia Serikali kwa kuwawajibisha mawaziri wazembe. Hata hivyo, mpango huo haukufanikiwa baada ya Spika wa Bunge Anne Makinda kueleza kuwa haukufuata taratibu zinazotakiwa.
Filikunjombe alipotakiwa jana kuzungumzia kuenguliwa kwake kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi wa ndani ya chama, alisema anaamini yeye na wenzake hao wa CCM, wametoswa kwa sababu ya kushiriki mpango wa kumng'oa Waziri Mkuu Pinda. Hata hivyo, alisema amelazimika kukubali hali hiyo na kupokea matokeo, kwa kuwa hatua yake ya kusaini kitabu hicho ilitokana na nia njema kutaka Waziri Mkuu ajiuzulu ili mambo fulani muhimu katika jamii yafanyike.
Filikunjombe alibainisha kuwa alisaini kitabu hicho cha kutokuwa na imani na Pinda akiwa na akili timamu na alikuwa anajua kinachoweza kutokea kutokana na hatua yake hiyo. "Nimesaini kitabu kile kwa nia njema, nikiwa na akili timamu na sijutii uamuzi wangu huo, ila siwezi kuwasemea Kigwangalla (Khamis mbunge wa Nzega) na Bashe (Hussein). Lakini sisi watatu (yeye, Lugola, Mkono) tumeenguliwa kwa sababu hiyo (ya kutokuwa na imani na Pinda)." Aliendelea: "Nashangaa leo naonekana adui wa chama wakati nilikuwa nakinusuru na kusema kweli adui wa CCM ni Wabunge wa chama hicho ambao hawakusaini kitabu hicho cha kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, " alisema Filikunjombe.
Mkono Mbunge wa Musomo Vijijini, Nimrod Mkono alisema kutoswa kwake ni uamuzi wa watu aliowaita wenye chama. "Walikata jina langu nikakata rufaa, likarudishwa Dodoma, lakini walipokutana wakaona sifai. Wakaamua kunifukuza sasa hapo mimi nifanye nini?" alihoji Mkono. Mkono alisema huu ni utaratibu wa chama chao cha CCM ambao umewapa baadhi ya watu haki ya kuwafukuza wengine bila kuwapa fursa ya kujitetea. "Kama ilivyotokea kwangu wamekaa na kuona Mkono hafai, fukuza basi wakafanya hivyo na hiyo haijalishi kama nilisaini kutokuwa na imani na Waziri Mkuu au la.
Suala la msingi ni kuwa Mkono amefukuzwa na atarudi kama ilivyokuwa kwa mwana mpotevu." alisema bila kufafanua. Kigwangalla Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla alisema anaheshimu uamuzi wa vikao vilivyokaa na kufikia uamuzi uliochukuliwa na kwamba, ataendelea kuwa mwanachama na kukitumikia chama pamoja na wananchi kwa nguvu zote bila kinyongo. “Nitaendelea kuheshimu vikao vya chama changu na kuwa mwanachama hai ingawa sijajua wametumia vigezo gani kuteua majina hayo,” alisema Dk Kigwangalla. Bashe Kwa upande wake Bashe alisema kilichotokea ni uamuzi wa chama na vikao halali vilivyokaa na kuchukua uamuazi huo.
“Sijui kwa nini jina langu halikupitishwa, lakini nitaendela kuwa mwanachama na kuwatumikia wananchi wenzangu wa Nzega,” alisema Bashe. Katika kuhakikisha hilo, Bashe alisema leo anakwenda Nzega kupeleka mifuko ya saruji tani 18 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za kata za chama hicho wilayani humo.
Nape ajibu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alitaka makada waliotoswa na wenye kinyongo wawasilishe malalamiko yao CCM kwa maandishi badala ya kulalamika nje ya utaratibu."Wathibitishe kwa maandishi nasi chama tutajua la kufanya, kwani wabunge hao hawakuingia katika vikao vilivyotoa maamuzi sasa nashangaa kusikia katika vikao tuliwajadili na hoja iliyowaondoa ni hiyo," alisema Nape. Maoni ya wasomi Wakizungumzia uteuzi huo wasomi na wanasiasa walitoa maoni tofauti huku baadhi wakisema chama kinatakiwa kuwa na sera na mtizamo wa kuliletea maendeleo taifa bila kujali kama chama kinaongozwa na wazee au vijana.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema uamuzi huo wa CCM umeonyesha kuwa, ndani ya chama hicho hakuna aliye juu kuliko mwenzake. “Wapo waliosema wakitoswa patachimbika, lakini wametoswa na hapajachimbika, uamuzi wa kuwatosa watu wa aina hii utarejesha nidhamu ndani ya chama hicho licha ya kuwa kazi bado ni kubwa,” alisema Dk Bana. Profesa Gaudence Mpangala alisema vijana kupewa nafasi kubwa ya kugombea nafasi mbalimbali ndani ya CCM, hakuna maana kuwa sera na mtizamo wa chama hicho utabadilika.
“Kuwa na wanachama au wagombea wenye umri wa wastani(vijana) sio kigezo cha chama kufanya vyema kwa sababu hawawezi kubadili sera na mtizamo wa chama husika,” alisema Mpangala. Dk Kitila Mkumbo alisema kuingiza vijana wengi katika mpambano huo ni hatua ya ukomavu wa kisiasa kwa kuwa chama hicho awali hakikuwa na utaratibu mzuri wa kuwapa nafasi ya uongozi vijana. “Awali Chadema ndio kilionekana chama kinachowapa nafasi zaidi vijana, lakini kwa hatua hii ya CCM ni nzuri, sasa tunasubiri utendaji wao kama utakuwa na manufaa kwa taifa,” alisema Mkumbo.
Bashiru Ally alisema kama kigezo cha kuweka vijana wengi kitazingatia msimamo, fikra na ufanisi katika utendaji kazi wao basi taifa lina kila sababu ya kuunga mkono hatua hiyo.Alisema kwa kuwa vijana ndio chachu ya maendeleo kwa mataifa mbalimbali duniani, hatua ya CCM kuwapa nafasi vijana ni nzuri kama wakiifanya kazi hiyo kwa manufaa ya taifa kwanza.
Habari hii imeandikwa na Ibrahim Yamola, Fidelis Butahe, Elizabeth Edward na Joseph Zablon,Mwananchi .
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment