Thursday, September 27, 2012

AMEEN KASHMIRI, MWANAJESHI MZALENDO WA TANZANIA ALIYEPITIA MENGI.




"MZIGO MZITO APEWE MNYAMWEZI".

Historia ya Tanzania ina mengi na ina wengi ambao hawajazungumzwa, kiasi ambacho kuna mambo yakizungumzwa basi yanaweza kukusisimua na kukufanya ujisikie fahari sana kuwa Mtanzania.

Leo tunamzungumza Mzee wetu Mashuhuri Ameen Kashmiri. Askari Mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambaye historia ya maisha yake inatupa mafunzo na kutufamamisha mengi sana ambayo hatukuwa tukiyajua.

Ameen Kashmiri alizaliwa tarehe 31 mwezi Oktoba mwaka 1935 huko Mjini Tabora wakati huo kukijulikana kama Jimbo la Magharibi, sehemu kubwa ya maisha yake ya utottoni ameyatumia huko wakati Baba yake ambaye alikuwa Mfanyakazi wa Shirika la Reli la Tanganyika alipokuwa kwenye Tawi hilo la Tabora.

Maisha ya Wafanyakazi wa wakati huo yalikuwa ya kuhamahama sana jambo ambalo lilimfanya Mzee Kashmiri asikae sana Tabora. Alihamishiwa Mkoani Dodoma, kisha Dar es salaam ambako nako hakukaa sana kabla ya kuhamishiwa Jimboni Tanga ambako ndipo sehemu alitumia sehemu kubwa ya maisha yake na ndipo Elimu na Mafunzo ya Mwanawe Ameen yalipopatikana.

WITO WA KUTUMIKIA UMMA, UBAGUZI KWA WATANGANYIKA.

Mwaka 1956 Bwana Ameen Kashmiri alihitimu Elimu yake ya Upili (Sekondari) katika Skuli Maarufu Jijini Tanga iliyojulikana kwa jina la Shule ya Karimjee (Sasa hivi ikijulikana kama Shule ya Sekondari Usagara), ambapo kwa wakati wake alikuwa mmoja ya wanafunzi wenye uelewa mkubwa sana.

Tokea Shuleni yeye na baadhi ya Wenzake walivutiwa sana na habari na masimulizi ya Ushujaa, Ujasiri na kusisimua ya wazee wengi wa Tanga ambao walikuwa Sehemu ya Jeshi la Wakoloni wa Kiingereza lililokwenda Burma na Somalia wakati ule wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, na hivyo kuwafanya wavutiwe sana na wawe na wito wa kuwa Maaskari Jeshi.

Mara tu alipomaliza Shule alifanya jitihada mbalimbali za kuomba kujiunga na Jeshi lakini mara zote alikataliwa. Pamoja na kuwa alionekana mweupe kwa rangi tofauti na Watanganyika wengine lakini bado alibaguliwa na Maofisa wa Kikoloni kwa kuwa Rangi yake haikuondoa Utanganyika wake au kubadili lafudhi yake ya Kiswahili safi, kwa wakati husika Askari wa Jeshi la Kikoloni la Tanganyika (Kings African Rifles) hawakuwa wakipenda sana kuwaingiza vijana wa Kitanganyika Jeshini kwa sababu mbalimbali.

Akiwa kakatishwa tamaa kwa kukataliwa kwake kuingia Jeshini, Ameen alikataa kuomba nafasi mbalimbali za kazi ambazo zilikuwepo kwa watu wa kiwango chake cha elimu kwa wakati huo. Baada ya Ushauri na kubembelezwa sana na baba yake aliamua kukubali ajira ya Uhasibu katika Kampuni ya Tom Co. Ltd kazi ambayo pamoja na kuwa hakuipenda lakini aliifanya kwa ufanisi sana kiasi kwamba baada ya muda tu alipandishwa cheo na kuwa Mhasibu Mkuu wa Kampuni.

MCHAKAMCHAKA, ASKARI MKAKAMAVU AMEEN KASHMIRI.

Mwishoni mwa Mwaka 1957 Jeshi la Wakoloni lilifungua Milango kwa Vijana wa Kitanganyika kujiunga nalo. Wakati huo wito na kampeni ilifanywa nchi nzima ili kuwahamasisha na kuwasajili vijana mbalimbali ambao walitaka kujiunga na Jeshi hilo nafasi ambayo Mzee Ameen hakuiacha impite hivi hivi, hivyo akawa miongoni mwa vijana wachache wenye Elimu wa Kitanganyika wa wakati huo kukubali kujiunga na Jeshi hilo.

Baada ya Maombi na Usaili mwezi Januari mwaka 1958 Mzee Ameen Kashmiri, Mrisho Sarakikya na Alex Nyirenda walichaguliwa kujiunga na Mafunzo ya Juu ya Kijeshi katika Chuo cha Royal Military Academy, Sandhurst, Nchini Uingereza ambapo baadaye Mzee Mrisho Sarakikya aliachwa katika Orodha ya Wanafunzi waliotakiwa kwenda Uingereza kwa sababu ya Ufaulu wake mdogo kwenye Somo la lugha ya Kiingereza. kabla ya kwenda huko Nchini Uingereza kwa ajili ya Mafunzo yao ya Juu ya Kijeshi kwanza walipelekwa Nairobi Nchini Kenya na kisha Jinja Nchini Uganda kwaajili ya Mafunzo ya kawaida ya Kijeshi.

Mafunzo ya Kijeshi yaliyokuwa yakifanyika Nairobi na kisha Jinja Nchini Uganda yalihusisha pia Vijana kutoka Kenya na Uganda, ambapo wakati wakimalizia mafunzo kule Jinja ni watu nane (8) tu katika kundi zima ambao walichaguliwa kujiunga na masomo ya Juu ya Kijeshi ambapo watatu walitoka Kenya na Tanganyika alikuwa ni yeye na Nyirenda tu baada ya kuondolewa kwa Sarakikya.

MAFUNZONI, JASIRI AMEEN KASHMIRI ALIYEWEKA MSINGI.

Mzee Ameen na vijana wenziwe walipokelewa vizuri tu Nchini Uingereza, lakini Bodi ya Uchaguzi wa Jeshi la Uingereza iliwachagua yeye na kijana wa Kizungu kutoka Kenya moja kwa moja kwenda Chuoni Sandhusrt na wale wenzao waliobakia (akiwemo na Nyirenda) walipelekwa katika Chuo cha Mafunzo cha Makuruta cha Mons kabla ya kurudisha kujiunga na kina Ameen miezi sita (6) baadaye.

Mwezi Juni mwaka 1960 alimaliza mafunzo na kufaulu kuwa Askari Jeshi Luteni mwenye Nyota Mbili (Second Lieutenant) ambapo alikuwa mtu wa kwanza kufaulu chuoni hapo kutoka katika Nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Mara baada ya kumaliza Mafunzo yake Ameen Kashmiri alirudi Tanganyika na kujiunga na kikosi Namba sita cha King's African Rifles katika Kambi ya Calito (sasa Lugalo).

KIKOSI CHA BENDERA, MZALENDO AMEEN KASHMIRI.

Mwaka 1961 Tanganyika ilipata Uhuru wake kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza, Usiku wa kuamkia tarehe 9 Desemba mwaka 1961 kulikuwa na Shamra shamra nyingi sana ikiwemo kitendo cha Mzee Nyirenda kuupandisha Mwenge wa Uhuru kwenda katika kilele cha Mlima Kilimanjaro na matukio mengine mengi sana ya kusisimua.

Mzee Ameen Kashmiri alikuwa katika Kikosi cha Bendera kwenye Sherehe za Uhuru zilizofanyika katika Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) Jijini Dar es salaam asubuhi ya siku hiyo ya Uhuru. Ameen alibeba Bendera ya Uhuru ya Tanganyika (kama anavyoonekana pichani) ambayo ilipandishwa Juu siku hiyo huku askari mwenzie akiwa amebeba Bendera ya Wakoloni wa Kiingereza ambayo ilishushwa rasmi siku hiyo na Kiongozi wa Harakati za Uhuru wa Tanganyika Mwalimu Julius K Nyerere kuashiria Uhuru kamili wa Tanganyika.

MASHUHURI AMEEN KASHMIRI, MBEBA BENDERA YA MATUMAINI YETU.

Jukumu kubwa na zito la kubeba Bendera ya Tanganyika katika siku ile ya kukumbukwa linaonyesha weledi, kuaminiwa, ujemedari na uzalendo wake ambao haukuwa na mashaka kwa Taifa hili, tukio hilo ni kiashiria na kielelezo cha umuhimu na mchango wake katika Historia njema ya Tanganyika.

Yeye binafsi siku zote anasema hawezi kulisahau kabisa tukio hilo mpaka kufa kwake, kwake ni tukio lenye kubeba ufahari wa kitanzania, umashuhuri wa kizalendo na ujemedari wa uaminifu wa kitumishi kwa umma wa Watanzania. Heshima ambayo alipewa na wanawema wenziwe haina mithali kwake.

Tukio la Mzee Ameen Kashmiri kubeba bendera ile ya Matumaini ni jambo lenye kusisimua sana nyonyoni mwetu watanzania wote mpaka leo hii, kumbukumbu njema za tukio hilo kwa wale waliokuwepo siku hiyo ni jambo la kifahari na linarithisha Uzalendo na kuipenda Nchi kwa sisi Vijana wadogo wa Kitanzania ambao hatukuwepo wakati ule, ni tukio adimu lenye kumfanya Mzee Ameen Kashmiri kuwa Mtu Mashuhuri sana nyoyoni mwetu.

MAASI YA KIJESHI, USULI WA "AFRICANIZATION". 

Usiku wa kuamkia Januari 21, 1964, Jeshi la Tanganyika liliasi na kushikilia serikali kwa muda, tukio ambalo Baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alilielezea kuwa ni “siku ya aibu sana kwa Taifa”. Wakati jeshi hilo likiasi siku hiyo hiyo, na saa hiyo hiyo, majeshi ya Kenya na Uganda nayo yaliasi kwa staili hiyo hiyo. Maasi yote ya nchi tatu hizo yalizimwa na majeshi ya Uingereza siku moja na wakati huo huo. Kwa Tanganyika, maasi haya yalitokea wiki moja tu baada ya mapinduzi ya umwagaji damu ya Zanzibar, Januari 12, 1964; na usiku huo wa maasi hayo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Zanzibar “Field Marshal” John Gidion Okello, alikuwa na mazungumzo na Mwalimu Nyerere Ikulu, Dar es Salaam, katika hali ya kubadilishana mawazo juu ya hali ya Zanzibar ambapo Mwalimu, alimshauri Okello afanye kazi kwa imani na Rais Abeid Amani Karume. 

Mara baada ya Uhuru Tanganyika (sasa Tanzania bara) ilirithi Jeshi kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza lililokuwa likijulikana kama “Kings African Rifles” – (K. A. R) na baadaye kuitwa “Tanganyika Rifles” (TR). Katika kipindi kufuatia uhuru, ili kukidhi matarajio ya Watanganyika, zilitakiwa hatua za haraka kuhakikisha nafasi zote za juu serikalini na taasisi zake (likiwemo jeshi), zinashikwa na Wazalendo. Huu ni utamaduni uliokuwa umejengeka kwa nchi zote za Kiafrika zilizokuwa zikipata uhuru

Nyerere hakuwa na ujasiri wa kuchukua hatua haraka hivyo, kama pia ambavyo Waziri wake wa Mambo ya Ndani wa wakati huo, Clement George Kahama, hakuwa na ujasiri wa kuwatimua Waingereza katika nafasi za juu ndani ya Jeshi la Polisi. Yakaanza malumbano ndani ya Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Tawala, Tanganyika African National Union (TANU), kwamba Nyerere alikuwa anairudisha Tanganyika katika enzi za Ukoloni, na hivyo kwamba “uhuru” haukuwa na maana kwa Watanganyika kwa kushindwa kwake kuwapa vyeo Waafrika.

Ili kuepusha shari, na ili Chama kisifarakane, Mwalimu akaachia ngazi Januari 16, 1962 na kurejea kijijini kuimarisha Chama kama Mwenyekiti wa Taifa wa TANU na Rashid Kawawa akachukua Uwaziri Mkuu. Naye Oscar Kambona, ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Elimu, akawa Waziri wa Mambo ya Ndani badala ya George Kahama. Wote wawili hao wakaachiwa kazi ya kuwaondoa Wazungu katika vyeo walivyokuwa bado wanashikilia haraka bila visingizio.

Kazi ya kwanza ya Kambona ilikuwa ni kumtimua Kamishna wa Polisi Mwingereza, na kumteua Bwana Elangwa Shaidi kuchukua nafasi hiyo, lakini hakufanya mabadiliko kwa Jeshi (Tanganyika Rifles).

Zoezi hili la “Africanisation” lilifanywa kwa kasi ya kutisha kiasi cha kuishitua jamii ya Kimataifa. Desemba 1962, ulifanyika Uchaguzi Mkuu ambapo Mwalimu Nyerere alichaguliwa kuwa Rais Mtendaji wa kwanza. Kwa hiyo, Januari 1963, Mwalimu alirejea madarakani kama Rais wa kwanza wa Tanganyika na kusitisha mara moja zoezi la “Africanisation” na kuchochea hasira ya viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi nchini, ambao waliapa kutolala usingizi, wala kuupa nafasi uamuzi wa Mwalimu wa kusisitiza zoezi la kuwapa madaraka Watanganyika.

AMEEN KASHMIRI CHINI YA ULINZI, ASKARI WA KWANZA WA CHEO CHA JUU KUKAMATWA. 

Matata yalianza usiku wa Januari 20, kuamkia 21 usiku huo, siku ambayo Okello alikuwa na mazungumzo na Mwalimu, Ikulu usiku. Mzee Ameen Kashmir anaikumbuka sana siku hii kwa kuwa yeye ndiye Aliyekuwa Ofisa wa zamu wa wiki ile.

Saa 11 jioni alianza utaratibu wa kichunguza (routine inspection) kwa kuanzia Eneo la Ikulu na kisha kupita katika maeneo yote nyeti ya Nchi ambapo kila kitu kilionekana kuwa shwari na hakukuwa na vishiria vyovyote vya uwepo wa tukio la Jeshi kuasi.

Mara baada ya ukaguzi huo kwenye maeneo nyeti ya Nchi aliamua kurudi katika kambi kuu ya Colito ambapo alishangazwa sana na hali ya kukuta taa zote za kambi zikiwa zimezimwa jambo ambalo halikuwa la kawaida lakini aliondoa hisia mbaya na kuhisi labda kulikuwa na matatizo ya umeme kambini hapo.

Wakati alipokuwa amevalia Sare zake maridadi za Jeshi alijitambulisha kama Askari wa Zamu wa Jeshi wa wiki, ambapo mara baada ya Geti kuu kufunguliwa na yeye kuingia alishangaa anawekwa Chini ya Ulinzi na Askari wenzie jambo ambalo halikumshangaza kwa kuhisi ni utani tu.

Baada ya muda aligundua kuwa kilichokuwa kinatokea si utani tena na ni uasi kamili wa Jeshi ambapo yeye alikuwa Afisa Mkuu wa Kwanza kuwekwa ndani, kisha king'ora kilipigwa kambini hapo kuashiria kutakiwa kwa askari wote kukusanyika katika uwanja, ambapo wasaa huo ndiyo ulitumika kuwaweka chini ya ulinzi Askari wengine wa kizungu waliokuwa na vyeo vya juu.

Lakini ilipofika saa 7:50 alfajiri, Januari 21, Mkuu wa Kikosi cha kwanza cha TR, Brigedia Patrick Sholto Douglas, aliamshwa nyumbani kwake na sauti ya baruji (buggle) na ving’ora, karibu na kambi ya Jeshi ya Colito (sasa Lugalo Barracks).

Alipotoka nje, aliona askari wake 12 wakikamatwa na wenzao wenye silaha na kutiwa mahabusu. Ndipo alipofahamu kwamba, nusu ya askari 800 wa Kikosi hicho walikuwa wameasi. Aliweza kutoroka yeye na familia yake hadi katikati ya jiji, akaiacha familia kwa Balozi wa Australia, kisha akakakimbilia kwa Afisa mwenzake, eneo la Oyster Bay na kutumia wasaa huo kumjulisha kwa Simu Waziri Kawawa juu ya kinachoendelea. Mzee Ameen anawataja askari wengine wa cheo cha juu waliofanikiwa kutoroka kuwa ni Meja Maricadi pamoja na Mkuu mwengine mmoja ambaye amemsahau jina ambaye alijificha kwenye mapori ya Kunduchi.

KASHMIRI UGHAIBUNI, HUZUNI YA KUKUMBUKA NYUMBANI.

Akiwa amefungiwa katika Mahabusu ya Jeshi katika kambi ya Colito, Mzee Kashmiri anakumbuka sana kumuona Waziri Kambona akifanya juhudi mbalimbali za kupoza na kutuliza maasi yale, Kama moja ya matakwa ya Askari wale waasi ilimbidi Kambona akubali kuwasafirisha mpaka Nairobi Viongozi wote wa Jeshi ambao walitiwa ndani (akiwemo Kashmiri) na wale walioasi bila kipingamizi ambapo baadaye walisafirishwa kwenda Uingereza.

Anakumbuka vyema wakati akiwa ndani ya Gari wakitaka kusafirishwa namna mwenzie Nyirenda alivyoulizwa "Wewe Mswahili nawe unakwenda wapi?", jambo ambalo lilimhuzunisha sana yeye kwa kuona ameachwa kwa kuwa yeye hakuwa Mswahili kama Nyirenda kwa kudhaniwa naye ni mzungu tu kwa sababu ya rangi yake.

Maasi yale baadaye yalizimwa kwa msaada mkubwa wa Majeshi ya Kikoloni ya Kiingereza na baadaye Kikosi cha Ulinzi cha Jeshi la Nigeria chini ya Generali Ochukwu kilikuja kuchukua nafasi ya Jeshi la Uingereza, wakati huo Kashmiri alikuwa tayari yuko Uingereza ambapo aliishi kwa muda wa miezi minne ya Upweke na kutokupata mawasiliano yoyote na Serikali ya Taifa lake. Waingereza walijaribu kumpa Ajira Mzee Kashmiri lakini aliwakatalia na kuwaambia kuwa yeye ni Mwanajeshi wa Tanganyika na hivyo hawezi kufanya kazi nyengine yoyote.

Mwezi April mwaka huo (1964) alipata simu ya maandishi (Telefax) kutoka kwa Waziri Mkuu wa Tanganyika, Mzee Rashid Mfaume Kawawa ikimtaka arudi nyumbani jambo ambalo lilimpa faraja kubwa sana. Kabla ya Maasi yale ya Jeshi alikuwa ameomba ruhusa Jeshini ya kwenda kusoma Kozi Fupi ya Utawala wa Jeshi hivyo aliomba kutumia muda ule ambao yuko kule Uingereza kusoma kozi hiyo ambayo aliimaliza Mwezi Julai mwaka huo huo kisha akarudi nyumbani ambapo wakati huo haikuwa Tanganyika tena bali Tanzania.

JWTZ, FAHARI YA WATANZANIA.

Mara baada kurudi Nchini Mzee Ameen Kashmiri alipewa Cheo cha Ukuu wa Utawala na Uhandisi ambapo alifanya kazi nzito na ya kizalendo ya kujenga Jeshi Imara la Wananchi wa Tanzania kwa muda wa miaka minane.

Ilipofika Mwaka 1974 Mzee Kashmiri alikuwa amemaliza kazi yake ya kujenga Jeshi lenye Askari Imara na wakakamavu zaidi ya 30,000 kutoka kati ya wale 400 waliobakishwa mara baada ya kuvunjwa kwa Tanganyika Rifles, ambapo anaelezea namna ambavyo waliweza kusajili askari zaidi ya 2,000 kwa kila mwaka mpaka kufikia kiwango hicho, ambapo alichangia kulijenga Jeshi hilo kuwa imara, lenye nidhamu na lililo madhubuti zaidi katika Ukanda wote wa Afrika Mashariki.

MTUMISHI WA UMMA ASIYECHOKA.

Mwezi Januari mwaka 1974 Mzee Kashmiri alistaafu kwa heshima zote kutoka Jeshini na kuwaachia nafasi vijana wapya ambao alishiriki kuwaunda washike nafasi yake ili kuliendeleza na kuliimarisha zaidi Jeshi kutoka pale yeye alipoishia.

Kama vile walivyo wazalendo wengine wote kustaafu hakuna maana kuwa hawezi tena kulitumika Taifa lake, alirudi tena kwenye utumishi wa umma mara baada ya kuombwa na Rais Nyerere kuwa Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Sukari (SUDECO), kazi ambayo aliifanya kwa muda wa Miezi Miwili mpaka alipoondoka kwenye Ukuu huo mwaka 1976 ambapo alirudi tena Jeshini wakati wa Vita vya Kagera. 

RAFIKI WA KWELI NA MZALENDO ANAYELIPENDA TAIFA LAKE.

Mzee Ameen Kashmiri yu hai, japo siku hizi amekuwa mtu mzima sana na akijishughulisha zaidi na shughuli zake binafsi katika sekta ya uchimbaji wa madini pamoja na kuwa karibu na Familia yake.

Wakati wa Kilele cha Sherehe za Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam mwaka 2011 Mzee Kashmiri alikuwa mmoja wa wahudhuriaji uwanjani hapo. Rais Jakaya Mrisho Kikwete alipata nafasi ya kuzungumza naye na alimpongeza na kummwagia sifa kwa kuwa mmoja wa mashujaa wachache wa Uhuru walio hai na kuvutiwa naye kwa kulipenda Taifa lake siku zote.

Wakati wa Maadhimisho ya Miaka Hamsini (50) ya Uhuru wa Tanzania Bara (Tanganyika) Familia ya Marehemu Brigedia Alex Gwebe Nyirenda (ambayo Mzee Kashmiri ndiye Baba Mlezi wa Familia hiyo) iliandaa tukio lililoitwa GWEMBE NYIRENDA MEMORIAL KILIMANJARO EXPEDITION ambalo limepangwa kufanyika kila Mwaka, tukio hilo likihusisha Upandaji wa Kuchochea Utalii na kuutangaza Mlima wa Kilimanjaro kwa kukumbuka Tukio la Kuupandisha Mwenge wa Uhuru Mlimani hapo lililofanywa na Nyirenda.

Mzee Ameen Kashmiri, Kaka na Dada Alex Foti Gwebe Nyirenda na Tima Gwebe Nyirenda (WATOTO WA MZEE NYIRENDA), Mobeen Kashmiri (MTOTO WA MZEE KASHMIRI) waliwaongoza ndugu jamaa na marafiki katika tukio hilo adhimu la kumkumbuka rafikiye Nyirenda.

Mzee Kasmiri ni mtu mwenye Utu, Upendo na kujali kulikopita mipaka, miaka yote amekuwa baba na mlezi mwema wa watoto hao wa Rafikiye wa kweli Nyirenda, kiasi amewafariji na kuwafanya wajihisi kama vile baba yao yu hai bado. Yote hayo yakionyesha sura halisi ya wema na umashuhuri wa Mzee wetu Ameen Kashmiri.

Chanzo: ukurasa wa facebook ‘watanzania mashuhuri’

No comments:

Post a Comment