Ndugu zangu,
Mungu akinipa uhai na afya
kesho nitakuwa safarini kuelekea Uganda ,
nafuatilia masuala yangu ya shule mjini Kampala .
Kwa muda mrefu tangu mwaka
2008 nimekuwa nikitumia njia moja tu kuenda na kurudi Kampala njia ya Arusha-Nairobi. Ni mara moja
tu nilitumia njia ya Tanga-Mombasa wakati nilipokuwa nikirudi mwanzoni mwa
mwaka huu.
Lakini kwa kuwa sasa nina
kitu cha kusemea, nataka kutumia njia ya Bukoba nipitie mpaka wa Malaba nitokee
Masaka kusini mwa Uganda .
Lengo ni kupata taswira ya
nchi yetu maana kwa njia hiyo ya kupitia Bukoba nitafanikiwa kupita mikoa
takriban saba ama minane. Niliwahi kupita mpaka wa Malaba mara moja nikielekea
Bukoba kutoka Kampala .
Ni katika kampeni za uchaguzi wa mwaka 2010-2011 zilizomrudisha madarakani kwa
mara nyingine Rais Yoweri Kaguta Museveni. Nilikimbia vurugu za Museveni na Dr Kiiza
Bessyige nikarudi nyumbani lakini niliishia Bukoba nikakaa wiki moja halafu
nikarudi Kampala ,
hivyo sikuifaidi mikoa mingine.
Mara hii nitafanikiwa kupita
mikoa kuanzia Dar es Salaam , Pwani, Morogoro, Dodoma , Singida,
Shinyanga, Mwanza na Bukoba. Si mzuri sana
wa ramani ya upande huu lakini nadhani mikoa hiyo nimeipatia vizuri kutoka Dar
es Salaam kuelekea Bukoba.
Ni safari ndefu na ya
kuchosha kidogo, lakini mara nyingi hupenda kuona mikoa mingi zaidi ya nchi
yetu kubwa. Kadhalika nitajionea karaha za barabara mbovu na hali halisi ya
maisha ya mtanzania alie mikoani.
Tumeshajizoesha kuishi mjini,
hatuoni mambo mengi yanayowasibu watu huko mikoani hasa maeneo ya vijiji. Yapo
mambo mengi sana
wananchi wa vijijini wanataka viongozi wayaone. Miundombinu mibovu, zahanati
chache tena zisizo na sifa, vyumba vya madarasa visivyo na hadhi na hata vyenye
hadhi havina walimu wa kutosha. Matatizo ya maji na umeme. Yapo mengi sana ambayo nitajionea.
Ningetamani kupata fungu zuri
la pesa halafu nikawa nasafiri kwa mafungu mpaka nifike safari yangu, yaani
kila mkoa nishuke na kukaa siku moja. Lakini kufanya hivyo kunahitaji pesa ya
kutosha na kama mnavyofahamu blogu yenu ni
changa haijaanza kupata matangazo. Lakini hiyo ni ahadi naiweka, Mungu
anisimamie niweze kuitimiza, ipo siku nikipata ufadhili nitaizunguka Tanzania na
kuanika kila tatizo linalokumba watu wa vijijini. Maana magazeti yetu
yanaandika habari za mjini tu na za kina Diamond na Mr Blue.
Labda niwape siri, nawapenda sana watu wa vijijini, ningetamani sana siku moja maisha yangu niyahamishie huko
nami niwe mkulima. Lakini nikihamia vijijini blogu ya kidojembe itakosa wa
kuiendesha maana vijiji vingi vya Tanzania
havina huduma ya mtandao, na hata ukiwepo unakuwa chini sana . Ingawa si vijiji vyote.
Mwalimu Nyerere, alipata
kutamka kuwa kama tunataka maendeleo ya nchi
kwanza tuimarishe vijiji vyetu. Tukipeleka huduma nzuri vijijini kama Zahanati na Hospitali kubwa, kuanzisha mashamba
makubwa ya mazao ya biashara na chakula, maduka makubwa ya pembejeo za kilimo,
shule za kisasa zenye walimu wa kutosha, barabara inayopitika kwa kipindi
chote. Na mambo mengi mazuri.
Basi mjini kutakosa watu,
maana watu wote watahamia vijijini kufanya kazi, hii itapunguza msongamano
mijini na hata ikibidi baadhi ya ofisi za serikali zikahamia huko vijijini
itaamsha ari ya watu kuendeleza vijiji ili pawe mahala bora pa kuishi.
Matokeo yake Tanzania nzima
itajengwa na itachochea wawekezaji na hata wageni watakuwa wengi kwa maana watu
hupenda maendeleo. Pesa itakuwa na mzunguko mzuri na hata thamani yake
itapanda, hivyo uchumi utakuwa kwa haraka bila kutarajia. Wawekezaji hawataki
kutuletea maendeleo, wanachotaka ni kuona tunajiendeleza wenyewe ili waje kuwekeza.
Aidha, vijijini ndipo palipo
na wapiga kura; watu wa mjini hawana muda wao wanatafuta pesa muda wote. Lakini
cha kushangaza viongozi wakishakwenda kuomba kura huko vijijini wanarudi mjini
na kusahau kabisa kama kuna watu waliwaahidi
jambo. Maendeleo yote huyaleta mjini. Kule mpaka baada ya miaka mitano ndipo
wanarudi tena.
Nifupishe mjadala huu kwa
kusema nakwenda kuwatazama watanzania halisi. Watanzania wanaoilisha nchi hii
na kuendelea kuwaweka madarakani viongozi ambao hawawakumbuki lakini hawakati
tamaa kuwapokea kila wanapoona umaarufu wao kisiasa unapungua.
Kesho nitakuwa safarini jembe
lenu niombeeni nirudi salama. Sitorudi mikono mitupu nitawaletea zawadi; na
zawadi ya mwandishi ni picha na habari..
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM , TANZANIA
0713 593894/ 0752 593894
09/09/2012
No comments:
Post a Comment