Sunday, September 2, 2012

Kumbe jeshi la polisi lilipinga chadema kufanya mkutano leo?


 Marehemu Daud mwandishi wa Channel ten mwenye mkoba kiunoni akiwarekodi wanachama wa chadema muda mfupi kabla ya kifo chake leo alasiri.


JESHI la polisi mkoa wa Iringa limesema limezuia mikutano ya vyama vya siasa kwa vyama vyote na sio kwa chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) pekee hivyo laonya vyama vyote kutii sheria bila shuruti.

Hata hivyo jeshi hilo la Polisi limesema kuwa halifanyi kazi kwa matakwa ya chama chochote cha siasa na kuwa si kweli kama wanavyodai viongozi wa Chadema kuwa jeshi la polisi linatumiwa na chama cha mapinduzi (CCM) kuzuia mikutano hiyo.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Michael Kamuanda ametoa kauli hiyo leo ofisini kwake alipozungumza na waandisha wa habari kuhusu zuio la mkutano wa Chadema uliopangwa kuanza leo katika wilaya ya Mufindi.

" Nawatangazia wanasiasa na vyama vyote vya siasa pamoja na wananchi wa mkoa wa Iringa kuwa hakutakuwa na mikutano ya kisiasa kutokana na shughuli za sensa zinazoendelea ....hivyo basi nawaomba wananchi wote kutoshiriki mikutano yoyote ya kisiasa itakayoitishwa na wanasiasa " alisisitiza.

Kuwa mikutano hiyo imezuiliwa kwa kipindi hiki cha sensa kilichoongezwa hadi hapo tamko litakapotolewa tena na msajili wa vyama vya siasa John Tendwa kama alivyokwisha kutoa tamko la kuzuia shughuli hizo za vyama vya siasa kwa kipindi hiki cha sensa.

"Wananchi wote wa mkoa wa Iringa mnaombwa kutii sheria bila shuruti hii ni amri ....nawaombeni sana wananchi kutodanganywa na wanasiasa kwa kuvunja sheria "aliongeza kamanda huyo wa polisi.

Hata hivyo alisema kuwa kimsingi zoezi la sensa lilipaswa kuhitimishwa Septemba mosi mwaka huu ila kutokana na serikali kuongeza muda wa zoezi hilo bado jeshi hilo la polisi linazingatia maagizo ya Msajili wa vyama vya siasa kama alivyoyatoa kwa jeshi hilo.

Kamanda Kamuanda alisema kuwa jeshi hilo la polisi wala msajili wa vyama vya siasa hajazuia vyama vya siasa kuendelea na vikao vyao vya ndani kwa kipindi hiki na kuwa hata Chadema wakiwa mkoani Iringa wameendelea kufanya vikao vyao vya ndani katika kata mbali mbali za mkoa wa Iringa na hakuna mtu aliyewazuia kuendelea kufanya hivyo.

Dkt Slaa awajibu Polisi
Wakati jeshi la polisi likipinga shughuli hizo za vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara katibu mkuu wa Chadema Taifa Dkt Willbroad Slaa ameibuka na kusema kuwa chama chake kitaendelea na mikutano kama kilivyojipangia na kuwa wapo tayari kwa lolote litakalojitokeza .

Dkt Slaa alisema kuwa walivumilia mara ya kwanza walipozuiwa mikutano hiyo mkoani Iringa na kuvuta subira hadi jumamosi zoezi hilo lilipomalizika sasa anashangazwa kuona jeshi hilo likiendelea kuzuia mikutano hiyo tena.

"Tumemsikiliza kamishina wa sensa Hajati Amina Mrisho Said kuwa hadi sasa watu asilimia 95 wameandikishwa huku akiwata wale ambao bado kuwapigia simu wenyeviti wa mitaaa na vijiji ili wakaandikishwe na makarani wa sensa ....sasa jeshi la polisi linataka kutuambia kuwa hao watu asilimia 5 waliobaki wapo Iringa peke yake hadi wakazuia mikutano yetu? tunasema hatutakubali tutaendelea na mikutano yetu kama kawaida hatupotayari kabisa kusubiri hadi tarehe nane" alisema Dkt Slaa.

Pia alisema kuwa kama ni uzalendo sasa umefika kikomo na kuwa wataendelea na ratiba zao za mikutano kama ilivyopangwa na watapambana kwa lolote .

Chanzo: Francisgodwinblog ( Iringa)

No comments:

Post a Comment