Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) Dk Mary Nagu
Waandishi Wetu
MBIO za uchaguzi ndani
ya CCM zimefikia patamu, baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Uwekezaji na Uwezeshaji) Dk Mary Nagu kuenguliwa kugombea nafasi ya Ujumbe wa
Nec kupitia Wilaya ya Hanang', huku Mke wa Rais, Salma Kikwete akiwa mgombea
pekee wa nafasi hiyo Lindi Mjini.
Mkoani Dar es Salaam , mbio hizo zimeonekana kuwaweka
pabaya Mwenyekiti wa UWT wa mkoa huo Zarina Madabida na Katibu wake, Tatu
Maliaga baada ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa, John Guninita kueleza kuwa viongozi
hao watafikishwa kwenye kamati ya maadili kueleza kwa nini wamesitisha uchaguzi
wilayani Kinondoni.
Habari kutoka Hanang'
zimeeleza kuwa Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya hiyo imemwengua Dk Nagu na
kuwabakiza wagombe wawili, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Leonsi
Marmo.
Taarifa kutoka kwenye
kikao hicho kilichofanyika juzi katika Ofisi ya CCM ya wilaya hiyo na
kuhudhuriwa na wajumbe 12 zimeeleza kuwa Dk Nagu ameenguliwa kutokana na
maelezo kuwa kanuni hazimruhusu kugombea.
Chanzo cha habari
kimeeleza kuwa kanuni iliyomwondoa Dk Nagu kwenye kinyang’anyiro hicho ni ile
inayowataka viongozi wenye kazi za kila siku; ubunge na uwaziri kutogombea.
Imeelezwa kuwa jitihada
za wajumbe watano waliojipambanua katika kikao hicho kumtetea Dk Nagu ziligonga
mwamba, baada ya wenzao saba kuunga mkono uamuzi huo.
“Kikao kilikuwa kizito,
lakini tulitazama zaidi kanuni, sifa za wagombea na uwezo wa wagombea hasa
katika nafasi hii nyeti ya Nec kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015,” alisema mmoja
wa wajumbe wa kikao hicho.
Alisema mapendekezo ya
kikao hicho, tayari yamefikishwa ngazi ya CCM mkoa kwa uamuzi zaidi na baadaye
yatafikishwa Kamati Kuu (CC) ya CCM.
“Sisi tumemaliza kazi
yetu, tunaamini kuwa tumetenda haki kwa manufaa ya chama chetu Wilaya ya
Hanang’,” alisema kiongozi huyo.
Hata hivyo, mjumbe
mwingine wa kikao hicho alisema, mgawo wa mkopo wa matrekta ambao umekuwa
ukiendelea Hanang’ umechangia kumwengua waziri huyo.
“Hapa kuna mambo mengi,
nadhani hao waliokuwa na taarifa hizi, wameshindwa kueleza zaidi. Kuna mambo ya
chinichini hasa baada ya baadhi ya viongozi kutounga mkono uamuzi wa Waziri
Nagu kusaidia baadhi ya wanaCCM wakiwamo viongozi kukopeshwa matrekta,” alisema
mjumbe huyo.
Kiongozi mmoja wa CCM
Wilaya ya Hanang’ ambaye hakutaka jina lake
litajwe , alikiri kufanyika kwa kikao
hicho na kueleza kuwa tatizo la Dk Nagu ni kutoombewa kibali na kamati ya siasa
wilaya au mkoa kama kanuni zinavyotaka.
Alieleza kuwa kanuni za
CCM zinataka viongozi wenye majukumu ya kila siku kuombewa kibali kwanza na
Kamati ya Siasa ya Wilaya au Mkoa kabla ya kugombea jambo ambalo halikufanyika
kwa Dk Nagu.
“Hadi kikao hicho
kinafanyika, Dk Nagu alikuwa hajaombewa kibali hicho na hili limetokana na
migogoro ya kisiasa iliyoko wilayani Hanang’,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu hilo , Katibu wa CCM
Wilaya ya Hanang’, Allan Kingazi alisema: “Ni kweli kikao kilifanyika, lakini
mapendekezo yetu ni siri na hao waliokuambia wamekiuka kanuni. Sisi baada ya
kumaliza kikao chetu, mapendekezo yetu tumeyapeleka ngazi ya mkoa ambako pia
yataendelea kuwa siri hadi majina yatakapotangazwa rasmi,” alisema.
Uamuzi wa Dk Nagu kuamua
kugombea NEC kupambana na Sumaye ambaye ndiye alimwachia jimbo hilo , ulitabiriwa kuibua mgawanyiko mkubwa
ndani ya wana CCM wa Hanang’.
Jitihada za gazeti hili
kumpata Dk Nagu kuzungumzia uamuzi huo zilishindikana baada ya simu yake ya
mkononi kuita muda mrefu bila kupokewa.
Kuenguliwa kwa Dk Nagu
kunatokana na sababu za kuwa na kazi za muda wote kumeibua hofu kuhusu hatima
ya viongozi wengine waliochukua fomu ambao kwa mujibu wa kanuni iliyomwondoa Dk
Nagu nao hawakupaswa kugombea.
Hao ni pamoja na Mbunge
wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu),
Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George
Mkuchika na Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk Abdallah Kigoda, Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk Emmanuel Nchimbi.
Wengine ni Wabunge Deo
Filikunjombe (Ludewa), Mussa Azzan Zungu (Ilala), Dk Hamis Kigwangalla (Nzega)
na Andrew Chenge (Bariadi Magharibi).
Salma akosa mpinzani
Lindi
Katika hatua nyingine
Mke wa Rais, Salma Kikwete amerudisha fomu ya kuwania ujumbe wa Nec Taifa
kupitia Wilaya ya Lindi Mjini.
Katibu wa CCM Wilaya ya
Lindi Mjini Mohamed Kateva, alisema jana kwamba Salma ni mgombea pekee
aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo katika wilaya yake.
www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment