Thursday, September 13, 2012

Je mnamjua huyu?
PHILIP NERI NDUNGURU, MCHORA VIBONZO WA KUPIGIWA MFANO.

Unakumbuka visa vya akina Komredi Kipepe, Dr. Love Pimbi, Lodi Lofa, Ndumi la kuwili na Madenge kwenye gazeti la SANI?.

Miaka ile, katuni hizi zilikuwa maarufu kiasi kwamba baadhi ya watu walipachikwa majina ya Vibonzo hivi kama majina ya utani. Mtunzi wa Vibonzo/ katuni hizi ni marehemu Philip Ndunguru, aliyefariki mwaka 1986 akiwa na umri
wa miaka 24. Katuni zake ziliendelea kuleta tabasamu miaka kadhaa iliyofuata.

MAISHA YAKE.

Philip Neri Ndunguru alizaliwa tarehe 28 mwezi wa kwanza mwaka 1962 katika Wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma. Yeye alikuwa mtoto wa nne katika Familia ya watoto nane ya Mzee Severin Ndunguru baba na Mkewe Bibi Martha Haule.

Kipaji cha Philip kilianza kuonekana katiaka umri wa awali tu wa maisaha yake mafupi hapa duniani, akiwa na miaka miwili tu alipendelea sana kuchora vipicha vidogo vidogo kila alipopata nafasi. Mwaka 1964 Mzee Severin Ndunguru alihamia Jijini Da er salaam na familia yake kwa ajili ya Ajira yake mpya katika Kitivo cha Jiographia ya Rlimu cha Chuo Kikuu cha Dar es salaam lakini akimuacha Philip nyumbani kwao Mbinga.

Philip alidhihirisha zaidi kipaji chake katika uchoraji mwaka 1967 wakati akiwa na umri wa miaka mitano kwa kuanza kuchora picha kubwa zilizokuwa zikivutia na kuonekana vizuri, ambapo baadaye alijiunga Jijini Dar es salaam pamoja na wazazi wake ili kuanza masomo.

Alijiunga na Shule ya Msingi Forodhani ambayo wakati huo ilikuwa ikijulikana kama St. Joseph Convent School. Shuleni hapo jitihada zake katika kukiendeleza kipaji chake zilizidi maradufu na kushajiisha umahiri wake kwenue uchoraji, akawa anachora picha nzuri, za kuvutia na kuchekesha jambo ambalo lilimpa mashabiki na wafuasi katika uchoraji miongoni mwa wanafunzi wenzake.

Mwaka 1972 Philip alihamia Shule ya Msingi Chang'ombe ambapo alifanikiwa kumaliza Elimu yake ya msingi mwaka 1974 na kufanikiwa kuendelea na masomo ya Sekondari katika Shuke iliyokuwa ikiendeshwa na T.T.C Chang'ombe.

SANAA.

Mwaka 1978 mara baada ya kumaliza Elimu ya Kidato cha nne Philip aliamua kujitupa rasmi kwenye sanaa na kukataa Ajira nyengine ya aina yoyote, alijifunza na kuchapa kazi kwa juhudi kubwa kwa lengo kuu la kutafuta mafanikio kupitia kazi pekee aliyoichagua mwenyewe.

Katika harakati zake za kujiendeleza, Philip alipata bahati ya kufundishwa na kupigwa msasa juu ya sanaa ya Uchoraji na Mwalimu mmoja wa Kiholanzi, Mwalimu huyo alikuwa Nchini kwa muda wa miaka mingi nyuma akijishughulisha na ukufunzi wa mambo mbalimbali ya sanaa na alimfahamu Philip kwa kuwa aliwahi pia kumfundisha baba yake Philip juu mambo kadhaa ya sanaa.

Mholanzi huyo aliyejulikana kwa Jina la Father Vaadmeir alitokea kumhusudu sana Philip baada ya kung'amua kipaji chake adhimu katika uchoraji, alijitolea kumfundisha kila aina ya mbinu ya uchoraji na kumshajiisha kuongeza jitihada na kuzidisha ubunifu juu ya uchoraji wake, jambo ambalo Philip alilifanyia kazi na kuchangia katika Umashuhuri wake, lakini Mwalimu wake huyo alifariki muda mfupi tu mara baada ya kuanza kumfundisha Philip.

SANI, CHIMBUKO LA UMASHUHURI WAKE.

Mara baada ya kifo cha Mwalimu wake, matumaini ya Philip katika kukiendeleza kipaji chake yalififia sana. Mara nyingi alikuwa mtu asiye na furaha na mwenye mawazo kwa kupoteza mtu ambaye alimsaidia sana katika kumuongezea ujuzi na maarifa katika sanaa yake na pia kumpoteza rafiki ambaye siku zote ushauri wake wenye kutia moyo ulichochea katika utendaji kazi wake.

Wakati huo Gazeti la Sani lilikuwa linatamba sana kwa vipicha vya kuchora na ndilo lililokuwa Gazeti pekee la aina hiyo Tanzania. Philip alionana na Mhariri wa Gazeti husika ambaye alimpa nafasi ya kukidhihirisha kipaji chake na kumfanya kuwa Mchoraji Mkuu wa Gazeti hilo.

Sani walimpa Moyo sana Philip kwa kumpa vitendea kazi bora pamoja na kumuendeleza kimasomo, jambo ambalo lilianza kumpa Umashuhuri kidogo na pia kuongeza ari ya utendaji kazi wake kwa kuwa mbunifu zaidi.

Wamasa walimpeleka Philip kwa Wasanii wa Kiuta na Printpak ili kumuongezea maarifa juu ya usanii wa uchoraji na uchapaji na pia walimkabidhi Philip kwa Mchoraji Mkongwe wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam aliyejulikana kwa jina la Raza ambaye alimuimarisha katika Mpangilio wa kutumia rangi mbalimbali na kumuongezea mbinu kadhaa za Uchoraji.

Philip hakuwa mtu mvuvi katika kujiendeleza na kujitafutia maarifa zaidi juu ya kazi yake, kwa wakati wake pia alipata mafunzo kutoka kwa Mkufunzi mwengine wa Kiganda Chuo Kikuu cha Dar es salaam aitwaye Msoke, ujuzi ambao ulimkomaza sana na kumuongezea kiwangio kikubwa cha Maarifa.

KILELE CHA MAFANIKIO.

Philip alishirikiana na Mzee S. M. M. Bawji katika kutunga hadithi na uchoraji wa Picha. Hadithi yao ya CHAKA LA MAUTI iliyotoka katika Gazeti la Sani iliwapaisha sana na kuwaongezea Mashabiki. Licha ya Hadithi hiyo lakini pia ufundi na ubunifu wa hali ya juu katika Uchoraji alioutumia Philip katika Kitabu cha Kipigo cha Dunia cha Mzee Meko ulionyesha zaidi Ugwiji na kubobea kwake katika Uchoraji.

Ubunifu wake katika Vikaragosi kama Madenge, Komredi Kipepe, Pimbi, Lodilofa, Zena na Betina, Ndumilakuwili nynginezo ambazo yeye alikuwa akizichora kwa ustadi mkubwa ulimpa heshima ya kipekee miongoni mwa mashabiki wa Jarida la Sani na kumfanya kuwa Mchoraji mwenye kupendwa zaidi katika wakati wake.

UJASIRIAMALI NA MAONYESHO YA KUVUTIA.

Mwishoni mwa Mwaka 1981 kulikotea matatizo ya Karatasi za Uchapishaji Tanzania jambo ambalo lilisababisha Gazeti la Sani kusimamishwa Uchapishwaji wake. Philip akajiunga na Kampuni nyengine ya Uchapishaji iitwayo Continental Publishers kama choraji Mkuu pia, uwepo wake katika Kampuni hii uliongeza ukazidi kumpa ujuzi zaidi na uzoefu katika kuandaa Kazi za Vitabu na Uchoraji wa Majalada.

Pia katika kujiongezea kipato, Philip aliamua kuanzisha shughuli zake binafsi nyumbani za Uchoraji wa Mambo mbalimbali, Usanifu, Uharirri na Ubunifu wa aina Mbalimbali za Kalenda pamoja na kutengeneza na kubuni Nembo mbalimbali.

Katika wakati husika pamoja na kupendwa sana kwa sanaa yake ya uchoraji wa Vibonzo lakini maslahi yake yalikuwa madogo sana, jambo ambalo lilimpa kiu ya kujaribu kutaka kufanya kazi hiyo nje ya Mipaka ya Tanzania kwa lengo la kujiongezea kipaji zaidi. Kabla ya kuondoka Nchini aliandaa Maonyesho ya Michoro na kazi zake mbalimbali aliyafanya Goeth Ins, na katika Hoteli ya Forodhani, maonyesho ambayo yalivutia watu wengi sana na pia kuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa kazi zake zote zilipata wanunuzi kwenye maonyesho hayo.

NJE YA MIPAKA, BALOZI MWEMA MWENYE KUPEPERUSHA BENDERRA YA TANZANIA.

Mafanikio makubwa aliyopata kwenye Maonyesho ya Kazi zake hapa Dar se salaam yalikuwa chachu ya Kusaka fursa zaidi nje ya nchi, mwitikio ambao ulionyeshwa na mashabiki wake ulionyesha dhahiri namna alivyokubalika na kumhakikishia juu ya umaridhwawa wa Kazi zake na kuwa anaweza kupata mafanikio kokote atakapoenda.

Ziara yake ya Mwanzoni ilikuwa Nchini Zimbabwe na Sweden, ziara ambazo zilikuwa na mafanikio sana kwani muitikio na mashabiki aliojizolea katika nchi hizo ulikuwa mkubwa mno.

Kazi zake za Uchoraji wa Vibonzo mara zote zilisimama juu ya Uhalisia na Tamaduni za Kitanzania zikiwakilisha na kutoa Taswira juu ya Maisha ya Mtanzania wa kawaida jambo ambalo liliongeza sana mvuto katika kazi zake, Kiswahili fasha kilichotumika katika kazi hizo kiliitangaza zaidi Lugha yetu Mashuhuri Duniani na kumfanya awe Balozi mwema aliyeipeperusha vizuri Bendera ya Taifa letu.

Kwa kuvutiwa zaidi na Kazi zake, Taasisi na Wasanii mbalimbali wa nchi hizo walishirikiana naye na kubadilishana naye ujuzi juu ya Tasnia ya Uchoraji wa Vibonzo, jambo ambalo lilimuongezea Ujuzi na Maarifa zaidi. Mafanikio yake kiuchumi na kisanaa kwenye ziara hizo yalizidisha Umashuri wake Duniani na pia kuongeza fursa za ajira kwake nje ya Tanzania.

"KAZIBURE" NCHINI KENYA.

Ziara yake ya Mafanikio Nchini Zimbabwe na Sweden ilimfungulia milango na Fursa nyingi za ajira, mara baada ya kurejea Nchini alijiunga na Kampuni ya Kenya Times ya Jijini Nairobi nchini Kenya ambapo alikuwa Mchoro Vibonzo Mkuu wa Gazeti hilo.

Umaarufu wake nchini Kenya uliibuka muda mchache tu tangu kufika kwake kwa kuchagizwa na umahiri wake kwenye uchoraji na pia ubunifu katika kuelezea visa vya michoro yake. Kibonzo chake Maarufu cha KAZIBURE ambacho Tanzania kilijulikana kama NDUMILAKUWILI kilipata umaarufu mkubwa Nchini humo kikitumika kuwatanabaisha na kuwajulisha Wasomaji wake wa huko juu ya Mbinu mbalimbali zilizokuwa zikitumika na Matapeli katika kurubuni watu.

Pamoja na Kibonzo chake hicho kuwavutia Wakenya wengi lakini pia alichagiza katika kuongeza Misamiati ya Kiswahili kwa kuwa Jina Kazibure lilitumika kama neno rasmi la kuwakilisha matapeli kama ilivyo kwa neno Ndumilakuwili nchini Tanzania. Kwakuvutia na ufanisi wa Kazi zake Wakenya wengi walikuwa wakituma barua kumpongeza na kuwa kipenzi kikuu cha Wasomaji wa Gazeti hilo.

KIZURI CHAJIUZA.

Sanaa na Kazi za Philip ziliwakilisha Ucheshi, Mafunzo na kuelimisha sana. Busara ambayo alitumia katika kuwasilisha sanaa yake pamoja na matumizi ya Lugha nzuri, yenye staha, fasaha na rahisi kueleweka na mtu yeyote ilimuongezea Mashbiki wengi katika Jamii ya Watu wa Afrika Mashariki.

Ubunifu wake katika kubuni na kuelezea visa vya vibonzo vyake lilikuwa jambo la kuvutia sana, vibonzo vyake vikipendwa mno na watu wa rika na jinsia zote, vikiwakilisha Maisha ya Tabaka la Chini la Wananchi ( Mfano Mzee Meko, Komredi Kipepe na Betina), vikichochea udadisi na kuonyesha madhara na athari za utukutu (Madenge) na pia vikiainisha mbinu ovu za Watu wabaya na Matapeli wa Mjini (Ndumilakuwili na Kazibure).

Vibonzo vyake kama Lodilofa na Pimbi vilitoa Taswira ya watu wa Tabaka la kati la Juu na kujaribu kuainisha tabia za watu wakorofi na wakware, Dr. Love Pimbi akiwakilisha Watu wakware na Lodilofa akiwakilisha Matajiri wakorofi na wenye lugha za kuchukiza. Vibonzo vyake kama Sukununu na Mwinyi Mpeku vikisimama Juu ya Busara ya kuchochea udadisi na Hekima ya Asili katika Misemo, Nahau na Methali zetu Waswahili huku visa vya Zena na Betina vikiainisha Maisha ya Wivu na Songmbingo za Wanawake wasiopatana.

Alitoa Burudani isiyomithilika, akifunza, kufurahisha na pia kuelimisha kwa kazi zake za Sanaa. Michoro yake yenye Nakshi na yenye kuvutia kuangalia ikionyesha Umahiri na Uanazuoni wake wa hali ya juu na utunzi pamoja na uwasilishaji wa visa vya michoro yake ukiainisha namna alivyo Gwiji katika kuielezea Jamii yake.

Elimu na Busara ambazo ameacha kwa Jamii ni mchango wa kupigiwa mfano, Sanaa yake ikiwa aina madhara kwa rika na jinsia zote, na zaidi ikichochea mafunzo kwa Vijana, ikihimiza busara kwa Wazee, ikiwazindua Matajir juu ya kutumia Lugha Njema, ikiwataka Vijana Kuacha Utukutu na pia kuendeleza na kukuza Lugha adhimu ya Kiswahili.

Philip Neri Ndunguru ameacha nyuma yake urithi mzito wa sanaa na mafunzo kwa jamii.

KIFO CHA MWANAZUONI NGULI NA SHABABI CHENYE KUACHA MAJONZI MAKUU.

Tarehe 29 mwezi wa 3 mwaka 1986 saa kumi za usiku wa siku ya Jumamosi ya Sikukuu ya Pasaka ilikuwa siku ya msiba mkuu kwa wazazi, ndugu, marafiki na wasanii wengi kwa kufiwa na Mpenzi wa Waprnzt wengi Marehemu Philip Neri Ndunguru.

Kifo chake kiliwashtua wasomaji wa Kikaragosi/ Katuni yake ya KAZIBURE huko Kenya pamoja na wafanyakazi wote wa Kenya Times. Na kwa Tanzania kiliwasikitisha na kuwatia majonzi makuu wasomaji wa Gazeti la Sani na Wamasa (Waliokuwa watoaji Maandishi wa Sani).

Marehemu Philip Neri Ndunguru alizikwa tarehe 31 mwezi wa 3 mwaka huo huku salaam nyingi za Rambirambi zikimiminika kwa Gazeti la Kenya Times na pia Sani kutoka kwa Wasomaji na Mashabiki wake Duniani kote.

Hisia za Majonzi na Simanzi zilizoonyeshwa na mamia ya Waombolezaji ambao walishiriki Mazishi yake zilionyesha dhahiri Majuto yao Makuu juu ya kumpoteza Mwanataaluama huyu Nguli katika Umri wake ule mdogo wa Miaka 24.

Umati mkubwa wa Wahudhuriaji wale Msibani ukionyesha namna alivyopendwa na Jamii yake na jinsi kazi zake zilivyotangaa, ambapo huzuni zaidi kwa Mashabiki wake ilidhihirika kwa kumuona Mwanaye Mchanga tu ambaye naye aliletwa Mazishini hapo.

Mara baada ya Kifo chake Gazeti la Sani lilitangaza kutafuta Wachoraji wapya ambapo wasanii wa Michoro kama Ibra Radi Washokera, Chris Katembo na wengineo walijitokeza na kuendeleza juu ya pale alipoachia Philip.

Mola Muweza amemtwaa Philip katika Umri Mdogo tu lakini bado kayafanya Maisha yake Mafupi yenye Mafanikio na Umashuhuri wa hali ya juu kuwa ni funzo kwetu juu ya Nafasi ya kutumia vipawa vyetu katika Ulimwengu huu, Mola Amlaze Pema Bwana Mashuhuri Philip Neri Ndunguru.

Chanzo: ukurasa wa facebook ‘watanzania mashuhuri.

No comments:

Post a Comment