Sunday, September 2, 2012

Katika maisha usikate tamaa...

Ndugu zangu,

Leo nimejifunza kitu kikubwa sana katika maisha yangu, ni kuhusu kutokata tamaa kwa kitu ulichojaaliwa na Mungu. Naam mtu anaedharau kipaji chake ujue anadharau maagizo ya Mungu.

Kuna msichana anaitwa Bertha Charles, nilisoma nae darasa moja chuoni Kampala International University- Uganda.

Leo nilikuwa nikitazama kipindi cha Bongo Star Search, ni shindano la kusaka vipaji hapa Tanzania linarushwa na televisheni ya ITV. Nilishangaa sana kuona namna alivyopita kwa mzunguko wa mwisho ambao umekusanya washiriki hamsini kutoka mikoa ya Tanzania.

Yeye alishiriki kutoka Dar es Salaam ambapo kulikuwa na washiriki zaidi ya elf tano, lakini yeye amepita na kuwa miongoni mwa washiriki watano ambao wataiwakilisha Dar es Salaam, katika mzunguko wa mwisho ulioshirikisha washiriki hamsini ili wapatikane washiriki 20 watakaoingia katika kambi ya BSS wiki hii jumanne.

Nilizungumza nae leo Bertha na kunidokeza kuwa amefanikiwa kupita katika mzunguko wa mwisho uliohusisha washiriki 50 na amekuwa miongoni mwa washiriki 20 walioingia katika BSS academy, ambapo watakuwa wakiimba na kupigiwa kura.

Dada huyu mpaka ninamzungumzia katika blogu hii si kuwa nampigia kampeni ama ninaonyesha kumjua sana. Ila ni kutokana na aina ya maisha aliyopitia, tukiwa chuoni alishashiriki mara nyingi katika mashindano ya vipaji lakini hakuwahi kushinda. Na mara nyingi alikuwa akilia baada ya kushindwa. Kwakuwa tulikuwa ugenini tukawa kama kaka na dada hivyo mara nyingi sisi watanzania tuliokuwa chuoni tukawa tukimpa moyo kuendelea na sanaa ya muziki.
                                         
Hata wasanii wa Uganda wengi wanamfahamu maana katika matamasha mengi ya uimbaji alikuwa akienda na kuonyesha uwezo wake. Ametumia pesa nyingi sana katika kutimiza ndoto yake ya muziki. Lakini katika majaribio yote aliambulia patupu.

Hata juzi wakati wa shindano la ‘Tusker Project Fame’ nchini Kenya alitoka Kampala kuja kushiriki kama mshiriki kutoka Tanzania, lakini kwa bahati mbaya alichelewa maana alikuwa na matatizo ya kifamilia.

Lakini huu ni muda wake. Wacha aonyeshe kipaji dada Bertha. Na hakika jembe lenu nina bahati sana kusoma na washiriki wa bongo star search.

Maana mshiriki wa BSS ya mwaka 2008 alikuwa mwanafunzi mwenzangu TSJ, nilisoma nae darasa moja na hata wakati anakwenda kushiriki aliniaga kama kaka yake ili kupata baraka. Aliitwa Baby Madaha. Na sasa amekuwa mwanamuziki na mwanafilamu maarufu, nadhani hata dada Bertha Charles anaweza kutoboa…. Mungu msaidie.

HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM, TANZANIA
0713 593894/0752 593894
02/09/2012


No comments:

Post a Comment