Nilichojifunza mchezo wa leo
kati ya Coastal Union na Yanga uwanja wa taifa.
Ndugu zangu,
Siku zote husemwa mficha
maradhi kifo kitamuumbua, leo nimeshuhudia timu yangu ya Coastal Union
ikifungwa goli mbili moja na vijana wa jangwani. Hakuna mtu ambae alishuhudia
mechi ile ya leo na kushindwa kuwamwagia sifa vijana wa Coastal.
Hakika walicheza kandanda ya
kufurahisha sana
na ya kutia hamasa sisi washabiki kutegemea mambo mengi mazuri kwa msimu ujao
wa 2012/2013.
Kuanzia dakika ya kwanza
mpaka dakika ya thamanini vijana wa Coastal walimiliki mpira, wakatoa pasi za
uhakika na chenga zenye kuonekana kiasi mashabiki wa Yanga wakawa kimya kabisa.
Hata goli lililofungwa kipindi cha kwanza cha mchezo na Razak Khalfan, lilikuwa
la kiufundi na hata namna walivyoweza kuzuia mashambulizi ya Bahanuzi kila mtu
alifurahi.
Hata kipindi cha pili
kilipoanza bado uhai wa Coastal ulionekana hasa katika upande wa viungo na beki
zote za kulia na kushoto ingawa kulikuwa na uhai mdogo katika safu ya
umaliziaji lakini inaweza kurekebishika.
Tatizo lilikuwa kwa golikipa
wa Coastal Juma Mpongo, bado anaonekana ana wasiwasi na anapangua sana kuliko kudaka
mipira. Tatizo hili ni dogo ikiwa kocha wa magolikipa Bakari Shime, atafanya
maamuzi ya haraka lakini litakuwa kubwa kama
ataendelea namna hii katika ligi kuu.
Tuende katika mada ya msingi,
upo upinzani mkubwa katika klabu ya coastal Union iliyo na makazi yake mjini
Tanga barabara ya 11. mashabiki asilimia thamanini hawamtaki kocha, naam Juma
Mgunda kocha mkuu wa timu hiyo hatakiwi hata kidogo na mashabiki wa wagosi wa
kaya.
Na leo nimegundua makosa
mengi ya kocha huyo, timu ilikuwa katika nafasi nzuri sana ya kushinda, lakini
makosa madogomadogo yaliyotoa upenyo kwa Mbuyu Twite kupiga shuti na mchezaji
wa coastal Jamal, kujifunga kwa kichwa wakati akijaribu kuokoa hatari hiyo; yaliwapumbaza
wachezaji wa Coastal maana kwa dakika mbili walikosa nguvu hasa baada ya
kujiona wapo pungufu baada ya mchezaji mwenzao Jerry Santo kupewa kadi nyekundu
kwa kumtukana mwamuzi.
Lakini badala yake Kocha
alitakiwa kusimama na kuwaambia wachezaji wasijali kujifunga ama timu pinzani
kusawazisha ni moja ya mchezo. Lakini hakufanya hivyo bali aliendelea kukaa
katika benchi la wachezaji wa akiba bila kusema lolote. Kazi kubwa alikuwa
akifanya kocha msaidizi Habib Kondo, ambae alionekana kusimama muda wote wa
mchezo.
Kocha wa timu pinzani hakika
alionyesha uwepo wake, hakukaa hata kidogo mbali ya timu yake kuwa nyuma kwa
goli moja na kuonekana kuelemewa lakini bado alikuwa akiwapigia kelele
wachezaji wake na kuwaita kuzungumza nao kila alipopata nafasi. Hilo sikuliona kwa kocha
wetu mchezaji wa zamani wa Coastal Union Juma Mgunda.
Hakujaharibika kitu, lakini
ipo haja kukaliwa kikao kwa mashabiki wote nchi nzima kujadili suala hili.
Maana nimesikia mashabiki wa Dar es
Salaam wanamtaka kocha na mashabiki wa Tanga
hawamtaki, kwakuwa mashabiki wa Tanga ndiwo wanaokaa na wachezaji kwa muda
mwingi wanaweza kuwashawishi kwa maneno ama kuwarubuni wauze timu ili ionekane
kocha hafai. Na hii ni mbaya sana
kwa mustakabali wa klabu hasa ikizingatiwa tunaingia katika msimu mpya muda si
mrefu.
Rai yangu ni kukaliwa kikao
ambacho kitaamua nini cha kufanya maana nimesikia mpaka wiki iliyopita katika
mechi ya kirafiki baina ya Polisi Dodoma na Coastal kocha alitaka kupigwa na
mashabiki mpaka ikabidi kupewa ulinzi wa polisi.
Hatutafika popote kama
tutaendelea na msuso huu, nimeshangaa sana
timu imekuja kutoka Tanga bila viongozi wa juu wala kikundi cha ngoma ambacho
mara nyingi hujitolea kuja kwa nauli zao….. Tafakari maneno haya mpenzi wa
Coastal..
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM , TANZANIA
0713 593894/ 0752 593894
1/09/2012
No comments:
Post a Comment