Friday, August 31, 2012

Bara la Afrika lanyemelewa na njaa...


Bei ya vyakula duniani ilipanda kwa asilimia kumi mwezi Julai na kusababisha hofu ya bei ghali ya vyakula barani Afrika.
Taarifa hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na benki ya dunia.
Ripoti hiyo imesema kuwa wimbi la joto lililokumba Marekani pamoja na ukame katika baadhi ya maeneo ya Mashariki mwa Ulaya ndio chanzo kikubwa cha kupanda kwa bei hizo.
Bei ya nafaka kama vile mahindi ,ngano na maharagwe ndio ilipanda pakubwa kulingana na ripoti hiyo.
Benki hiyo sasa imeonya kuwa nchi ambazo hununua nafaka kutoka nje ndizo zitaathirika pakubwa.
Kuanzia mwezi Juni hadi Julai mwaka huu, bei ya mahindi ilipanda kwa asilimia 25 wakati bei ya maharagwe aina ya soybean ikipanda kwa asilimia 17. Ni bei ya mchele pekee ilishuka kwa asilimia nne.
Nchini Marekani, ukame ulioripotiwa na kutajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya karibuni, ulisababisha uharibifu wa mahindi na maharagwe wakati nchini Urusi, Ukraine na Kazakhstan, ngano iliharibika sana.
Benki ya dunia pia imesema kuwa hatua ya kutumia mahindi kuzalisha mafuta inawezekana ni mojawapo ya sababu ya kupanda kwa bei ya mahindi nchini Marekani.
Nchi hiyo hutumia aslimia arobaini ya zao lake la mahindi kutengeza mafuta yanayotokana na mimea.
Kwa jumla, ripoti ya benki ya dunia kuhusu bei ya vyakula ambayo hufanyia utafiti bei ya vyakula duniani, iligundua kuwa bei ilipanda kwa asilimia sita zaidi mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana.
Chanzo: BBC Swahili.

No comments:

Post a Comment