SENSA ya Watu na Makazi
jana iliingia siku yake ya pili, huku kasoro kadhaa ikiwamo ukosefu wa vifaa,
upungufu wa makarani na watu kugoma kuhesabiwa vikiripotiwa.Katika baadhi ya
maeneo hadi jana, wananchi walikuwa hawajaanza kuhesabiwa kwa kile kilichoelezwa
kuwa ni kutokana na ukosefu wa vifaa na makarani.
Ofisa Uhamasishaji wa
Sensa Taifa, Said Ameir alikiri kupata taarifa za kasoro hizo lakini akaeleza
kushangazwa na chanzo chake, akisema: “Vifaa tulivigawa maeneo mbalimbali
nchini kulingana na mahitaji. Tunashangazwa na taarifa hizo kwamba hata wengine
wamekosa reflector (makoti ya kuakisi mwanga) na vitambulisho.”
“Tunachofanya sasa ni
kuchunguza tatizo hilo
limeanzia wapi na limesababishwa na nini. Vilevile tunajitahidi kuhakikisha
kuwa vifaa hivyo vinapelekwa sehemu hizo ili kazi hiyo iendelee kama kawaida.”
Alisema pamoja na kasoro
hizo, kazi hiyo inaendelea vizuri na itakamilika ndani ya siku saba kama ilivyopangwa.
Kasoro
Baadhi ya makarani wa
Kata ya Ubungo wamesema baadhi ya wajumbe wa nyumba kumi wamekataa kushirikiana
nao.
Mratibu Msaidizi wa Sensa
kata hiyo, Pertronia Lyamuya alisema tatizo jingine ni baadhi ya waumini wa
Kiislamu kugoma kuhesabiwa kama ilivyokuwa kwa baadhi ya wakazi wa Kinondoni
Shamba, Dar es Salaam .
Katika baadhi ya maeneo,
makarani, walilazimika kutumia polisi kutekeleza majukumu yao . Baadhi ya mitaa ambayo polisi walitumika
ni Juhudi, Kingugi na Kiburugwa iliyoko Temeke. Mitaa hiyo ilikuwa imebandikwa
matangazo ya kuwahamasisha watu wasishiriki Sensa.
Ofisa Mtendaji wa Kata
ya Kiburugwa, Engerasia Lyimo alisema kazi ya kuhesabu watu ilisimama kwa muda
kusubiri polisi wa kuwasindikiza makarani hao kwenye nyumba hizo ili kulinda
usalama wao.
Lyimo alisema katika
Mtaa wa Kingugi, alijitokeza mjumbe wa shina wa CCM (jina tunalo),ambaye
aliwahamasisha wakazi wa eneo lake
wasijitokeze kuhesabiwa.
Mwenyekiti wa Serikali
ya Mtaa wa Basihaya, Kinondoni, Daniel Aron alisema kaya nane zilikataa
kuhesabiwa kwa maelezo kwamba hazioni umuhimu wake. Alisema baada ya tukio hilo alitoa taarifa Ofisi
ya Kata ya Boko.
Alisema kimsingi, changamoto
kubwa katika eneo lake
ni uchache wa vifaa kiasi
cha makarani kushindwa kuanza kazi hiyo.
Msimamizi wa Kata ya
Buguruni, Wilaya ya Ilala, Stella Mshana amesema kuwa baadhi ya watu wamekataa
kuhesabiwa, wengine kutokana na imani za kidini na wengine kwa kutoelewa
umuhimu wake.
“Maeneo ya Mnyamani
tumekutana na vikwazo lakini kusema ukweli idadi yao ni ndogo kuliko wanaotupa ushirikiano.
Unaweza ukakuta labda katika watu sabini, mmoja ndiye anakataa,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Said Meck Sadiki amesema Serikali itaendelea kupambana na kundi la watu
wanaojihusisha na kusambaza ujumbe wa kupinga kushiriki Sensa.
Alisema jana kwamba hadi
sasa Polisi inawashikilia watu wanne kutoka Wilaya za Temeke na Kinondoni....
“Kijana mmoja alijulikana kwa jina la Yusuph Ernest alikamatwa akisambaza
ujumbe huo maeneo ya Magomeni Kagera.”
Arusha
Watu wasiojulikana, juzi
walibandika mabango yanayowazuia makarani wa Sensa kutekeleza wajibu wao katika
Kata za Ngarenaro na Unga Ltd. Mabango hayo yalibandikwa katika eneo la Daraja
la Ngarenaro.Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo pamoja na Mratibu wa Sensa
Mkoa wa Arusha, Magreth Martin walisema hadi jana hakukuwa na tukio la
kukwamisha Sensa licha ya kuwapo kwa tukio hilo.
“Nawashukuru sana
wananchi wa Arusha kwa kushiriki vyema Sensa katika siku hizi mbili za mwanzo
baada ya kuelimishwa na kuelezwa umuhimu wake kwa mipango ya Serikali na
maendeleo ya taifa licha kuwapo baadhi ya watu waliojaribu kuwashawishi
kususia.”
Tanga
Mkuu wa Wilaya ya
Muheza, Subira Mgalu na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Ibrahim
Matovu wamewaagiza makarani wa Sensa kwenda kuwahesabu wanawake ambao waume zao
wanadaiwa kukimbilia kusikojulikana kukwepa kuhesabiwa.Walitoa amri hiyo baada
ya kuripotiwa kuwa baadhi ya Waislamu wa Kijiji cha Kigombe, Muheza,
wamekimbilia porini kukwepa kuhesabiwa.
Inadaiwa kuwa baadhi ya
wanaume waliondoka na kutoa amri kwa wake zao kutohesabiwa vinginevyo wangepewa
talaka.Kaimu
Mtendaji wa Kijiji cha Kigombe, Mashauri Kanyama alisema tatizo hilo
limesababisha baadhi ya makarani kushindwa kutekeleza kazi zao kikamilifu.
Ofisa Mtendaji wa Kata
ya Kigombe, Mohamedi Hatibu alisema baadhi ya wakuu wa kaya wametishia pia
kuwapa talaka wake zao iwapo watahesabiwa.
No comments:
Post a Comment