Saturday, August 25, 2012

Ndugu zangu, Mambo ya sensa haya...

Huyu ni karani wa sensa alijitambulisha kwa jina moja tu la Othman, akiwa maeneo ya magomeni mapipa akichukua taarifa za wakazi wa kaya hii ambao hawakutaka kujitambulisha.

Huyu ni mtaa wa idirisa Magomeni Mapipa Dar es Salaam. Makarani wa sensa wakiwa kazini. Hawataki mchezo.

Katika hili nina cha kugusia kidogo, kutokana na hotuba aliyoitoa Mh Rais Kikwete jana nimeona hakuna haja ya kulumbana na Seriikali katika mambo ambayo kimsingi yataathiri vizazi vyetu.

Waislamu wamepanga kususia sensa ya kuhesabu watu na makazi, sababu ni kutowekwa kipengele cha dini katika dodoso la sensa. Kwa maana wanadai wamepuuzwa kwa kutosikilizwa walichokitaka.

Leo katika ukurasa wangu wa facebook nimeandika neno la leo kama ilivyo ada, na leo nimeandika neno zito kidogo. 'Kuwa mpuuzi ni kutorekebisha ujinga wako'

Ujinga si tusi, bali ni kutokuwa na elimu juu ya masuala fulani, lakini ujinga ukiendelea kwa muda mrefu unakuwa ni upuuzi, na mwenye kumiliki ujinga huo nae anabadilika jina kutoka mjinga mpaka mpuuzi.

Mpuuzi kwa lugha ya kiswahili cha kawaida ni mtu anaepuuza kila anachokiona, kawaida ubongo wa binaadamu umejawa na udadisi, kadiri unavyodadisi mambo kwa wingi inaonyesha ni namna gani ubongo wako unafanya kazi vizuri na kwa ufanisi.

Hivyo nataka kuwaambia waislamu wenzangu 'naomba nikiri au wazungu wanaita ku-declare interest' kuwa nami ni muislamu na hata rais wetu ni Muislamu.

Hivyo suala la kusema tunasusa sensa ni upuuzi, tunaahirisha matatizo badala ya kuyatatua sasa. Yatakuja kuwasumbua ndugu zetu. Udini hauna nafasi Tanzania ni nia njema tu iliyofanya watangulizi wa taifa hili kupinga udini.

Tukishajijua idadi yetu waislam itatusaidia nini katika kufanya ibada. Waache watu washerehekee idadi ya uongo wanayoitangaza, lakini kawaida mtu anaposherehekea idadi ya uongo katika mapambano hana anachoficha zaidi ya kuhadaa nafsi yake. Kushituka kwetu ni ushindi kwao. Lazima kuzingatia hili.

Hivyo nawaasa waislamu kuacha kuwa wapuuzi bali tufikiri kama tulivyoagizwa na Mtume wetu Mohammed SAW. Ambae amesifiwa kwa hekima.

HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM, TANZANIA
0713 593894/ 0752 593894
kidojembe@gmail.com
26/08/2012

No comments:

Post a Comment