Kumekuwepo na taarifa tofauti kuhusu kuanza kwa Ligi Kuu ya Bara ambayo kwa mujibu wa kalenda ya Shughuli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), inatakiwa kuanza Septemba 01, 2012. Baada ya kikao cha pamoja baina ya TFF na viongozi wa klabu za Ligi Kuu kilichofanyika Jumatatu ya Agosti 20, 2012 kwenye ofisi za TFF, TFF inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao:
1. Baada ya kikao cha pamoja baina ya TFF, Kamati ya Ligi na viongozi wa klabu zote za Ligi Kuu, ilionekana kuwa kutokana na kutokamilika kwa mazungumzo baina ya TFF/Kamati ya Ligi na mdhamini wa sasa, yaani Vodacom, mwanzo wa Ligi Kuu unatarajiwa kuwa Septemba 15, 2012. Hii inatokana na ukweli kwamba kukamilika kwa mazungumzo baina ya pande husika, ndio kutatoa picha halisi ya Ligi Kuu ya msimu ujao.
2. Mazungumzo baina ya TFF/Kamati ya Ligi na Vodacom yanatarajiwa kukamilika mwishoni mwa wiki hii kwa kuwa yameshafikia hatua nzuri na hivyo mkataba unaweza kusainiwa wakati wowote baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo.
3. Kukamilika kwa mazungumzo hayo ni muhimu kwa kuwa kutasaidia Ligi Kuu kuanza bila ya matatizo yoyote kwa klabu zinazoshiriki, TFF na Kamati ya Ligi hasa kutokana na ukweli kuwa baadhi ya mambo yatakayokubaliwa yatalazimika kuingizwa kwenye Kanuni za Ligi; yatasaidia upatikanaji wa fedha kwa muda muafaka; upatikanaji wa vifaa kwa muda muafaka na masuala mengine muhimu.
4. Ratiba ya Ligi Kuu sasa inatarajiwa kutangazwa mapema wiki ijayo pamoja na tarehe rasmi ya kuanza kwa Ligi Kuu
5. Kutokana na kusogwezwa mbele kwa tarehe ya kuanza kwa Ligi Kuu, mchezo wa Ngao ya Jamii baina ya mabingwa wa Tanzania Bara na washindi wa pili, nao sasa utapangiwa tarehe nyingine ambayo ni wiki moja kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu. Kwa maana hiyo mchezo huo utachezwa katika siku itakayotangazwa baadaye.
6. Kuhusu chombo kitakachoongoza Ligi Kuu, TFF ilitoa mapendekezo ya Kamati ya Utendaji kwa Kamati ya Ligi na baadaye kwa viongozi wa klabu za Ligi Kuu kuhusu muundo wa chombo hicho kulingana na mwongozo wa Katiba ya Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) na Katiba ya TFF na suala hilo kwa sasa linajadiliwa na klabu za Ligi Kuu kwa ajili ya hatua za mwisho.
Imetolewa Agosti 21, 2012 na
Angetile Osiah
Katibu Mkuu wa TFF
No comments:
Post a Comment